Kwanza niwashukuru wasomaji wangu ambao wamekuwa wakinipongeza kutokana na yale ambayo nimekuwa nikiyaandika kupitia safu hii. Mmoja wa wasomaji hao ni Nasra wa Kilombero ambaye ni mfanyabiashara.
Kwa nini nimpe shukrani za kipekee? Hivi karibuni alinipigia simu na kuniambia: “Nakushukuru, mada zako zimenisaidia sana, nimekuwa nikifanyia kazi unayoandika na hakika maisha yangu yamebadilika, asante na Mungu akubariki.”
Ni ushuhuda mfupi lakini mzito. Kikubwa ni wewe pia kufanyia kazi yale ninayoandika, naamini kwa kufanya hivyo utakuwa na maisha mazuri na mafanikio yatakuwa hayachezi mbali na wewe.
Baada ya kusema hayo nigeukie mada yangu la wiki hii. Ndugu zangu, huko mtaani wapo watu ambao wanafikiria sana kuhusu maisha yao ya baadaye. Hilo siyo jambo baya hata kidogo.
Ndiyo maana tunasoma ili tuje kuwa na maisha mazuri baadaye, tunawapeleka shule watoto wetu ili kesho na keshokutwa waweze kuajiriwa au kujiajiri na kuyaendesha maisha yao vizuri.
Pia huwa tunalimbikiza pesa zetu benki ili tuje kujenga nyumba nzuri, tununue magari ya kifahari pamoja na kufanya mambo makubwa baadaye.
Sioni tatizo katika hayo na ndiyo maana nilishawahi kuandika makala kwamba, unapopata pesa usizitumbue, fikiria pia na maisha yako ya baadaye.
Lakini sasa jambo ambalo leo nimeona ni vyema nikalizungumzia ni hili la baadhi ya watu kujinyima sana ili kujiandalia maisha mazuri ya baadaye.
Utakubaliana na mimi kwamba, wapo watu ambao licha ya kuwa na vipato vizuri wanaishi maisha kifukara sana. Ukiwauliza watakuambia wanabania pesa zao ili waje kuzifanyia mambo makubwa baadaye.
Hivi kweli inaingia akilini pesa unazo kisha uishi maisha ya kujinyima kwa ajili ya kuja kuzifanyia mambo makubwa baadaye? Una uhakika gani wa kuiona kesho?
Mimi nadhani mpaka kufikia hatua ya kuanza kufikiria maisha yako ya kesho, hakikisha kwanza leo unaishi maisha mazuri.
Unakula vizuri, unakaa pazuri, unaendesha gari zuri, watoto wako wanapata elimu nzuri kisha ziada inayopatikana ndiyo ufikirie maisha ya baadaye. Sisemi uzitumbue ovyo, zitumie kwa mpangilio.
Nasema hivyo kwa kuwa, unapowekeza pesa zako benki kisha ukaishi maisha yasiyo na nyuma wala mbele, kwanza watu watakushangaa lakini pili unaweza kujikuta unaondoka duniani na kuwaacha ndugu zako wakizitumbua bila mpangalio kwa kuwa, hawakusumbuka kuzipata.
Katika kumalizia naomba nimtolee mfano jamaa mmoja ambaye alikuwa mpangaji mwenzangu.
Nisingependa kumtaja jina ila kwa sasa ni marehemu.
Jamaa alikuwa akifanya biashara katika Soko la Tandale jijini Dar. Alikuwa akiijua pesa kiasi kwamba alikuwa mbahili wa kupitiliza.
Wanaye kuna wakati walikuwa wakifukuzwa shule kwa sababu ya ada, mke wake nimewahi kumsikia akilalamikia maisha duni wanayoishi.
Katika kufuatilia nikagundua kumbe jamaa anajenga. Lilikuwa si lengo baya lakini ujenzi huo ulimfanya aishi maisha ya kifukara sana licha ya pesa alizokuwa nazo.
Kilichotokea ni kwamba, wakati ile nyumba ipo katikati akafariki dunia na kuiacha familia yake kwenye wakati mgumu. Hilo ni fundisho kwetu!
GPL
3 comments:
You nailed it.
Nikiongeza kiduchu kuna wale ambao wananjinyima ili wasomeshe watoto shule za academia ya bei mbaya. Mtu mwenye mshahara wa milioni moja anapeleka mtoto shule ya milioni tano kwa mwaka, anabaki kapanga chumba na sebule. mlo mara moja na nusu kwa siku.
Kama mtoto angeenda shule ya laki tano, familia ingeweza kujimudu na kuwa na furaha na kaakiba kangepatikana. au siyo?
Kama msanii wa masuala ya fedha, nimevutiwa na habari hii nikitaka kujua mapendekezo ambayo mwandishi atatoa kwa jamii wanaosoma blog hii. Uandishi wako umelenga kwa mfanyabiashara ambaye alifariki huku akiwa amejinyima raha ya maisha kutokana na kujibana kimatumizi. Labda hujamaliza habari yako , suali langu ukijaaliwa kuishi maisha marefu na kuishiwa nguvu ya kufanya kazi ningeomba nijue pendekezo lako.
Labda nimsaidie mto mada, hakuna na maana ponda mali kufa kwaja. NO maana yake ni mpangilio wa kipato. Usijinyime saana ila usiponde mali ukapitiliza. Kwa mfano hapo juu kama kipato kinatosha badala ya kuishi chumba kimoja na familia kwa miaka kumi ili ujenge nyumba, basi panga vyumba vitatu na ujenge kwa miaka 15. Ukisema unabana matumizi kwa jumla kudunduliza ili umalizie nyumba yako, huku wote mnalala chumba kimoja, hakuna privacy, hakuna furaha mapenzi kwa mwezio yatapungua kwa kukosa faragha. Watoto hawana raha. Kuangalia world cup mpaka uende kwa jirani basi inakuwa taabu. Je Mwenyezi Mungu akikuchukua kabla ya kumalizia hiyo nyumba? Ni muhimu kuwa na bajeti kiasi kadhaa unaweka kaakiba. Kila mwenye unachanga changa basi ujenzi unaendelea. Kujenga kusikukoseshe usingizi. Kweli wenzio wamejenga. Rafiki yako ana ghorofa. Lakini unajua vipato vyao vinatoka wapi? Furahia maisha sasa unavyoweza. Ukiwa na uwezo wa kuitoa familia out mara moja kwa mwezi supa huo ndio uwezo wako. Kama watoto wanapata uniform mpya kila temu ndio uwezo wako ila ukijipinda sana ili ufanikishe jambo fulani hakikisha hau sacrifice maisha ya leo. Remember today is the present. You have it. Nitakupa mfano wa dada yangu mmoja alitaka sana asome apate digrii kwasababu hakufanikiwa alipomaliza form six. Ana kazi serikalini inalipa vya kutosha, ana mume na wachache wanaomtegemea. Dada huyu alipata Certificate alipomaliza akaenda Diploma. Kumaliza sasa ameanza Digrii kwenye chuo fulani cha Private. Tatizo wakati anapigania Digrii umri unakwenda anakaribia miaka Arobaini, Mwenyezi Mungu hajamjaalia mtoto bado, nyumbani mume na nduguze wameanza maneno. Nyumba inavamiwa na wageni kila kukicha kwa sababu mwenye nyumba hayupo. Huyu dada atapata Digrii baada ya miaka 4. Ila akiisha ipata atagundua haibadilishi sana maisha yake. Labda atapata furaha ila kazini atafanya shughuli ile ile mshahara labda utaongezeka kidogo. Ila yale aliyoya postpone miaka nane anapotafuta elimu hawezi kuyakamilisha kwani umri ukienda majukumu yanabadilika. Naona niishie hapa.
Post a Comment