Mwanamuziki Kida Waziri anasimulia kilichotokea katika maisha yake baada ya kifo cha mzazi mwenzake, Hemed Maneti Ulaya mwaka 1990.
Maneti alikuwa kiongozi wa Bendi ya Vijana Jazz na alifanikiwa kupata mtoto na Kida ambaye amepewa jina la Cecelia.
Kida ambaye naye alitamba na bendi hiyo alikuwa akinyanyapaliwa na kuambiwa kuwa mzazi mwenzake alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Hatimaye mwanamuziki huyo mwaka 1991 akajikuta akiangukia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine mwenye asili ya Kiarabu aitwaye Majid.
Katika uhusiano huo, Kida akajikuta akiwa mjamzito na mhusika akiwa Majid ambaye alikuwa akiyapuuza maneno ya watu waliokuwa wakinyanyapaa Kida.
Hebu endelea na pale tulipoishia wiki iliyopita…
Kida anasema Majid alipofika tu, mwenye grocery baadhi ya watu wakamweka chini na kuanza kumwambia kila kitu kilichotokea muda mchache uliopita.
“Hata hivyo, tofauti na matarajio yao, Majid aliwambia kitu ambacho kiliwafanya wabaki midomo wazi, aliwaambia inzi kufia kwenye kidonda siyo ajabu ni halali yake,” anasema Kida.
Hata hivyo, Kida anasema kuwa maneno hayo yalikuwa yamemwingia Majid ingawaje hakupenda kuonyesha mbele yangu.
“Majid hakupenda kuniambia kwamba kuna maneno ameyasikia ila baada ya kipindi kirefu ndipo aliponiambia hayo yote aliyokuwa akiambiwa na watu,” anasimulia Kida.
“Siku aliyoniambia maneno hayo nilijua kwamba Majid alikuwa na uvumilivu wa hali ya juu, kwani alisema lengo lake lilikuwa ni kunipa faraja.
“Aliniambia alikuwa na jukumu la kunifariji kwa wakati ule lilikuwa ni la kwake, hivyo hakutaka kunivunja nguvu kwa kuwa kila binadamu anahitaji faraja na hakujua Mungu amempangia nini?” Kida anasema kile alichoambiwa na Majid.
Mimba yataka mapupu, majivu ya sigara
Kwa mujibu wa Kida, mimba yake ilikuwa ni ya ajabu sana tofauti na nyingine mbili alizotangulia kuzibeba na kujifungua watoto wawili, Waziri na Cecilia.
“Kwanza nilikuwa napenda sana kula mapupu, hivyo ilitulazimu kwenda Tandika Mabatini ambako nilipafahamu kutokana na Majid kwenda kutengeneza magari yake.
“Mapupu niliyokuwa nayapenda ni yale yaliyotengenezwa katika baa, lakini siyo yaliyotengenezwa nyumbani, nilikuwa natoka Kinondoni kuyafuata Tandika.
“Pili nilikuwa napenda sana kusikia harufu ya majivu ya sigara na majivu ya mkaa. Nilikuwa nayachukua na kukaa nayo ili niweze kuyanusa, nilikuwa napenda harufu yake,” anasema Kida.
Alitapika kwa miezi tisa mfululizo
Kitu kingine kilichomtesa Kida ni kutapika mfululizo, anasema kwamba alianza kutapika kuanzia mimba ikiwa changa hadi alipoenda kujifungua.
“Ilikuwa ni ajabu, kwani niliacha kutapika wiki mbili baada ya kujifungua, hakika mimba hii ilinitesa sana,” anaongeza. Kupandisha mashetani, Kida anasema kitu kingine cha ajabu ambacho kilimtokea ni kupandisha mashetani.
“Ilianza kidogokidogo na baadaye ikawa inanisumbua sana na kuanza pilikapilika za kutibiwa kwa muda mrefu sana,” anasema.
Safari za kwenda kwa masheikh, wachungaji
Mwanamuziki huyo anasema kuwa hali ilikuwa mbaya sana, wakaanza kwenda hospitali, lakini vipimo vyote vilionyesha kwamba hakuwa na ugonjwa wowote.
Ikambidi kuanza kuombewa kwa masheikh na wachungaji mbalimbali, lakini hali yake ilikuwa inatulia kwa muda kisha kujirudia tena.
Kida anasema alipokuwa akipandisha mashetani yalikuwa yakitoa masharti ya kumtaka awe na mume wa kufunga naye siyo kujihusisha na uhusiano nje ya ndoa.
Pia, mashetani hayo yalikuwa yakilalamikia kitendo chake cha kubeba ujauzito nje ya ndoa na hayakutaka aendelee kufanya shughuli za muziki.
Mashetani yalimuanza zamani
Hata hivyo, Kida anasema kuwa tatizo la kukumbwa na masheteni lilimuanza muda mrefu tangu akiwa katika bendi ya Vijana Jazz, lakini hakuwa hakijua.
