Wiki iliyopita nilieleza kuwa, ili kujiweka mbali na upweke ni pamoja na kujijali kwa maana ya usafi na mambo mengine. Siyo lazima wakati wote uwe safi kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ngumu ambazo mazingira yake lazima anakuwa mchafu, lakini baada ya kazi unapaswa kuwa nadhifu mbele za watu.
Upande wa wasichana siyo lazima uweke nywele dawa au usuke rasta wakati vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza kusuka nywele zako vizuri au wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakutafsirisha vibaya kwa jamii.
Anza kujipenda kabla ya kuhitaji upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.
UNATAKIWA KUJIAMINI
Kukosa kujiamini ni tatizo lingine la kisaikolojia. Kuna baadhi ya watu hawajiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa akijitoa kasoro.
Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi; kwamba hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo. Mwingine hujiona kuwa ana kasoro nyingi kiasi kwamba hawezi hata kuolewa!
Nani amekuambia kuwa una kasoro ndugu yangu? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo, amini Mungu ana makusudi yake kukuumba ulivyo.
Kujitoa kasoro na kutojiamni ni kosa baya kwa kuwa unajiathiri kisaikolojia na mwisho wake utajiona hufai au huna bahati hivyo kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi, jambo ambalo si sahihi.
Huyo utakayemkimbilia kwa lengo la lengo la kujitoa nuksi, hatakuwa na mapenzi na wewe, akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya kujipenda wewe mwenyewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine sasa anaweza akajitokeza mtu akupendaye kwa dhati.
Ndugu yangu, kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo.
Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe tu!
Baada ya kukuomba muwe pamoja kimapenzi unatakiwa kumchunguza kwanza na hata baada ya kumchunguza usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi. Starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako.
Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati. Hapo sasa upweke utakuwa umeondoka moyoni mwako. Bila shaka tumeelewa. Ahsanteni sana marafiki. Hadi wiki ijayo katika mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano na Maisha anayeandikia magazeti ya Global Publishers.
No comments:
Post a Comment