Baadhi ya wanaharakati ngazi ya jamii wakielezea mafanikio ya utafiti wa kiragibishi unaofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika maeneo yao ulivyokuwa chachu ya baadhi ya mabadiliko kwenye mkutano jijini Dar es Salaam.
WANAHARAKATI ngazi ya jamii kutoka mikoa ya Morogoro, Shinyanga, Mbeya, Mara na Jijini Dar es Salaam wamesema utafiti wa kiraghbishi unaofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika maeneo yao unaleta mafanikio kwani changamoto zinazoibuliwa katika maeneo ya utafiti baadhi zimeaza kufanyiwa kazi.
Kuanzia Machi 9 hadi 31, mwaka huu TGNP Mtandao iliendesha utafiti wa kiragibishi kwa kuishirikisha jamii katika kata tano za Mondo (Shinyanga), Tembela (Mbeya), Kiroka (Morogoro), Nyamaraga (Mara) na Kata ya Mabibo ya jijini Dar es Salaam ambapo jamii iliibua kero katika maeneo yao na kupaza sauti kwa mamlaka husika kuchochea mabadiliko.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwanaharakati ngazi ya jamii, Leah Peter kutoka Kata ya Mondo, Wilaya ya Kishapu kwa niaba ya wenzake alisema kero lilizoibuliwa katika utafiti baadhi zimeanza kushughulikiwa na mamlaka husika.
Bi. Peter alisema eneo lao wakati unaendeshwa utafiti wananchi walilalamikia kitendo cha wajawazito wanaohudumiwa katika Zahanati ya Mondo, wilayani Kishapu kulipishwa shilingi 500 kulipia kadi ambayo imeandikwa ‘haiuzwi’ kitendo ambacho kwa sasa hakifanyiki tena baada ya kupaza sauti.
Mmoja wa washiriki wa semina ya kutathimini utafiti wa kiragibishi uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika baadhi ya kata za mikoa ya Morogoro, Shinyanga, Mbeya, Mara na Jijini Dar es Salaam akichangia mada. Semina hiyo ya mrejesho ilishirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini na asasi binafsi.
Mmoja wa washiriki wa semina ya kutathimini utafiti wa kiragibishi uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika baadhi ya kata za mikoa ya Morogoro, Shinyanga, Mbeya, Mara na Jijini Dar es Salaam akichangia mada. Semina hiyo ya mrejesho ilishirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini na asasi binafsi.
“…Eneo letu awali wajawazito katika Zahanati ya Mondo tulikuwa tukidaiwa shilingi 500 kulipia kadi ya kliniki ambayo ina maandishi ya ‘haiuzwi’ kitendo hiki kwa sasa hakifanyiki tena na kila muhudumu wa zahanati hiyo kawa mlinzi wa mwenzake hili tunajivunia,” alisema Bi. Peter.
Alisema mabadiliko mengine ni pamoja na mikutano ya mapoto na matumizi ya vijiji kufanyika jambao ambalo walililalamikia wananchi kuwa lilikuwa halifanyiki, alisema huduma za maji ambazo ni kero eneo hilo kwa sasa halmashauri imeleta shirika linaloendelea na maandalizi ya kuchimba visima vya maji katika shule za msingi Kabila na Buganika. Alisema na Shule ya Msingi Mwigumbi imepata madawati jambo ambalo lilikuwa kero.
Kwa upande wake Bi. Neofita Kunambi kutoka Mtaa wa Azimio Mabibo jijini Dar es Salaam alisema kero ya ngoza maarufu kwa jina la ‘vigodoro’ zimepigwa marufuku eneo lao baada ya kulalamikiwa, huku amri ya wajawazito wanaojifungulia katika Hospitali ya Parestina kutakiwa kwenda na ndoo ya kubeba kondo la uzazi ikipigwa marufuku jambo ambalo liliibuka katika utafiti ragibishi eneo hilo.
Aidha alisema wanajamii eneo hilo pia walilalamikia kupanda kwa bei za maji huku kila muuzaji akiuza bei atakayo kero ambayo imeanza kusikika kwani sasa bei zimepungua tofauti na ilivyokuwa awali. “…Maji eneo letu kila muuzaji alikuwa na bei yake lakini sasa imeshuka waliokuwa wakiuza miambili ndoo sasa wanauza 100, hili pia lililalamikiwa na wananchi kwenye utafiti,” alisema Bi. Kunambi.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya mafanikio ya utafiti huo Kata ya Nyamaraga mkoani Mara imefanikiwa kupaza sauti kupinga zoezi la bomoabomoa iliyotaka kutekelezwa eneo hilo bila wahusika kulipwa haki zao, huku wananchi wa Kata ya Mondo Kishapu kuandamana wakati wa ziara ya Waziri wa Maji eneo hilo kudai maji safi na salama.
Taarifa ilifafanua kuwa Kata ya Kiroka utafiti umesaidia watendaji wa huduma ya afya kuwajibika na kuwasikiliza wananchi na suala la kero ya upatikanaji wa dawa imebadilika tofauti na ilivyokuwa awali. TGNP Mtandao imewakutanisha baadhi ya wanaharakati ngazi ya jamii kutuka maeneo ya utafiti jijini Dar es Salaa ili kwa pamoja kutathimini matokeo ya utafiti huo na kuwashirikisha kutoa mapendekezo na mikakati ya kufanya kwa jamii ili kuchochea mabadiliko zaidi.
Credit:full Shangwe
No comments:
Post a Comment