Friday, June 27, 2014

Raia Oman mbaroni kwa dawa za kulevya

Wakati jana ilikuwa siku ya kupinga dawa za kulevya duniani, Mtanzania mwenye asili ya Oman, Hafidh Hamood Al Ghfri (37) ametiwa mbaroni na maofisa usalama wa Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroine kete 21 amezificha sehemu za siri.

Mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa na dawa hizo zenye thamani ya mamilioni ya fedha, alitaka kuwahongwa maofisa wa uwanja huo kiasi cha Sh.milioni 20 pamoja na gari ili waweze kumuachia na kutomkabidhi kwa askari polisi.

Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na dawa za kulevya nchini, Godfrey Nzowa alithibitishwa kukamatwa kwa mtu huyo jana saa 5:00 asubuhi.

Maofisa usalama wa JNIA waliiambia NIPASHE eneo la tukio kuwa Ghafri, alikamatwa wakati akitaka kusafiri kwa ndege ya Shirika la ndege la Qatar kwenda Muscat kupitia Doha.

”Maofisa usalama wa kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere walimgundua abiria huyo aliyekuwa amevalia kanzu nyeupe wakati wa ukaguzi wa kawaida akiwa ameficha dawa za kulevya sehemu za siri,” alisema ofisa mmoja.

Alisema mtu huyo baada ya kukamatwa alikiri pia kuwa alikuwa amemeza kete nyingine nne tumboni huku akiwashawishi maofisa usalama wa uwanja huo kuwapatia Sh. milioni 20 na gari ili wasimkabidhi kwa askari polisi.

Kwa mujibu wa maofisa hao, Ghafri alikuwa anatokea Dar es Salaam kuelekea Muscat na kwamba dawa hizo zilikuwa zikitokea nchini.

Hadi NIPASHE linaondoka katika uwanja huo, mtuhumiwa huyo alikuwa akiendelea kushikiliwa katika kituo cha Polisi kilichoko kiwanjani hapo.

Kukamatwa kwa mtu huyo kumekuja siku mbili tu tangu Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kueleza kuwa vijana 65 wa Tanzania wamehukumiwa adhabu ya kifo nchini China baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Lukuvi alisema vijana hao ni kati ya zaidi ya vijana 403 wa Tanzania wanaoshikiliwa katika nchi mbalimbali duniani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo.

Akizungumzia maandalizi ya siku ya maadhimisho ya kupinga dawa za kulevya mjini Dodoma Jumanne wiki hii mjini Dodoma,, Lukuvi alisema tangu mwaka 2008 kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wenye asili ya Kitanzania kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Alisema idadi yao ni kubwa kiasi cha kufikia zaidi ya vijana 400 wanashikiliwa katika nchi mbalimbali ambazo pia adhabu zao zinatofautiana kulingana na sheria za nchi hizo.

Alizitaja baadhi ya nchi ambako vijana hao wanashikiliwa kuwa ni Brazil (108), Hong Kong (118), Kenya (34), Pakistan (16) na China 65.Nyingine ni Japan (7), Malawi (5), Uganda (3), Uswisi (2), Marekani (2), Uturuki (1), Botswana (5) na Msumbiji (1).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake