ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 10, 2014

UNYENYEKEVU KWA MWENZI WAKO NI UTUMWA?-2

MARAFIKI Ijumaa ijayo itakuwa ni Sikukuu ya Wapendanao. Naamini kuna mengi mmepanga kwa ajili ya wenzi wenu, ni jambo zuri hakika. Hapa kwenye Let’s Talk About Love nimewaandalia zawadi nzuri sana ambayo nitawapatia wiki ijayo.

Hebu sasa tumalizie mada yetu. Msingi wa mada hii ni unyenyekevu kwa mwenzi wako. Je, ni utumwa? Tumeona mengi wiki iliyopita, ambapo niliishia kwenye kipengele cha uvumilivu.

Ndugu zangu, katika ndoa utakutana na matabaka mengi, watu hutofautiana tabia, mfano wewe ni mwanamke umeolewa, mumeo akaamua kuishi na dada zake yaani wifi zako, unatakiwa kuwasoma tabia ili uendana nao.

Lazima uwe na busara, uvumilivu, unyenyekevu na kuonyesha kuwajali, hii inaweza kukusaidia sana kwani watakapokutendea mambo ya ajabu nawe ukaanza kuwaropokea matusi, utakuwa unajiingiza kwenye migogoro ambayo mwisho wake huweza kuwa mbaya zaidi kwako kuliko kwao.

Kama wakikukosea, endelea kuwa na ukarimu wako lakini usiwe mkorofi. Zungumza ukweli na mumeo na umweleze kwa sauti ya taratibu kabisa.

Usimwambie kwa kauli kali au kuonyesha nia ya kutaka waondoke nyumbani kwenu.
Mweleze ukweli kwa utaratibu, kwa sababu si kawaida yako kuwa mkorofi, bila shaka atakuelewa na atazungumza na ndugu zake.

Huo ndiyo uvumilivu ninaouzungumzia, siku zote wewe ndiye unayetakiwa kuwa na uchungu na ndoa yako.

Kabla ya kuzungumza jambo lolote fikiria mara mbili, halitasababisha matatizo kwako? Ukipata matatizo au kuachika huyo wifi yako atakuwepo? Jibu ni hapana!

Utakaporudishwa nyumbani kwenu, utawaangaliaje wazazi wako ambao walikulea katika malezi mazuri na kukufunda vyema? Ni nini kama siyo aibu mtoto wa kike utakuwa umewapelekea wazee wako?

UNYENYEKEVU JE?
Sawa kabisa! Sasa kama usipomnyenyekea laazizi wako, ambaye mwenyewe ulikubali kuwa naye na kufunga naye ndoa unataka umnyenyekee nani? Mumeo/mkeo ndiyo wa kumnyenyekea siku zote za uhai wako.

Lazima uwe na kauli ya huba iliyojaa ukarimu. Ndoa kubembelezana bwana, mpenzio akija na mawazo yake, mtu amemuudhi kazini, kwako ndiyo mahali haswa anapopaswa kunyenyekewa na kupewa raha.

Wewe ndiye mganga wake wa kweli wa kumwondoa stress zote anazokumbana nazo siku nzima. Acha kujidanganya kwamba, kumnyenyekea ni utumwa, ni wajibu wa kila mmoja katika ndoa kuhakikisha anamshika mwenzake sawasawa!

Wewe ndiye unapaswa kumsahaulisha kabisa mambo yote mabaya anayokumbana nayo katika maisha yake.
Mpokee kwa upole, mwambie pole, mkaribishe chumbani kisha mvue nguo zake na umpeleke bafuni mwenyewe.

Anza kumwogesha bila kuzungumza naye maneno mengi. Tumia dodoki au kitambaa laini kumsafisha ngozi ya mwili wake.

Baada ya hapo mkaushe kwa taulo laini kisha mrudishe chumbani, mpe nguo za usiku kisha mpeleke mezani kwa ajili ya chakula. Hapo sasa utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumwuliza kuhusu mabadiliko uliyomwona nayo siku hiyo.

Lazima atakuwa mkweli kwako. Kumbuka kwa mapokezi mazuri uliyompa, atakuwa mpole na mnyenyekevu.

Atasema kinachomtesa lakini kubwa zaidi ni kwamba utakuwa umesaidia kumuondoa kwenye mawazo aliyokuja nayo nyumbani.

Bado unaendelea kuamini unyenyekevu ni utumwa? Badili fikra zako ndugu yangu. Usisahau wiki ijayo nina zawadi nzuri sana ya Valentine’s Day. Ni hapa hapa, USIKOSE!



Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano na Maisha anayeandikia Magazeti ya Global Publishers.
Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: