ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 9, 2014

Utekwaji wa Wasichana Nigeria…..Wapi Sauti ya Waafrika?

Na Mwandishi wetu
Walio wengi tumesikia na kusikitiswa na habari za utekwaji  wa wasichana wanafunzi nchi Nigeria. Wengi tunakubaliana kwamba ni jambo baya, la kusikitisha  na inabidi likemewe kwa nguvu zote. Tukiendelea kufuatiliana kwa karibu suala hilo kupitia  vyombo vya habari mbali mbali, tunaona juhudi zinazofanywa ili kuwanusuru wasichana hao kutoka mikononi mwa waliowashikilia yaani kikundi cha Boko Haram.
Juhudi nyingi zinafanywa na mataifa yaliyopo nje ya Afrika tumesikia Rais wa Marekani Baraka Obama akituma kikosi cha wataalamu wa Kijeshi  na wataalamu wa utafiti katika mambo ya utekaji. Tumesikia China nao wametuma wataalamu wao kwenda Nigeria, tumesikia waziri mkuu wa Uingereza David Cameroon akitoa msimamo wake kuhusu kukamatwa waliowateka na kutokomeza kabisa kikundi cha Boko Haram
Zaidi tumeshuhudia  maadamano makubwa katika miji mbali mbali nchini Marekani, Uingerereza na Nageria watu wakitoa hisia zao kuhusu kurudishwa kwa hao wasichana. Kweli dunia yote imeamuka kuhusu suala hili. Jambo ambalo ni zuri kuona dunia inalipa kipaombele na kuliongelea kwa namna ya pekee hasa kwenye hizo nchi za dunia ya kwanza.
Tumeshuhudia mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama amebeba bango lililoandikwa “Bring Back Our Girls” na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mama Hillary Clinton ameungana na dunia nzima kupaza sauti akiomba wasichana warudishwe.

Bahati mbaya sisi ambao tunakaa na hawa (wazungu) ambao kama nilivyowaeleza jinsi walivyoonesha kuguswa na jambo hili, hapa wanatuuliza  uko wapi msimamo wa waafrika katika jambo hili. Ni swali ambalo najaribu kulipoza kidogo kwani nikiliuliza kama walio wengi wanavyoliuliza wengine mtatamani kurusha ngumi. Swali hili lina ukweli kwa asilimia kubwa tu kadiri ya muono wangu.
Kwanza kabisa tuanze na Nigeria yenyewe, juzi tumeshuhudia Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan akiomba msaada kutoka Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibu hakutaja nchi yeyote ya Afrika. Kipi kinachoendelea kichwani mwake, ni kwamba msaada daima utoka Magharibu na kwa suala hili ni lazima nchi za magharibi zipewe namba moja.Hii hali imeendelea kuitesa Afrika miaka nenda rudi. Kabla ya Rais wa Nigeria kuomba msaada kutoka Magharibi Rais wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa naye Ikulu ya Nigeria, na baadhi ya Marais wa Afrika wapo Nigeria kwa Mkutano Mkuu wa Kiuchumi. Lakini ni nchi za Magharibi zinazopewa kipaumbele.
Pili  ni asili ya tatizo lenyewe, watekaji ambao ni kikundi cha Boko Haramu chini ya kiongozi wao Abubakar Shekahu wamekuwa wakipinga kila kitu chenye viashilia vya Kimagharibu hasa vile vinavyoshikamana na utamaduni wa magharibu. Katika hali hiyo Boko Haram wanasema na elimu ina viashiria vya Magharibi. Na sasa tunawaleta watu wa Magharibi ndio waje kuwaambia kwamba lazima mfuate mambo yetu kwa nguvu. Na Rais wa Nigeria kasema wazi kwamba huu ndio utakuwa mwisho wa Boko Haram. Yahani mwisho wao ni mpaka wateke Wasichana? Kuna watu wengi wameuwawa Nigeria na hakuna mtu aliyeangazia suala hilo mpaka nchi za magaharibi zilipolishupalia.
Kwa hili waafrika tuna maswali mengi ya kujiuliza na kubwa zaidi ni  kwamba ‘tutaendelea kutegemea usaidizi wa Magharibi mpaka lini?’ je sisi wenyewe tunaaaminiana? Tutajenga uwezo lini wa kutatua matatizo yetu wenyewe. Haya mambo si mageni sana ndugu zangu, watu wanaoishi katika nchi za magharibu wanayajua haya, mwafrika anaweza kuona ugumu wa kukueleza kitu wewe mwaafika mwenzake na akaona ni rahisi kumweleza mzungu, wakati mzungu hawezi hata siku moja kufanya hivyo. Tatizo ndugu zangu waafrika lipo wapi?

Sisi ni mashuhuda siku ya Sherehe za Muunganao ncini Tanzania, jeshi letu lilionesha ukuaji na uwezo mkubwa, sio kwamba uwezo hatunao bali kujiamini na kuondoa dhana ya utegemezi. Angalau jana vikundi vya kupigania haki za bibadamu nchini Kenya vililifanya maandamano mpaka ubalozi wa Nigeria nchini Kenya na kutoa hisia zao. Lakini wapi viongozi wetu wa Afrika jamani? Jambo hili limetokea Nigeria na kesho laweza kutokea Tanzania, Uganda, Malawi, Zambia, Kenya, Rwanda je tutaendelea kuomba msaada wa kijeshi waafrika? 

No comments: