Wednesday, August 13, 2014

ACHA KUMUUMIZA MOYO WAKE, THAMINI HISIA ZAKE!-2

KARIBU kwenye All About Love, bila shaka kuna vitu vipya vingi unavyovuna katika ukurasa huu. Kama ni mara ya kwanza kusoma hapa, tabasamu maana umeingia kwenye ulimwengu wa elimu kubwa ya uhusiano na mapenzi.

Unaweza kunisoma pia kwenye Let’s Talk About Love kwenye gazeti la Ijumaa, Elimu ya Mapenzi katika gazeti la Championi Jumamosi na Love & Life ndani ya gazeti la Uwazi kila Jumanne. Ungana nami uzidi kukuza ufahamu wako kuhusu uhusiano na mapenzi.

Naam! Sasa tuendelee na mada yetu. Nazungumza juu ya mwanamke atakavyoweza kumkabili mwanaume ambaye si chaguo lake. Hakuna haja ya kuachiana maumivu.
Mengi tumezungumzia wiki iliyopita, lakini kubwa zaidi nilisema kwamba, jambo la kwanza ikiwa unajua huna mtu kwa maana ya mume au mchumba, mbinu hizi zinakuhusu sana.

Pili, nilifafanua kwamba, mwanamke anapaswa kukubali kukutana na mwanaume husika, lakini katika eneo ambalo si la hatari kumuingiza kwenye vishawishi, kisha mpe nafasi mwanaume huyo ajieleze.
Wakati namalizia wiki iliyopita, nilitania kwamba, kumsikiliza kwa makini ni jambo zuri, maana inawezekana ukabadilisha mawazo na kuamua kuwa naye. Ni kweli, ni jambo linalowezekana.
Kikubwa ni kuwa makini na hisia zako. Huenda sera zake zikakufurahisha na ukaona kumbe ni aina ya mwanaume uliyekuwa ukimhitaji. Sasa tuendelee.

THAMINI MAWAZO YAKE
Ni wazi baada ya kumpa nafasi azungumze, alikutamkia kuwa anakutaka! Ukweli uliopo katika moyo wako ni kuwa humuhitaji kwa namna yoyote. Mshukuru kwa kukupenda, onyesha kumthamini, onyesha imani juu yake.

Onyesha masikitiko kutokana na jibu utakalompa kwa sababu ni wazi kuwa hatalipenda. Hii itamfanya mwanaume huyo ajione wa thamani ila kwa bahati mbaya alichelewa. Thamini alichozungumza na jitahidi kuonyesha umakini lakini mwambie amechelewa, una wako (hata kama huna).

SHEA UKWELI
Mpaka amefikia hatua ya kutoa dukuduku lake moyoni na kukutamkia bayana kuwa anakuhitaji ni wazi kuwa mwanaume huyu anakupenda. Sasa kama ndivyo na imetokea bahati mbaya hana sifa unazozihitaji, usimjibu vibaya tumia akili yako ya kuzaliwa kufikisha hisia zilizopo katikati ya moyo wako lakini asijisikie vibaya.

Unaweza kumwambia: “Ahsante sana kwa kunipenda, hata mimi nakupenda pia, lakini kwa bahati mbaya umewahiwa, nina mchumba ambaye nampenda na yeye ananipenda na siyo vizuri kumsaliti.”
Huu ndiyo msumari wa mwisho. Kama alikuwa ni mwanaume mwenye mapenzi ya kweli kwako na siyo wa kukuchezea, bila shaka atathamini maneno yako kutokana na ukweli halisi uliompa hasa ukizingatia kuwa kama yeye ndiye angekuwa anasalitiwa asingejisikia vyema.

MTAKE RADHI
Lazima utakuwa umempotezea muda wake kukutana na wewe na kuzungumza pamoja. Isitoshe inawezekana mazungumzo yenu mlikuwa mkizungumzia katika hoteli, mgahawa au mahali pengine ambapo alitumia gharama hivyo kuhisi kuwa umempotezea fedha kwenye jambo ambalo halikuzaa matunda.

Kubwa zaidi utakuwa umemwacha na majeraha katika moyo wake hasa kama na yeye alikuwa akikupenda kwa dhati. Baada ya kumweleza hali halisi, mtake radhi kwa kumpotezea muda wake, pia mwambie asikuchukie na mbaki mnaheshimiana.

Hapo utakuwa umemwacha mwanaume huyo katika hali nzuri ya kutojisikia vibaya au kushushwa thamani yake tofauti na kutumia maneno makali au matusi katika kumkatalia.
Bila shaka utakuwa umeongeza kitu kipya katika ubongo wako…

wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mada nyingine kali, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake