ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 7, 2013

WAMAREKANI KUSAIDIA UJENZI WA CHUO CHA UUGUZI KARAGWE

Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akizungumza na ujumbe ulioongozwa na Professa Evene Estwick ( kushoto kwa Balozi) kutoka Chuo Kikuu cha Wilkes ( Marekani) ambacho kinaushirikiano na Hospitapi ya Nyakahanga iliyopo Wilayani Karagwe Mkoani Kagera wengine ni Dkt. Andrew Cesari aliyeketi kulia kwa Balozi ambaye ni Msimamizi wa Hospitali hiyo na anayefuatia ni Afisa Ubalozi, Bw. Khamis akifuatilia mazungumzo hayo aidha katika mazungumzo hayo yupo pia Dkt. Andrew Mayala ambaye ni Medical Officer wa Wilaya ya Karagwe na Bi. Lorienetter Williams ambeye ni mwanafunzi kutoka Chuo cha Wilkes
Balozi Manongi akiwa na Professa Estwick ambaye chuo chake kinauhusiano na ushirikiano na hospitali ya Nyakahanga, uhusiano huo unaokaribia miaka kumi na tatu sasa unahusisha utoaji wa misaada mbalimbali ikiwamo ya vifaa vya hospitali, usomeshaji wa watoto yatima na ujenzi wa Chuo cha Uuguzi ( Nursing Collage) kulia kwa Balozi ni Bi. Williams ambaye ni mwanafunzi kutoka chuo hicho.
Balozi Tuvako Manongi akiwa na Madaktari Andrew Cesari na Andrew Mayala kutoka Karagwe ambao walikuwapo nchini Marakani kwa ziara ya kikazi kwa mwaliko wa wenyeji wako Chuo Kikuu cha Wilkes kupitia mpango wa kubadilishana wataalam. wakiwa hapa Marekani pamoja na mambo mengine walishiriki katika makongamano ya kitaaluma ambapo walibadilishana mawazo na uzoefu na wenyeji wao kuhusu namna wanavyokabilliana na changamoto zitokanazo na maradhi ya ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya.


 Wilaya ya Karagwe  iliyopo katika Mkoa wa Kagera nchini Tanzania,   inatarajiwa kuwa na Chuo cha kwanza cha aina yake  katikafani ya Uuguzi ( Nursing Collage )kitakachojengwa kwa misaada na ushirikiano kutoka   Chuo Kikuu cha Wilkes  kilichopo  katika mji wa Pennyslavia, nchini Marekani.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa  wiki na   Professa  Evene Estwick  wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na  Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi. Mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Uwakilishi huo jijini New York.
Akiwa  ameambatana na Dkt. Andrew Cesari ( MD, MBA) ambaye ni  msimamizi wa Mganga  wa   Hospitali  Teule ya Nyakahanga wilayani  Karagwe ambako chuo hicho kitajengwa , Professa Estwick alimweleza  Balozi   Manongi kwamba   Chuo hicho  kinatarajiwa kuwa tayari mwishoni mwa mwaka ujao na kwamba michoro tayari imeshakamilika.

