Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Chaguzi za udiwani katika kata 27 uliofanyika jana katika maeneo tofauti ulitawaliwa na matukio mabaya yakiwamo ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi, huku mbunge mmoja akicharangwa mapanga na kukimbizwa hospitalini kupatiwa huduma.
Katika kata ya Sombetini, jijini Arusha, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walirusha mabomu ya machozi kutuliza vurugu za watu waliokuwa wakimbia ovyo katika kata hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya watu wenye mapanga waliokuwa wanamsaka Diwani wa Kata ya Engutoto (Chadema), Elibariki Male, kwa lengo la kumkamata na kumshambulia.
Male alinusurika kuuawa, baada ya yeye pamoja na wenzake kuamua kulilinda gari walilolishuku kuwa na mapanga na silaha za moto.
Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser (hard top) lenye namba za usajili T 399 BFE, lilikuwa limeegeshwa nje ya kuingilia kituo cha ofisi ya kata hiyo, ambako kulikuwa na vituo 34 vya kupigia kura.
Aliyeegesha gari hilo hakufahamika mara moja, ingawa baadhi ya watu walidai kuwa alikuwa ni dereva wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza baadaye, Male alisema wakati wakilinda gari hilo, kundi la watu wachache lilitoka na kuanza kuwafukuza.
“Nilikimbia. Ilikuwa ni hatari sana kwangu ningeweza kufa leo. Nashukuru Mungu kwa sababu asubuhi nilienda kumuomba Mungu kanisani. Kama sikufa leo (jana) nadhani sitaweza kufa hivi karibuni,” alisema Male.
Male ambaye alikuwa amevaa kaunda suti, alisema alikimbia mita kadhaa kuokoa maisha yake na kulazimika kuingia ndani ya ofisi za CCM za kata hiyo, ambako kulikuwa salama yake.
Hatua ya diwani huyo kufukuzwa, iliamsha watu wengi kukimbia na hivyo, polisi kulazimika kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya.
Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) ya Arusha, Muroto alimtuma askari mmoja baadaye kwenda ofisi ya CCM kuangalia kama kulikuwa na mtu amejificha humo.
WENGI WAJITOKEZA KUPIGA KURA
Pamoja na yote hayo kutokea, mamia ya watu walizidi kuongezeka eneo la kupiga kura.
LEMA, WENZAKE WALISHUKU GARI
Awali, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, na wenzake alimweleza OCD kuhusu shaka yao juu ya gari hilo.
Baadaye gari hilo lililokuwa na vioo vya giza (tinted) lilitolewa eneo hilo na dereva anayedaiwa kuwa polisi.
Gari hilo lilisindikizwa na magari mawili yaliyojaa askari wa FFU hadi makao makuu ya kikosi hicho Mkoa wa Arusha, Mbauda. Baadaye, hali ya utulivu ilirejea
GARI LATUMIKA KUWASOMBA WANAWAKE KUPIGA KURA
Kabla ya hapo, ilizuka vurugu kati ya Lema, aliyekuwa pamoja na baadhi ya viongozi wa Chadema na wanachama kadhaa wa chama hicho.
Vurugu hizo zilizuka wakati Lema na viongozi hao wa Chadema walipoingia katika eneo la kupiga kura wakitumia gari ya wazi aina ya Suzuki lenye namba ya usajili T 439 CBN.
Baada ya kuteremka kwenye gari hilo, Lema na wenzake walimwendea Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Gilles Muroto, na kumtaka amwondoe mtu mmoja aliyekuwa akiwasaidia wanawake kwenda kupiga kura.
Mtu huyo aliyetambulika kuwa ni Katibu wa CCM Kata hiyo, Gerald Munisi, ambaye alidaiwa kutumia gari lake aina ya Toyota lenye namba za usajili T 751 ALY kwenda kuwachukua wanawake katika maeneo ya mbali na kuwapeleka kupiga kura.
Hali hiyo ilisababisha kuzuka hali ya kutoelewana na kumfanya Lema na viongozi hao wa Chadema kumtaka OCD kumwondoa kada huyo.
“Anafanya nini hapa tangu asubuhi? Aondoke. Hatukubali. Aondoke. Mbona sisi umetuondoa na huyu amebaki anafanya nini?” alihoji.
Hali hiyo iliwalazimu polisi waliokuwa wakiongozwa na OCD Muroto kumtaka aondoke eneo hilo ili kurejesha amani na ndipo kada huyo alipoingia kwenye gari lake akiwa na akina mama na kuondoka. Baada ya kuondoka hali ya utulivu ilirejea.
LEMA, CHATANDA WATAMBIANA
Mapema jana asubuhi, Lema na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda walirushiana tambo, katika eneo la kupigia kura, hali iliyomfanya Muroto kuwafukuza wote eneo hilo. Katika tambo hizo, Lema na Chatanda walirushiana maneno ambayo kimaadili hayaandikiki gazetini, huku kila mmoja kumtambia mwenzake akidai kuwa atashinda uchaguzi huo.
Tukio hilo lilitokea nje ya ofisi ya kata hiyo, iliyopo eneo la Mbauda Sokoni, majira ya saa 2:00 asubuhi kabla ya tukio hilo, wawili hao walikutana katika eneo hilo na kusalimiana kwa kukumbatiana.
Lakini baada ya muda mfupi walipokutana tena eneo hilo, Lema alimweleza Chatanda, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kutoka Mkoa wa Tanga, kuwa hadi ikifika jioni atakuwa amemshinda. Wabunge hao walizozana kwa maneno na ishara zinazoonyesha mambo yasiyoandikika.
OCD AWAFUKUZA LEMA, CHATANDA
Kutokana na hali hiyo, OCD Muroto aliwafukuza wote katika eneo la kupigia kura.
OCD Muroto alianza kufanya hivyo kwa Lema kwa kumuamuru kuondoka eneo hilo na baadaye akafanya hivyo kwa Chatanda.
Wabunge hao wakiwa na wapambe wao walikuwa wakizunguka hapa na pale kwenye eneo la kupigia kura na hivyo kuvuta watu wengi.
“Lema na wenzako ondokeni eneo hili…Chatanda ukiondoka hapa utakuwa umenisaidia sana,” alisema OCD Muroto na wabunge hao walitii na kuondoka.
Akizungumzia na NIPASHE baadaye, OCD Muroto alisema alilazimika kuwafukuza wabunge hao eneo hilo kutokana na ukweli kwamba, uwapo wao ulikuwa ukivuta watu wengi kujazana katika eneo hilo bila sababu za msingi.
“Tunawaondoa watu ambao wakionekana hapa wanasababisha watu wengine kujazana hapa bila sababu,” alisema OCD Muroto.
VITUO VYAFUNGULIWA KWA WAKATI
Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji, Namnyaki Laitetei, alisema vituo vyote katika kata hiyo vilifunguliwa kwa wakati na hapakuwa na tatizo la kuchelewa kwa vifaa vya uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kulikuwa na changamoto kidogo kwa upande wa wapigakura.
KADI ZA KUPIGA KURA ZINA WALAKINI
Alisema baadhi walikuwa na kadi, lakini namba za kadi zao zilikuwa zikitofautiana na zile zilizokuwa zimeandikwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
“Kulikuwa na changamoto ndogo ndogo, kama vile baadhi ya wapigakura namba za kadi zao zilikuwa zikitofautiana na zile za kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Hii imesababishwa na baadhi yao kuwa waliandikishwa mwaka 2005, lakini wakapoteza kadi na walipoandikishwa tena 2010 namba zao zilikuwa bado hazijarekebishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema Laitetei.
NEC YATAFUTA UFUMBUZI
Alisema hata hivyo, timu ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, walikuwapo wakitafuta ufumbuzi wa matatizo hayo na kwamba wote walisaidiwa.
ZOEZI LAENDA VIZURI
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Chale Sanai, alisema hali ya upigaji kura ilikuwa ikiendelea vizuri.
Mpambano wa kugombea udiwani katika kata hiyo upo kwa Ally Bananga (Chadema), David Mollel (CCM) na Ally Mkali wa CUF.
Ulinzi mkali wa polisi waliovaa kiraia na sare, wakiwamo FFU uliimarishwa katika maeneo yote ya kupigia kura.
Baadhi ya watu, ambao hawakuwa wakipiga kura hawakuruhusiwa kukaa ndani ya mita 100 kutoka eneo la kupiga kura.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
duh! Ukisoma hii habari unajuwa wazi CCM kiwisney mpaka inatumia mapanga? Alafu eti police wametumia mabom ya machozi kutawanya watu au wakikuwa wanawatisha? Sababu kwanini hawakulikamata Ilo gari lenye tint badala Yake walilisindikiza na dereva wa Ilo gari lenye mapanga ni police CCM HACHENI KUUWA.
Luka sijachafuwa Hali ya hewa chanzo ni nipashe na tunawashukuru sisi tulio ughaibuni basi utaona watu waliopoteza mda wao huku wanaifagilia CCM sababu maisha yamewashinda mchweeeeee.
Post a Comment