Anza Siku njema na NENO la MUNGU kila siku kwa kutembelea Ibada ya Kiswahili website na Ukurasa wa Ibada ya Kiswahili kwenye Facebook.
** ** ** ** www.iykcolumbus.org ** ** ** **
Kwa maana nimemwambia (Eli) ya kwamba,nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua:kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. 14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli,ya kwamba uovu wa nyumba y Eli hautasafishika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.
TAFAKARI: Eli alikuwa mcha Mungu na Kuhani mkuu katika Hekalu la Bwana. Eli alikuwa na watoto wawili Hofni na Fineasi. Sifa mbaya za hawa wototo zilienea katika mji walipoishi. Walikuwa wananyanyasa waumini wakienda kuabudu na kutoa sadaka. Baba yao Eli alijua habari hizo za sifa mbaya za watoto wake lakini hakufanya lolote kuwazuia. Hiki kitendo cha kutowazuia watoto wake kutenda maovu kilimchukiza sana Mungu. Ndipo Mungu kupitia kwa mtumishi wake Samweli akatoa adhabu kali sana kwa Eli na familia yake.
Mara nyingi wazazi wanashindwa kuwalea watoto wao katika njia ambazo zinampendeza Mungu. Wanawaachia watoto wanakuwa vituko, wanakuwa wezi, wanakuwa hawaheshimu watu. Maandiko matakatifu katika kitabu hiki cha Samweli wa kwanza yanatuonya kwamba hukumu ya Mungu itatuangukia sisi wazazi pamoja na watoto wetu kama hatutachukua hatua zinazostahili kurekebisha watoto wetu. Wazazi wengi wanashindwa kuwarekebisha watoto wao tangu wakiwa wadogo, kitu ambacho kinapelekea kuwa vigumu sana kuwarekebisha wakishakuwa wakubwa. Ukiendelea kusoma mistari ya mbele katika kitabu hiki cha 1 Samweli utakuta kuwa Hofni na Fineasi waliuawa siku moja wote wawili na baba yao Eli alifariki baadaye. Wazazi hamtaweza kujitenga na uovu wa vizazi vyenu. Ni vema kumuomba Mungu aibariki familia ya kila mmoja wetu ili nyumba zetu zikuwe katika mazingira ya kumpenda bwana Yesu. Luka 6:43, Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya,wala mti mbaya uzaao matunda mazuri.
SALA:Mwenyezi Mungu tunakuja kwako na watoto wetu na wazazi wetu na vyote vilivyo ndani ya nyumba zetu. Tunakuomba utupe busara za kuweza kuwalea watoto wetu katika mwenendo wa kukupenda na kukutumikia wewe. Utusamehe pale tunapokosea. Roho wako mtakatifu akae ndani yetu Milele. Amen. © IYK_NENO

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake