ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 2, 2014

Abiria aleweshwa madawa na kuibiwa milioni 1.8/-

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo, Justus Kamugisha

Abiria aliyekuwa akitokea Singida kwenda Mwanza, Shija Nkande, amedaiwa kuleweshwa madawa ya kulevya ndani ya basi alilokuwa akisafiria na kuibiwa Sh. milioni 1.8 na mtu asiyefahamika.

Akitoa taarifa za mtu huyo kwa vyombo vya habari, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Fedreki Mlekwa, alisema Julai 30, Nkande alipelekwa hospitalini hapo akiwa hajitambui.

Alisema baada ya matibabu alimhoji mtu huyo kusema alikuwa akisafiri kutoka Singida kwenda Mwanza akiwa amekaa jirani na kijana aliyempa karanga za kukaanga, ambapo baada ya kula muda mfupi alipoteza fahamu.

Alisema wakati akimpokea mtu huyo mifuko ya suruali yake ilikuwa imechanwa kwa wembe.

Dk. Mlekwa alisema Nkande alisema alikuwa na Sh. milioni 1.8 kwenye mifuko yake.

Hata hivyo, alisema Nkande baada ya kupata nafuu alitoroka hospitalini kabla ya kupewa ruhusa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo, Justus Kamugisha, alisema hana taarifa juu ya tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: