Dar es Salaam. Katiba ya Simba imekwama kupita kwa Msajili wa Vyama vya Michezo baada ya kuwa na upungufu kidogo wa kisheria.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo alisema katiba hiyo haijapita kwa vile kuna makosa ambayo wameyabaini, hata hivyo hakutaka kuyaweka wazi makosa hayo.
“Katiba tumeirudisha Simba waifanyie marekebisho upya na kurekebisha yale ambayo tumeyaona yataleta mkanganyiko katika masuala ya kisheria, hatutaki kuingia kwenye malumbano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),” alisema Thadeo.
Thadeo alisema wamemaliza mchakato wa kuipitia katiba hiyo ya Simba juzi na kubaini mapungufu hayo ambayo yanakinzana na katiba ya TFF, hivyo kuipitisha katiba hiyo kutaleta mkanganyiko wa kisheria.
“Kamwe hatuwezi kwenda kinyume na Katiba mama ya TFF ambayo inawaongoza, kilichomo kwenye Katiba ya TFF ndicho kinachotakiwa kiwemo kwenye katiba za klabu zote za soka labda TFF wawe wamebadilisha Katiba yao,” alisema Thadeo huku akigoma kuzungumzia upungufu hayo.
Katiba ya Simba ilifanyiwa marekebisho katika Mkutano Mkuu uliofanyika Machi 16 mwaka huu na kurekebishwa baadhi ya vipengele lakini baada ya kuipelekea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), shirikisho hilo liliyakataa mapendekezo ya mabadiliko ya kipengele namba 26 cha Katiba hiyo yaliyotaka kuruhusiwa kugombea kwa mtu aliyewahi kufungwa jela.
TFF iliyakataa mapendekezo hayo kwa maelezo kuwa yanapingana na kipengele namba 29 (4) cha Katiba ya shirikisho hilo na kutaka kipengele cha awali kibaki kama kilivyo. Mabadiliko mengine yalibarikiwa kupita.
Hata hivyo, Thadeo alipoulizwa iwapo ni kipengele hicho kilichowazuia kuipitisha, alisema: “Upungufu uliopo ni kidogo na mengine ni makosa ya kiuandishi tu, ni lazima iwe na usahihi ili ilete maana, wakiyafanyia marekebisho na tukaridhika nayo basi tutawarudishia hata siku hiyohiyo waendelee na mchakato. Kuwahi au kuchelewa itategemea na wenyewe Simba.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Simba, Ezekiel Kamwaga ambaye alikabidhiwa katiba hiyo jana, alisema: “Ninachoweza kusema katiba yetu haijapita, tunaenda kufanyia marekebisho kama tulivyoelekezwa kwa vile kesho (leo ) ni sikukuu basi Ijumaa tutairudisha upya ikishindikana Jumatatu.”
Klabu ya Simba inatarajia kufanya uchaguzi mkuu baada ya uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kumaliza muda wao mwezi ujao.
Hata hivyo, uchaguzi huo bado haujatangazwa rasmi na Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwanasheria Damas Ndumbaro kwa sababu ya kusubiri kupitishwa kwanza kwa Katiba yao mpya na ofisi ya msajili ili kuweka hadharani mchakato kamili wa kinyang’anyiro hicho.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment