Advertisements

Sunday, July 20, 2014

Neema ya gesi sasa yaonyesha mwanga

Yapo matukio mengi yaliyojitokeza tangu nchi hii ilipopata uhakika wa kuwako kwa gesi nyingi huko Mtwara, baadhi walibeza kuwa gesi hiyo haipo bali ni kiini macho tu, wakati wengine waliitaka gesi hiyo iwanufaishe wananchi wa huko kwanza kabla haijasafirishwa nje ya mikoa ya Mtwara na Lindi.

Kila mtu anakumbuka fujo zilizojitokeza ambazo zilisababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya mikoa hiyo pamoja na uharibifu mkubwa wa mali kwa kuchomewa majengo mbalimbali pamoja na vitendo viovu vya wizi wa mali za serikali na watu binafsi.

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo akiambatana na Balozi wa China nchini Dk. Lu Youging hivi karibuni walifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi linalotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa Watanzania.

Imeelezwa kwamba mradi wa ujenzi wa bomba la gesi utakapokamilika, utachangia kuiingiza nchi kuwa kati ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Balozi wa China Youging aliongea na waandishi wa habari na kusema ziara ya kukagua bomba la gesi walioifanya na Prof. Muhongo, ililenga kuhakikisha kazi inayoendelea kufanyika ipo katika kiwango cha ubora na katika viwango vinavyotakiwa na kuifanya nchi yake kuwa sehemu ya mradi na maendeleo ya nchi.

Katika hatua za ujenzi wa bomba kama iliyofikiwa, tayari wananchi wa Lindi na Mtwara wameshaanza kunufaika kutokana na kupatiwa ajira, kuboreka kwa huduma za jamii, na pia wamepewa kipaumbele katika masuala ya elimu nk.

Hadi kufikia hatua hiyo, Prof. Muhongo aliwaeleza wananchi wa Mtwara kuwa wasitegemee manufaa ya kuwapo kwa rasilimali ya gesi kwamba kutatoa fursa kwao kugawiwa fedha.

Aidha Prof. Muhongo aliwataka wananchi kujiendeleza kielimu na kutumia fursa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo ili waweze kujikwamua kimaisha na kunufaika na gesi iliyogundulika katika eneo lao.

Mhandisi anayesimamia ujenzi wa bomba hilo, Balthazar Mrosso alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 70 na maeneo yaliyosalia ni yale yanayohitaji umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na maeneo yanayoathiriwa na mafuriko pemnbezoni mwa mto Ruvu.

Tunaamini kuwa hatua zote za utekelezaji wa mradi huu zinahitaji nguvu kazi ya rasilimali watu, na hiyo ni fursa kubwa ya ajira kwa wananchi. Mradi huu utakuwa wa kudumu, na ndiyo maana fursa ya elimu imetolewa kwa wananchi wa mikoa hiyo ili elimu watakayoipata iweze kuwasaidia kwa ajira za muda mrefu.

Tunatambua kuwa uwekezaji katika gesi kutoka makampuni ya nje umeongezeka hadi Mamlaka ya Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) imekiri kuwa makampuni ya mafuta na gesi ya kimataifa (IOC's) yanayofanya kazi hapa nchini, yamewekeza katika sekta hiyo kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.7 ambazo ni sawa na trilioni 7.52/-.

Fedha hizo zitaibua miradi lukuki ambayo wananchi wa kawaida nchini watapata ajira, na taarifa kutoka taasisi ya Uingereza ya ufuatiliaji wa Biashara Kimataifa (BMI), imetoa tathmini ya mwenendo wa biashara ya uwekezaji kuwa Tanzania imeshaipita hata Afrika Kusini kwa kuwavutia wawekezaji katika mafuta na gesi.

Ipo miradi mingi itakayotokana na matumizi ya gesi ambayo wananchi wataendelea kunufaika nayo, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Muhongo alisema wiki hii kuwa miradi yote nchini inatakiwa kukamilika ifikapo Juni 2015, na kwamba usambazaji wa umeme vijijini utaenda sambamba na ukamilishwaji wa miradi mingine.

Wananchi wanatakiwa kujipanga na kuwa tayari kushiriki katika kuinua uchumi wa nchi kupitia miradi mbalimbali itakayoanzishwa baada ya mradi wa gesi kukamilika.

Kushiriki kwao kutokane na maandalizi ya kuanzia sasa kwa kujitafutia elimu inayofanana na taaluma za teknolojia ya sayansi ya gesi.

Tunaamini kuwa kila mwananchi, na hasa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara sasa wameelewa vyema umuhimu ya bomba la gesi na namna litakavyowanufaisha wao wenyewe pamoja na kuinua uchumi wa taifa, tunawasihi waendelee kuweka mshikamano wa kuthamini na kutunza miundombinu ya mradi huo kwa faida ya kizazi hiki pamoja na kizazi kijacho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: