Samweli Ruhuza
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza jana alizimia ghafla wakati akihudhuria semina ya chama hicho na kupelekwa Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea saa 7.30 mchana katika Hoteli ya Lamada wakati chama hicho kikiendelea na semina ya mafunzo kwa viongozi wake.
Baadaye, Ruhuza alipatiwa matibabu na kurejea katika semina hiyo ya siku moja iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.
Akielezea tukio hilo akiwa hospitalini hapo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ambar Khamis alisema mara baada ya kumalizika kwa uwasilishwaji wa mada, Mbatia aliwaomba wajumbe kusimama ili kujinyoosha kutokana na baadhi kuwa wamechoka.
“Wote tulisimama lakini Ruhuza alibaki amekaa, Mwenyekiti (Mbatia) alimuuliza Ruhuza mbona husimami? Ruhuza alibaki amekaa akiwa amenyoosha mkono juu kuashiria kutokuwa sawa lakini akawa bado amekaa na akainamisha kichwa katika meza ndipo Mbatia akaniambia hebu nenda kamwone Ruhuza anaonekana kama hayuko sawa.
“Nilikwenda alipokuwa amekaa, nilipofika nikamshika mkono alikuwa wa baridi, nikamuuliza Ruhuza, vipi mbona umekaa? Ruhuza akasema ‘siko vizuri najisikia vibaya’. “Mwenyekiti alitueleza tumpeleke Hospitali ya Amana wakati huo alikuwa hajitambui.”
Akizungumza huku akiwa anatabasamu katika chumba cha dharura namba tano hospitalini hapo, Ruhuza alisema: “Unajua naumwa kisukari na ni miaka 15 sasa, lakini kwa kipindi chote sijawahi kupatwa au kukutwa na mkasa kama huu. Hii ni mara yangu ya kwanza.”
“Nakumbuka nilikuwa nimekaa katika ile semina ndiyo kumbukumbu yangu ya mwisho, nimezinduka na kujikuta nipo hapa kitandani nikiwa nimewekewa dripu, sukari ilishuka lakini sasa niko ‘fit’ na ninakwenda tena katika mkutano.”
Awali, semina hiyo iliazimia kwamba wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotokana na chama hicho watakaokaidi msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kutorejea bungeni, hawatatakiwa ndani ya chama hicho.
“Eti... atakayekwenda bungeni na kukaidi msimamo wa Ukawa anatakiwa ndani ya chama chetu?” Mbatia aliwahoji wajumbe ambao waliitikia kwa kelele “Hatakiwi...” na wakiimba wimbo wa sema... usiogope... sema.
Mbatia alisema: “Ukawa tunasimamia maoni ya wananchi na tunamwomba Rais Jakaya Kikwete kulisitisha Bunge hilo kwani halina uhalali wowote na linatumia vibaya fedha za walipakodi bila manufaa yoyote.
“Tunajua Bunge hilo lina vishawishi kwani kwa kipindi cha siku 84 kila mjumbe ataondoka na Sh22 milioni lakini Ukawa hatutarudi bungeni wao waendelee na kitu ambacho tunajua itakuwa ngumu kupatikana kwa theluthi mbili hasa kule Zanzibar.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake