Upande wa mashitaka katika kesi ya kuingiza nchini vipimo bandia vya
kupima virusi vya UKIMWI (HIV), umeiomba Mahakama kwenda kumsomea
mashitaka nyumbani Mkurugenzi wa Operesheni Kanda ya Kaskazini wa Bohari
ya Dawa (MSD), Sylvester Matandiko.
Wakili kutoka Taasisisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Leonard, Swai alitoa ombi hilo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuwa mshitakiwa huyo anaumwa kiharusi.
Mbali na Matandiko, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, ambaye pia ni Meneja wa Viwango, Sadiki Materu na wasajili kutoka Bodi ya Maabara za Afya, Zainabu Mfaume na Joseph Nchimbi. Washitakiwa wengine walishasomewa mashitaka yao.
Awali, walipofikishwa mahakamani hapo, washitakiwa watatu walisomewa mashitaka, lakini Matandiko hakufika mahakamani. Wakili Swai alidai jana kuwa aliwasiliana na mke wa mshitakiwa, ambaye alimueleza kuwa Matandiko anaumwa na hawezi kutembea kwa umbali mrefu. Kutokana na hali ya mshitakiwa huyo, anaiomba Mahakama ihamie nyumbani kwake kwa muda na kumsomea mashitaka mshitakiwa huyo.
Upande wa utetezi walidai kuwa walipata taarifa kuwa mshitakiwa ana kiharusi na kuiomba Mahakama wakati inamsomea mashitaka, waangalie hali ya afya yake.
Hakimu Mkazi, Hellen Liwa hakujibu maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Mei 30, mwaka huu, itakapotajwa tena.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka saba: Ya kula njama, kutumia madaraka vibaya, kuingiza vipimo bandia vya HIV na kusababisha hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni tatu.
Matandiko anadaiwa Februari 3, 2012, katika ofisi za MSD wilayani Temeke, Dar es Salaam, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuruhusu Bodi ya Maabara za Afya kutoa kibali kwa Kampuni ya SD Africa, kuingiza vitendanishi bandia vya HIV SD Bioline ½ 3.0 vilivyotengenezwa na Kampuni ya Standard Diagnostics ya Korea, vilivyozuiliwa na Serikali kuingizwa nchini hivyo kusababisha hasara hiyo
No comments:
Post a Comment