
Pombe Haramu au Chang'aa kama inavyojulikana nchini Kenya
Watu zaidi ya hamsini na tano wamefariki katika maeneo mbali mbali nchini Kenya baada ya kunywa pombe 'haramu'.
Maeneo hayo yako katika mkoa wa kati na katika eneo la Mashariki mwa Kenya.
Vifo hivyo vilitokea kuanzia
Jumapili siku ambayo watu zaidi ya miamoja walibugia pombe haramu
inayosemekana ilikuwa imechanganywa na kemikali aina ya
Methanol ambayo
ni sumu kwa mwili.
Maeneo hayo ni pamoja na majimbo ya Kiambu
ambako watu 15 wamefariki, Jimbo la Embu Mashariki mwa nchi ambako
wengine zaidi ya 20 wamefariki. Katika majimbo ya Kitui na Makueni
mashariki mwa Kenya watu 20 wameripotiwa kufariki.
Inaarifiwa wengine zaidi ya miamoja wamelazwa
hospitalini baada ya kubugia pombe hiyo haramu siku ya Jumapili, baadhi
wakiwa katika hali mahututi huku wengine wakiwa wamepoteza uwezo wao wa
kuona.
Watu hao inashukiwa walikunywa mvinyo ambao
ulikuwa umechanganywa na kemikali ya Methanol. Mwanamume mmoja ambaye
alienda ulevini na mkewe alisema kuwa mke wake alianza kwa kupoteza
uwezo wake wa kuona na kisha kufariki muda mfupi baadaye.
Wengi waliofikishwa hospitalini walikuwa
wanaumwa na tumbo, wanahisi kisunzi na kuumwa na kichwa. Wengine
walifikishwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi na kufariki
wakipokea matibabu.
Shirika la kupambana na utumiaji wa pombe na
madawa ya kulevya, NACADA limesema kuwa wale waliohusika katika uuzaji
na usambaji wa pombe hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Vita dhidi ya pombe haramu nchini Kenya vimekuwa
vigumu kushinda kwani watu wenye kipato cha chini huchagua kutumia
pombe ya bei nafuu ambayo huwa sio pombe halali na kukabiliwa na hatari
kama hizi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake