Serengeti. Maisha ya wanyamapori katika Hifadhi ya Serengeti na wanaoishi katika maeneo ya Mikoa ya Mara na Mwanza yapo hatarini kutokana na kugundulika kwa mmea hatari maarufu kwa jina la maguguvamizi na unaua majani na mimea mingine inayoota karibu yake.
Maguguvamizi hayo yanayojulikana kitaalamu Chromoleana Odorata, kwa kipindi cha miaka 10 yamesambaa katika maeneo mengi ya Wilaya ya Serengeti ikiwamo maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, mapori ya akiba ya Ikorongo na Gurumeti na Wilaya za Butiama na Tarime mkoani Mara.
Hata hivyo, taarifa za watafiti wanaoendelea na utafiti wao kuhusu mmea huo bado hazijatolewa.
Maguguvamizi hayo ambayo wakazi wa Wilaya ya Serengeti hasa Tarafa ya Ngoreme wameyabatiza jina la ‘amachabongo’ (ikiwa na maana lililokuja hivi karibuni) yanadaiwa kuingia nchini kutokea Sudan, Kenya kwa kupitia mwambao wa Mto Mara.
Maguguvamizi hayo ambayo yakikatwa huchipua haraka na yanapoota hakustawi kitu kingine kwa kuwa hufunika eneo lote na kusababisha kutoweka kwa nyasi na kuathiri malisho ya mifugo na wanyamapori.
Taarifa za Wataalamu
Mfungo Makunja Ofisa Kilimo Kata ya Kenyamonta Tarafa ya Ngoreme anasema mwaka 2004 maguguvamizi hayo yaliingia kidogokidogo na wakayaona ya kawaida.
“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi tulidhani ni gugu la kawaida. Mwaka 2008 yalianza kufunika maeneo mengi ukipita unaona kijani kana kwamba ni mazingira yamehifadhiwa, lakini ukiangalia chini hakuna kitu kinachoota, hakuna nyasi, miti inakufa hata katani, tulishtuka,” anasema.
Athari zajitokeza waziwazi
Makunja anasema athari zake zilianza kujitokeza waziwazi na kulazimika kutoa taarifa ngazi ya wilaya kwa hatua za haraka kwa kuwa kusambaa kwake kuliwashangaza, miti ilianza kupungua kwa kuwa haioti eneo maguguvamizi hayo yamestawi, mifugo ikaanza kukosa malisho, watu wakaanza kusaka miti ya kujengea na nyasi za kuezekea.
Mbegu zake zinasababisha upofu kwa mifugo
Anabainisha kuwa mbegu za maguguvamizi hayo umbo lake ni sawa na nyuzi laini aina ya sufi, zikiingia ndani ya macho ya mifugo hata binadamu husababisha upofu.
“Kuna kesi kama hizo zimejitokeza eneo hili, tukabaini mbegu hizo ni chanzo, kwa kuwa ni nyepesi sana,” anasema Makunja.
Mtaalamu huyo anasema mmea huo hutoa matawi mengi na kwamba shina lake lina matundu yanayohifadhi maji wakati wa masika ambayo hulisaidia kustawi wakati wa kiangazi.
Wanyama, magari na upepo husafirisha mbegu
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo mbegu za maguguvamizi hayo husafirishwa kwa njia mbalimbali ikiwamo wanyama wanapokuwa malishoni huingia kwenye manyoya na husambaza wanapokuwa wanatembea katika maeneo mengine.
Makunja anasema: “Wanyama wa kufugwa wakirudi nyumbani mbegu za maguguvamizi hupukutika na ikitokea mtu akachukua mbolea katika zizi hilo kupeleka shambani husaidia mbegu hizo kuota kwa kasi kwenye mashamba na kuathiri mazao,” anasema.
Anasema utafiti umebaini kuwa shughuli za binadamu ikiwamo mavazi na utengenezaji wa barabara kwa kutumia mitambo zimechangia kusambaa kwa maguguvamizi hayo kando kando ya barabara.
“Mbegu zake ni za ajabu wakati wa mvua magari huchangia kuzisafirisha zinanata kwenye magurudumu na viatu vya binadamu vinavyokuwa na udongo,” anasema na kuongeza:
“Kwa hali ilivyo kunatakiwa mikakati mbalimbali ili kuyadhibiti maana kasi ya kusambaa ni kubwa sana,” anasema.
Sehemu za miinuko na milima katika tarafa hiyo ambayo hutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo, maguguvamizi hayo yametapakaa. Hivyo kwa mtu mgeni akipita atawasifu wakazi wa eneo kwa kutunza mazingira, wakati chini hakuna mmea mwingine na hustawi zaidi milimani.
Watafiti hawajatoa majibu
Watafiti mbalimbali kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sua) Ukiriguru, Nile Basin Initiative, Tafiri, Sederec, Senapa na Gurumeti Reserves wanaendelea kufanya utafiti kuhusu mmea huo.
Wananchi wamekata tamaa
Sagati Mwikwabe mkazi wa Kitongoji cha Kemahiri, Kijiji cha Hekwe Kata ya Kenyamonta anasema wao wameshakata tamaa kwa kuwa maguguvamizi hayo yamemaliza malisho ya mifugo na hata mazao, kwa kuwa likiota shambani huathiri ukuaji wa mazao.
“Maguguvamizi hayo yana harufu mbaya, mifugo inapata shida, ardhi hukauka sehemu yalipo. Kama ni shambani unalazimika kupalilia mara kwa mara kwa kuwa hukua haraka na kufunika mazao, inapotokea hivyo huwezi kupata mavuno,” anasema.
Andrew Maro mkazi wa Kitongoji cha Kemuresi, Kijiji cha Hekwe anasema pamoja na jitihada za kufyeka na kuchoma maguguvamizi hayo yamekuwa yakizidi kustawi, kila baada ya muda mfupi.
Naye Nyahende Wangwe (46) mkazi wa Kijiji cha Mesaga, Kata ya Kenyamonta akizungumza na gazeti hili akiwa shambani kwake anasema hali ya mavuno imeshuka, chanzo ni maguguvamizi hayo.
kwa kuwa kabla ya kuingia eneo hilo walikuwa wakivuna mazao mengi na eneo hilo halikuwa na tatizo la njaa.
Itaendelea Jumamosi...
Mwananchi
No comments:
Post a Comment