“Kuna wakati nilikuwa nikipanda jukwaani nasahau kuimba nyimbo zote mfano kama ule wa Penzi Haligawanyiki, nikishuka jukwaani nilikuwa nakumbuka, mpaka kuna wakati Maneti alidhani nilikuwa nafanya makusudi,” anasema.
Kida anaendelea kusimulia kuwa uso wake uliwahi kwenda upande alipopanda jukwani alipokuwa na bendi nyingine (siyo Vijana Jazz).
“Watu walikuja kushtuka baada ya kuniona hivyo, kumbe yalikuwa ni mashetani yananifanyia vituko, lakini sikujua,” anaongeza.
“Vitendo vya ajabu vilitufanya tuanze safari za kwa waganga kwa kuamini kuwa masheikh na wachungaji walikuwa wameshindwa
“Huwezi kuamini, kuna wakati nilikuwa nasikia mtu akiniita nje kwa kulitaja jina langu tena usiku wa manane.
“Siku moja Majid alitoka akiwa ameshika silaha kumuona huyo aliyekuwa akija usiku na kuniita, lakini alichokutana nacho, hakuweza kukieleza,” anasema.
Kida anasimulia kwamba, Majid alipigwa na upepo mkali na hakuweza kutambua kililichoendelea na aliporudi ndani alishindwa kusema chochote.
Kama vile haitoshi, mwanamuziki huyo alisema kuna wakati akiwa amelala usiku na kuzima taa, ghafla taa hiyo ilikuwa ikiwashwa na mtu asiyeonekana.
“Kutokana na vitu vilivyokuwa vikitokea, mara mnakuta damu nje ya nyumba mara vitu vingine visivyokuwa vya kawaida, ilitulazimu kuanza kutafuta waganga,” anabanisha.
Ajifungua salama, daktari asisitiza kuhusu Ukimwi
Kida anasema kuwa ulipofika muda wa kwenda kujifungua alifanikiwa kupata mtoto wa kike ambaye baba yake baadaye alikuja kumwita jina la Samia.
“Nilijifungulia kwa Dk Andrew ambaye kwa mara nyingine alinithibitishia kwamba sikuwa nimeambukizwa ugonjwa wa Ukimwi.
“Dk Andrew aliniambia kwamba hata nilipojifungua mara ya kwanza, mimba ya Cecilia, alijua kwamba sikuwa nimeambukizwa virusi vya ugonjwa huo,” anasema Kida.
Zawadi ya gari
Baada ya kujifungua salama na kwa kuwa Majid ambaye alikuwa nje ya nchi aliporudi alimpa zawadi ya gari.
“Majid alifurahi sana, akanipa zawadi ya gari, hapo ndipo aliponiambia maneno yote aliyokuwa akiyasikia juu yangu kuhusu kuumwa Ukimwi, penzi letu likaanza kuchanua upya,” anasimulia.
“Baada ya kujifungua, Majid aliniongezea mfanyakazi mwingine na kuwa na wafanyakazi wawili, hakutaka nipate tabu,” anasema.
Kida anasema katika maisha changamoto hazikosekani na siku zote watu hamuwezi kuwa na furaha muda wote, maisha yalibadilika baada ya maneno kuanza upya.
“Safari hii hayakuwa kuhusu ugonjwa wa Ukimwi tena, la hasha bali visa vingine kabisa, ambavyo viliuweka uhusiano wetu pabaya,” anasema.
Kida anasema kuwa baadhi ya watu wakasema kuhusu Majid kuwa na uhusiano na mwanamuziki, mwanamke wa Kiswahili na mengine mengi.
Mwanamuziki huyo anasema kuwa, Majid alikuwa akiendelea na safari zake na alikuwa akimwachia fedha za kutoka kama kawaida.
“Lakini baadaye mwanaume akabadilika na kuanza kuwa na wivu juu yangu, kitu ambacho mwanzo hakikuwapo kabisa,” anasema.
Mzimu wa Maneti watokea nyumbani
Kida anasema kabla ya kuendelea mbele kuna siku mzimu wa Maneti ulitokea nyumbani kwao.
“Siku hiyo, mimi na Majid tulikuwa tumesafiri kwenda kutembea mkoani Tanga, nyumbani tukiwa tumewaacha watoto Waziri, Cecilia na wafanyakazi wawili,” anasema.
Nini kiliendelea katika makala haya? Usikose kufuatilia Jumamosi ijayo.
Mwananchi
Pole sana dada Kida kwa manyanyaso. Kumbuka siku zote watu husema penye penzi hapakosi tezi. Ni wivu tu unawasumbua watu.
ReplyDeletehii kweli au nihadithi za hekalu/za simulizi za mama nyangoma
ReplyDelete