Aidha  ilibainishwa katika mazungumzo hayo kwamba, wataalamu  wawili katika fani ya uuguzi wanatarajiwa kwenda mwakani  huko Karagwe kwa lengo la  kuangalia namna  bora zaidi ya  kushirikiana  katika eneo hilo.
Katika mazugumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Dkt. Andrew  Mayala ( MD, MPH) ambaye ni Medical Officer wa    Wilaya ya Karagwe na  Bi. Lorienetter Williams ambaye ni Mwanafunzi kutoka  chuo hicho,  ilielezwa kwamba ujenzi wa Chuo hicho cha Uuguzi  unatokana na uhusiano na  ushirikiano wa  takribani miaka  kumi na tatu  uliopo kati ya  Chuo Kikuu cha Wilkes na Hospitali ya Nyakahanga.  
Kwa mujibu wa Dkt Andrew Cesari ambaye ndiye mwanzilishi wa fikra hiyo ya kuwa na  Chuo cha Uunguzi, alisema kwa kuanzia chuo kitakuwa kinatoa mafunzo ya uuguzi, lakini  lengo ni kukipanua kwa kuongeza fani mbalimbali ili kuwapata wataalamu wengi Zaidi.
“Nilipofika  Wilayani Karagwe mwaka 2007, nilikuta wilaya  hii ingawa ni kati ya wilaya kongwe nchini, ikiwa haina  chuo  cha aina yoyote  hata cha VETA, ndipo likanijiwa wazo la kubuni mradi huu, na bahati nzuri  marafiki zetu wameonyesha nia ya kutusaidia kufikia lengo hili na mambo  yote yakienda sawa ujenzi wa chuo utaanza mwakani”.
Akielezea umuhimu wa   Chuo hicho, Dkt. Andrew  Cesari anasema manufaa hayatakuwa kwa kuzalisha  wataalamu  wengi katika  eneo la afya, lakini  kitakuwa na  manufaa makubwa kwa vijana wengi  hasa wale wanaomaliza elimu  na kushindwa nini cha kufanya au wapi pa kwenda hasa katika maeneo hayo na ya  jirani.
Kwa hiyo   itakuwa  ni fursa nzuri  kwa vijana wengi kujipatia  ujuzi zaidi na kupanua huduma na raslimali watu katika eneo hilo la afya. Anasema Dkt.  Cesari
Dkt.  Cesari  na Dkt.   Mayala walikuwa hapa  Marekani kwa mwaliko wa washirika wao yaani  Chuo Kikuu cha Wilkes kupitia  utaratibu wa kubadilishana wataalamu (exchange program) na wameshiriki katika mijadala mbalimbali ya kitaalam ukiwamo ule  uliofanyika katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo walipata fursa ya kuelezea uzoefu wao na kubadilishana mawazo na washiriki wengine na pia walifanya ziara katika  Chuo  kijulikanacho kama Commonwealth Medical  Collage kilichopo Scranton.
Ushirikiano kati ya  Chuo Kikuu hicho na Hospitali ya  Karagwe  ulilanza kwa utekelezi wa milady midogo     ukiwamo ule wa  upelekezaji wa  vifaa vya hospitali,  ubadilishanaji wa wataalamu na kuwasaidia watoto  yatima  wanne ambao  wamepoteza wazazi wao  kutokana na  maradhi ya  ukimwi.
Watoto hao wanne  husaidiwa ada na gharama nyingine za shule vikiwamo vitabu kupitia mradi ujulikanao kama “Embrace a Child.”   Mradi unao  ratibiwa na  Chuo hicho. 
Na cha kutia  moyo zaidi ni kwamba wanafunzi hao akiwamo  Kihinga George   wanafanya vizuri  kiasi cha kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha sita na matarajio yake ni kuwa daktari.
“  maendeleo ya watoto hawa ni  kati ya hadithi nzuri za  ushirikiano wetu, ni watoto wenye akili sana, wanaojituma na walio makini. Tunaona matunda yake, hasa kwa kuzingatia kwamba  watoto hawa walikuwa hawana msaada wowote tangu wakiwa wadogo” anasema  Dr. Evene Estwick kwa furaha kubwa.
 Kama hiyo haitoshi, gharama za kuwasomesha yatima hao zikiwamo za ada na  vitabu  zinatokana na michango  ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Wilkes kupitia harambee wanazozifanya  wao wenyewe.
Kwa upande wake,  Balozi Tuvako Manongi, alielezea kufurahishwa kwake na uhusiano  uliopo  baina  ya  Chuo Kikuu cha Wilkes na Hospitali ya  Nyakahanga na kwamba ni jambo linalotakiwa kuenziwa na kudumishwa.
Akasema Serikali inathamini na kutambua mchango wa wadau mbali mbali katika kuchagiza juhudi za serikali za kufikisha huduma za afya karibu na wananchi.  Kama  sehemu ya  utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ( MDGs) ambayo ufanikishwaji wake   wake unahitaji sana ushirikiano kati ya serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi.
Akabainisha kwamba  uboreshaji wa sekta ya afya ni moja ya vipaumbele  vya Serikali na hasa katika uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto na kwamba ujenzi wa  Chuo cha Uuguzi  siyo tu utakuwa unachagia juhudi hizo za serikali bali pia ni ukombozi mkubwa kwa wananchi  kutokana na upungufu mkubwa wa wataalamu.
Aidha Balozi Manongi akasema inatia faraja sana kwamba watoto yatima ambao  wanasaidiwa  kupitia ushirikiano huo wanafanya  vizuri  sana katika masomo yao na ni kielelezo kizuri kuwa michango inayotolewa na wahisani  inawafikia  na kuwanufaisha walengwa na akatoa  shukrani zake kwa walimu na wanafunzi kwa moyo wao huo wa kujitolea.

No comments: