ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 5, 2014

SOTE TUWAJIBIKE LINAPOKUJA SUALA LA UTAWALA BORA-TANZANIA

Ujumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Ahmed MAKAME HAJI- Tume ya Mipango na Bihindi Nassor Khatib Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha wakifuatilia majadiliano kuhusu maendeleo endelevu.
Muwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akichangia wakati wa Mkutano wa siku nne wa Kilele wa Kisiasa uliokuwa ukijadili mada mbalimbali zinazohusiana na masuala ya maendeleo endelevu. Mkutano huo uliandaliwa na Baraza Kuu la Uchumi na Maendeleo la Umoja wa Mataifa 9 ECOSOC). katika ujumbe wake Balozi aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, aliikumbusha jumuiya ya kimataifa kuwa suala la utawala bora ni jumuishi ambapo jumuiya ya kimataifa pia inahusika nalo. Nyuma ya Balozi ni Bi Amina Shaaban Mkurugenzi Mtendaji, Tume ya Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Kilele wa Kisiasa wa siku nne uliofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ukiwashirikisha wajumbe kutoka mataifa mbalimbali, wanazuoni,wataalamu wa kada mbalimbali, makundi maalum na Asasi zisizo za kiserikali.


Na  Mwandishi  Maalum
Wakati   mchakato wa  maandalizi ya   ajenda   na malengo  mapya ya maendeleo endelevu  baada ya 2015 ukiendelea  kushika kasi  kwa mijadala mbalimbali inayoendelea  hapa  Umoja wa Mataifa. Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania, kwa upande wake imesisitiza  kuwa   pamoja na kukubaliana kwamba  suala la utawala bora ni  muhimu katika  utekelezaji wa  maendeleo na kupiga vita umaskini, hata hivyo eneo hilo halipashwi kuwa la upande mmoja.
 “Hoja ya  utawala bora  ni muhimu sana,   ni muhimu sana katika uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na hata upatikanaji wa nishati endelevu kwa watu wetu.Lakini  utawala bora hauwezi  kuelekezwa  au   kuwa ni    hoja ya  nchi  moja moja  au kanda, bali ni hoja inayokwenda  mbali  zaidi,  utawala  bora  unatuhusu sote  hadi katika  ngazi ya kimataifa sote tunapashwa kuwajibika katika eneo hili” akasema Balozi Tuvako Manongi

Moja ya eneo  ambalo  alilitolea mfano kama linalohitaji uwajibikaji wa pamoja  inapokuja hoja ya utawala bora ni  eneo la  fedha haramu au kwa maneno mengine utoroshwaji wa fedha kutoka nchi zinazoendelea  na kwenda kufichwa  nje. Akisema  ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo kwa namna moja ama nyingine lina changia  katika  ukwamishaji wa   maendeleo  linahitaji ushirikiano  wa pamoja.  
Muwakilishi huyo wa Tanzania katika  Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo mwisho wa mkutano wa siku nne wa Kilele wa Kisiasa  ulioadaliwa na  Baraza Kuu la Uchumi na Maendeleo la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC) na  kuwashirikisha  nchi wanachama,  wanazuoni , wawakilishi wa makundi maalum pamoja na    Asasi zisizokuwa za kiserikali.
Mkutano huo wa siku nne,   ulijadili  mada mbalimbali lakini zote zikijikita katika  mihimili  mikuu mitatu  inayosimamia maendeleo endelevu kama yalivyoainishwa katika  Mkutano wa Kimataifa wa  RIO+20 uliofanyika nchini  Brazili. Maeneo hayo na ambayo yanatakiwa kutekelezwa sambamba ni    maendeleo ya  Kijamii,  maendeleo ya Kiuchumi na  Mazingira.
 Pamoja na kuzungumzia  hoja ya utawala bora,  Balozi Tuvako Manongi pia  amesema  majadiliano ya DOHA kuhusu  fursa za  biashara kwa nchi zinazoendelea  yapashwa kukamilishwa. Kwa kile alichosema  majadiliano ya DOHA ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa  Maendeleo endelevu baada ya 2015
“ Biashara ni muhimu sana  katika  maendeleo,  na kwa sababu ya umuhimu wake,  ujumbe wangu ungependa kusisitiza kwamba majadiliano ya DOHA yanapashwa  kukamilishwa  kama ilivyoahidiwa huko Bali, Indonesia.
Kuhusu nafasi ya   sekta binafsi  katika kuchagiza maendeleo,  Balozi Manongi alisema,  sekta binafsi  inatakiwa kuwezeshwa kwa kuundiwa sera na mazingira ambayo  itaiwezesha kukua , kuimarika na hivyo  kuwa katika nafasi nzuri ya kuchangia utekelezaji wa maendeleo na  kupanua wigo wa ajira.
Kuhusu mchakato mzima wa maandalizi ya agenda mpya za maendeleo na  malengo yake,  Muwakilishi huyo wa Tanzania,  alitahadharisha kuwa,  agenda hizo na malengo yake,   ni lazima yazingatie  hali halisi ya kila nchi, uwezo wake na utayari wa kuyatekeleza, kipi  kinahitaji na kipi haikihitaji. Kwa kile alichosema   nchi  hazifanani ,ni tofauti na  hata katika  kiwango  cha umaskini  zinatofuatiana. 

No comments: