ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 12, 2014

Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Watanzania.


Mhe. Rais Jakaya Kikwete
Ndugu Mheshimiwa Raisi, ni kwa moyo mzito na uliojawa na matumaini nachukua nafasi hii kukujumuisha katika uhalisia wa nchi yetu inapokwenda, ilipo kwa sasa na ilivyokuwa hapo awali kutonana na mtazamo wangu binafsi. Najua ni wazi kuwa kila mwenye mapenzi na nchi hii, ukiwemo wewe Mheshimiwa Raisi, unatambua wazi kuwa nchi yetu ilipo na inapoelekea si kama tulivyotarajia . Katika barua hii, nitazungumzia kwa ufupi nchi yetu ilivyokuwa hapo awali, ilipo sasa na inapoelekea pamoja na kutoa mapendekezo jinsi ya kutatua baadhi ya matatizo yanayotukabili.
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, kama Conficius,mwanafalsafa mashuhuri alivyosema, "Jifunze yakale kama unataka kuchambua yajayo" nami nitaanza barua yangu hii kwa kuchambua kwa kifupi jinsi nchi yetu ilivyokuwa hapo awali. Kwa wale wote ambao walijifunza historia kidogo ya nchi yetu,
tunajua kabla ya mkoloni nchi yetu ilikuwa ikitawaliwa na tawala za kichifu ambazo zilisisitiza wanajamii wake kuishi kwa kupendana na ushirikiano. Falsafa ya jamii hizo zenye tawala za kichifu zilisisitiza umuhimu wa jamii kabla ya umuhimu wa mtu binafsi. Falsafa hii ilijikita katika mila zetu na kwa asilimia kubwa ilitoa muongozo kwa tamaduni mbalimbali ambao zilichanua katika jamii hizo. Katika jamii hizo, udini baina ya jamii na jamii ulitawala na kwa yoyote asiyesoma kitabu cha Kinjekitile anaweza kutambua hili. Hata hivyo, kutokana na udogo wa jamii hizi pamoja na karibia kila jamii kuwa na Miungu yake, udini haukuwa tatizo kubwa zama hizo. Baada ya uhuru, jamii nyingi zilijikuta zikilazimika kubadili mifumo yao ya kitawala na kwa mara ya kwanza kutii utawala mmoja ambao uliongozwa na Mwalimu Nyerere. Pamoja na uchanga wa umoja ambao makabilia na watu wenye itikadi mbalimbali walilazimika kuutumika baada ya uhuru, Watanzania walionyesha mshikamano mkubwa na uvumilivu ambao uliifanya nchi yetu isifike nje na ndani kutonaka mshikamano huo baina ya makabila zaidi ya 120 yenye mila na imani tofauti. Kwa ujumla kwa yoyote atayeangalia jamii hizi  za hapo awali, atatambua kuwa jamii hizi ziliungana kutona na kuwa na adui mmoja ambaye alikuwa mkoloni na mshikamano na heshima baina ya jamii hizi uliendelea baada ya uhuru kutokana na uhalisia kuwa jamii zao zilipitia unyasasaji na unyonyaji uliofanana kutoka kwa mkoloni. Neno uzalendo nyakati hizo lilikuwa na maana kubwa na uongozi uliokuwa ukiongozwa na Mwalimu Nyerere haukusita kuwawajibisha wale wote ambao walikuwa hawana uzalendo katika kuliongoza taifa letu. Kama wote tunavyojua, sera za Mwalimu Nyerere zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuleta umoja baina ya Watanzania hata hivyo zilishindwa kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizoikumba jamii yetu. Hata hivyo, pamoja na sera za kimaendeleo za Mwalimu Nyerere ambaye alifuata sera za Kijamaa zenye sura ya Kiafrika kushindwa katika sekta ya uchumi, Mwalimu alitambua umuhimu wa elimu kwa katika maendeleo yetu na alifanya kila awezalo kuhakikisha unongozi wake unatilia mkazo elimu. Kofi Annan, moja ya nyota za Afrika zilizongara katika jukwaa la kimataifa aliwahi kusema," elimu ni haki ya binadamu na ina nguvu kubwa ya kumbadilisha. Katika misingi yake, mihimili ya uhuru, demokrasia  na maendeleo endelevu hupatikana." Mwalimu Nyerere kwa kulitambua hili, hakusita kutilia mkazo wa kipekee katika elimu hata pale alipotambua wazi kuwa sera zake za Kijamaa hazikuwa zikizaa matunda yalitarajiwa.
            Baada ya Mwalimu kuachia madaraka na Mzee Mwinyi kuchuka nchi, Tanzani ilijikuta katika ya dunia ambayo ilikuwa ikipitia mabadiliko makubwa kama mwisho wa Ukomunisti katika Jamuhuri ya Kisovieti na Demokrasi kuchua uongozi kama mfumo katika serikali nyingi duniani. Mnamo mwaka 1992, kama wote tunavyofahamu, Tanzania haikuwa na budi ila kuingiza mfumo wa vyama vingi nchini kama njia mmojawapo ya kukuza demokrasia. Hata hivyo, mfumo wa demokrasia haukukosa kasoro katika jamii ambayo ilikuwa imeunganishwa na sera za ujamaa. Demokrasia pamoja na ukosefu wa elimu ulikuwa ukiwakumba Watanzania wengi kwa nyakati hizo, ulisababisha mabadiliko makubwa ya jamii yetu ambayo kwa mara ya kwanza iliruhusu watu wenye itikadi tofauti za kisiasa na kidini kujadili tofauti zao hadharani. Bila kutazamia, jamii yetu ilianza kuwa na matabaka ambayo yaliletwa na utofauti wa kipato, maarifa pamoja na itikadi za kisiasa lakini tafaouti hizi zilikuwa za kutarajia kwa jamii yoyote ile ambayo ilikuwa katika mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
            Baada ya miaka karibia 21 ya mfumo wa nyama vyingi na miaka 51 na moja ya kujitawala, jamii yetu imepitia  mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, siasa na kijamii. Sera kama za Ujamaa zimebaki kuwa sera zinavyofundishwa mashuleni bila kuwa na nguvu katika uhalisia. Vile vile, demokrasia ambayo ilikuja na chembe za ubepari(soko huru), imefanya jamii yetu ya sasa kuwa na tofaouti kubwa kati ya matajiri na maskini. Mbali na hayo, mabadiliko ya kidunia ambapo vita dhidi ya ugaidi vimepewa vipaumbele katika sera za mataifa yenye nguvu kubwa za kiuchumi, zimefanya nchi yetu ijikute katika changamoto zisizozuhilika kutokana na muundo na upeo wa jamii yetu.
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, sote tunatambua kuwa katika kila badiliko ambalo jamii yoyote ile itapitia, lazima kuwe na changamoto mbalimbali ambazo zitajitokeza. Kwa wale ambao walibahatika kusoma historia ya dunia kwa ujumla, watatambua kuwa mabadiliko ya kiuchumu, kisiasa na kijamii  ambayo yalitokea katika nchi mbalimbali hapo karne za awali,yalitawaliwa na machafuko makubwa. Bila kupoteza dira ya mjadala huu, nchi yetu kwa sasa inakumbana na changamoto za kiuchumi, kidini, kisiasa na kijamii kutokana na mabadiko mbalimbali ambayo nchi yetu imepitia na inayoendelea kupitia.
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, changamoto za kiuchumi nchini kwetu zinaletwa na kuyumba kwa uchumi wa dunia na baadhi ya sera zisizo na tija ambazo serikali yetu zinatekeleza. Ndugu Mheshimiwa Raisi, nadhani bila shaka unatambua jinsi serikali yako inavyoshutumiwa kwa kutokuwa makini katika sekta ya uchumi. Kila kukicha wabunge wetu wanatuonyesha Watanzania jinsi serikali yetu isivyo makini katika kusimamia miradi ya kiuchumu pamoja na upotevu wa mamilioni ya shilingi unaoletwa na uzembe huo. Mikataba mibovu, viongozi wasio na upeo pamoja na uzembe wa usimamizi wa miradi ni baadha tu matatizo ambayo yanakuza tatizo la uchumu dhoofu katika nchi yetu. Mheshimwa Raisi, nadhani wimbo huu si mgeni katika masikio yako na bila shaka unafanya kila uwezalo kama unavyotakikana na katiba na sera ya chama chako kutafutia ufumbuzi tatizo hili la uchumi. Hata hivyo, Mheshimiwa Raisi kwa kiasi kikubwa sera za chama chako zinaruhusu tatizo la uchumu kuendelea kukua na mara nyingi viongozi wetu wamekuwa wakiendesha nchi kwa kutumia uzoefu bila tija na utalaamu unaohitajika hivyo kufanya tatizo la uchumu kukua kila kukicha.Mheshimiwa Raisi, katika nakala hii nataka kukujulisha vile vile jinsi jamii yetu unavyochangia katika tatizo la uchumi.
            Ndugu  Mheshimiwa Raisi, baada ya sera ya Ujamaa kushindwa kuzaa matunda katika sekta ya uchumi, na nchi yetu kukumbatia demokrasia na ubepari(soko huru), asimilia kubwa ya jamii yetu haikuwa tayari kielimu kakabiliana na mabadiliko haya. Mheshimiwa Raisi, kama wote tunavyotambua, ili demokrasia iweze kufanikiwa, lazima kila mwananchi afahamu majukumu yake katika maendeleo ya kiuchumi na awe na utashi wa kuyatekeleza majukumu hayo. Sio siri kutokana na mfumo wa vyama vingi na ushindani unaoletwa na mfumo huu, baadhi ya vyama zimeelekeza juhudi zao kuwashawishi Watanzania kuwa jukumu la kuleta maendeleo kwa asilimia kubwa ni la serikali kwa kutoa ahadi zisizo za kweli. Utegemezi huu kwa serikali umezalisha jamii ambayo kwa kiasi kikubwa haiwajibiki katika kujiletea maendeleo. Mheshimiwa Raisi, natambua wazi kuwa Serikali yoyote ile iko madarakani kutoa muongozo stahiki kwa wanachi wake ili kuwaletea maendeleo katika sekta mbalimbali. Hata hivyo, kwa mataifa ambayo yameendelea, wananchi wake huwajibika kwa asilimia kubwa katika kujiletea maendeleo na kazi za serikali zao hubakia kuwa ni kutengeneza mazingira yanayostahili ili wananchi wake waweze kutekeleza mipango yao. Katika nchi yetu kumekuwa na matatizo mawili makuu katika suala hili. Kwanza kabisa asilimia kubwa ya wananchi wamelazimishwa kuamini kuwa jukumu la kuleta maendeleo kwa asilimia kubwa, ni la serikali, na vile vile serikali yetu imekuwa haitengenezi mazingira stahiki kwa wananchi wake kutekeleza mipango yao hivyo kuwavunja moyo wale wachache wenye kutekeleza majukumu yao. Uzembe huu wa serikali unatokana na siasa zenye chembechembe za ushabiki wa sera za kijamaa. Kwa mfano, nchini mwetu ni jambo la kawaida kusikia wizara fulani au sekta fulani inatawaliwa na watu wa kabila au itikadi fulani.Tatizo hili la upendeleo ambalo husababisha utendaji hafifu kutonana na watendaji wa sekta hizo kutowajibishana ipasavyo, misingi yake iko katika elimu haba ambayo Watanzania wengi wanaendelea kuipata, na waliyopata, wakati wanabadili mifumo ya kisiasa na kijamii miaka ya tisini. Jamii yetu haikuelimishwa vizuri njia mbadala za kuachana na sera za kijamaa, na mwishowe tumejikuta tukiandamwa na ujamaa katika zama ambazo tumeipa demokrasia nafasi kubwa katika mfumo wetu wa kuendesha nchi. .
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, changamoto nyingine ambayo inaikabili jamii yetu kwa sasa ni ile ya udini. Changamoto hii kwa asilimia kubwa imezaliwa na muelekeo wa sera za mataifa yenye nguvu kiuchumu duniani na nchi yetu imekumbwa katikati ya tatizo hili. Kama sote tunavyojua, suala la ugaidi ni suala tete ambao watu wengi hulitafsiri isivyo na kusababisha uhasama baina ya watu wa madhehebu mbalimbali. Ugaidi kuambatanishwa kimakosa na dini yenye wafuasi wengi duniani, kumesababisha kutokea kwa uhasama baina ya Waislamu na watu wa madhehebu mengine. Waislamu wanaamini wameonewa kwa dini yao kufananishwa na Ugaidi na hivyo basi kuchukua jukumu la kuilinda dini yao. Mheshimiwa Raisi, sitazungumzia kwa undani jinsi dhana hii potofu kuwa Ugaidi unaletwa na Waislamu wenye kufuata miiko ya dini yao, bali nitaongelea kwa ufupi jinsi uhalisia wa hali hii unavyojitokeza katika jamii yetu na kutoa mapendekezo jinsi ya kupambana nao.
            Mheshimwa Raisi, siamini  kuwa mtu au jamii yoyote ile ina haki ya kunyooshea vidole dini nyingine kwa sababu tu kuna baadhi ya wafuasi wa dini hiyo wanahusishwa na matukio ya fulani. Hata hivyo,kwa upande mmoja ni jukumu la viongozi wa kidini kutoa tafsiri stahiki za maandiko ya kidini ili kuepusha kutoposhwa kwa ukweli wa maandiko hayo. Pamoja na misingi ya tatizo hili la udini kutokea nje ya nchi yetu,baadhi ya wanasiasa wetu wamekuwa wakitumia suala hili la udini kupenyeza sera zao kwa wananchi.Viongozi hawa ni wazi wanatakiwa wawajibishwe ipasavyo kwani kiongozi yoyote yule katika jamii ana ushawishi mkubwa kwa watu, hivyo basi lazima katiba itimike ipasavyo kuelezea mipaka ya ushawishi huu walionao viongozi wetu. Serikali haina budi kushughulikia kwa urahaka na bila upendeleo tofauti zote za kidini ambao zinazojitokeza ndani ya nchi yetu pamoja na kutoa elimu itakayowaelimisha wananchi namna mbadala ya kuishi kwenye jamii iliyo chini ya serikali isiyo na dini.
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, hivi karibuni tumeshudia kwa huzuni kubwa asimilia sitini ya watahiniwa wa kidato cha nne wakifeli katika mitiyani yao hivi juzi juzi. Mheshimiwa Raisi, yote niliyozungumzia hapo awali hatayakuwa na umuhimu wowote kama watu ambao taifa letu linawategemea kuleta maendeleo ya kifikira, kisiasa, kijamii pamoja na kiuchumi hawana ufamu wa kina wa mambo. Hali hii ya sasa nchini inakatisha matumaini ya maendelea yoyote yale kwani ili kutela maendeleo, lazima wananchi wale na maarifa toshelezi yanayoendana na nyakati ambayo yatawawezesha kupanga na kutekeleza mipango sanifu ya kimaendeleo. Vile vile, lazima wananchi wawe na uelewa wa kutambua nafasi yao na ya serikali katika kujiletea maendeleo. Mheshimiwa Raisi, pamoja na kutambua kuwa serikali yetu ina changamoto nyingine ambazo zinahitaji kushughulikwa kwa haraka kama ukosefu wa maji, umeme na miundombinu, sekta ya elimu ni uhai wa taifa lolote lile na sote tunafahamu hili. Mheshimiwa Raisi, nchi yetu iko katika dunia ambayo inapiga hatua kubwa katika sekta ya elimu ambayo manufaa yake yanaonekana kwenye kila ngazi katika jamii mbalimbali duniani hivyo basi hatuna budi kuacha mzaha na sekta hii.
            Ndugu Mheshimiwa Raisi, mwisho wa barua hii  napenda kuwapongeza na kuwakosoa wanasiasa wetu ambao wamekuwa wakijituma kuwaletea Watanzania maendeleo na vile vile kwa nyakati nyingine wamekuwa wakileta matatizo katika harakati zao za kisiasa. Mheshimiwa Raisi, sio siri kuwa kwa sasa nchi yetu imekumbatia Demokrasia kwa mapana yake na kwa asilimia kubwa wanasiasa wetu wameanzisha utamaduni wa kuwajibishana wao kwa wao kwa nia ya kumletea maendeleo Mtanzania wa kawaida. Wanasiasa wanaonyesha ukomavu na uvumilivu mkubwa unaotakikana katika demokrasia bila kuleta machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiwakumbwa majirani zetu. Hata hivyo, katika zama hizi ambazo demokrasiia inashamiri, wanasiasa wengi wamekuwa wakitumia vibaya Watanzania kueneza siasa za chuki na kidini wakisisitiza wanapiginia demokrasia.Mheshimiwa Raisi, natambua kwa mapana ya haki kujielezea kama inavyoelezwa na misingi demokrasia, lakini pamoja na mapungufu ya serikali yetu, baadhi wanasiasa wamekuwa wakiweka ushabiki wa kisiasa mbele katika kukosoa au kupongeza serikali yetu. Vile vile, serikali yako imekuwa haitoi ushirikiano stahiki kwa wanasiasa wa baadhi wa vyama vya upinzani hivyo basi kuwafanya watumie njia ambazo mara nyingine husababisha machafuko katika jamii wakati wa kuwakilisha kero za wananchi wao. Mheshimiwa Raisi, ili kuendelea kuienzi amani yetu, serikali yetu inapaswa kushirikiana na wadau wote katika siasa bila upendeleo unaotokana na itikadi za kisiasa au kidini ile kumletea Mtanzania wa kawaida maendeleo ya kweli. Wanasiasa nao lazima watumie njia mbadala kuwakilisha kero za wananchi na kufichua uzembe wowote ule kwa upande wa serikali na wananchi bila uchochezi huku wakiendelea kuwajibishana wao kwa wao.
            Mheshimiwa Raisi, najua kwa asilimia kubwa yote niliyoyazungumza kwenye barua hii si masuala mageni masikioni mwako, na ninatumaini utaendelea kuchukua hatua stahiki kwa ushikiano na wananchi, viongozi wa kisiasa, kidini na taasisi mbalimbali katika kulikumbusha taifa misingi yake ambayo inahatarishwa na mabaliko ya kidunia,kijamii, kidini na kisiasa nchini kwetu .
            Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Africa.
Dennis John,

Mtanzania Mkereketwa. 

4 comments:

Anonymous said...

Well written. I

Anonymous said...

Dennis man what a joke! Umeandika garbage nyingi. Wewe ni ukawa au Chadema puppet?We are doing well as a country! Of course we have more work ahead of us, lakini Tanzania inasonga mbele. Maybe not at the speed of your liking mr. Fake Dennis! Assuming that we elect you as the next President, please post on this blog your five years development plan. Unfortunately, the use of cheap pseudo-names such as Dennis and the likes, would only advance the interest of the opposition at the expense of Tanzanians. Mimi ni mtanzania ambaye nimechoshwa na watu wanao mdharau Rais ambaye alichaguliwa na mamilioni ya watanzania. People like Dennis should just shut up, and I mean it!

Anonymous said...

Ndugu "Anonymous", ni wazi ufahamu wako kwenye masuala fulani muhimu ni haba. Sidhani kama umesoma vyema barua hii kwa jinsi ulivyocomment. Muhandishi wa barua hii amepitia kwa umakini vipengele ulivyozungumzia na vile vile ameonyesha mawazo komavu kwa kutambua kuwa na pamoja kuwa tuko nyuma kimaendeleo tumepiga hatua kubwa kimaendeleo toka tulipopata uhuru. Vile vile, hamna kipengeleo chochote katika barua hii ambacho kinamkashifu Raisi Kikwete kama unavyodhani na pia muhandishi wa barua hii amekemea kwa asilimia kubwa jinsi wapinzani wanavyotumia jukwaa la vyama vingi kukwamisha maendeleo. Kama msomaji wa barua hii nimesikitishwa na jibu lako ambalo linanifanya nitilie shaka umri na uwezo wako wa kufikiri, yaanii kwa upeo wako wewe umeona ushabiki wa chama au kejeli kwa Raisi Kikwete katika barua hii na kwa wakati huo huo unajiita Mtanzania aliyechoshwa na ushabiki wa chama?

Anonymous said...

Hello! My name is Dennis and I claim the responsibility for the content of this letter. Dear "anonymous",following your comment I was lost of appropriate words to address your stance! However, it was obviously you didn't read the letter as your comments projected.I clearly highlighted how we have great strides in development and how relative comparison of our development to other developed country can be totally unfair give majority of the developed countries took a couple of centuries to advance! "Ukawa"?, Chadema? I had to go back to my letter and try to find where I seemed to advance the agendas of the mentioned groups without success, kindly point out the specifics and I'll gladly respond. If you had read the letter, you might concluded that to a greater extent I was critical of the opposition while at the same time acknowledging their efforts in challenging for a better Tanzania. Secondly, I personally hold Hon. Kikwete in high esteem(I'll vote for him if it were possible for him to run again by the way!) that's why I invited him to share my thoughts of how we can build a better foundation for any sustainable development.My letter didn't suggest I was critical of any development plan laid forward by Hon. Kikwete, but I urged him to spearhead the culture of accountability, enforce quality education, eradicate religious barrier and fairness in order to pave a smooth path for your apparent "five plans".I am not sure if further explanation is worth my time since your mediocre response to my article does not suggest you are willing to reason critically although I'll like to believe otherwise.