Wataka asiteue marafiki
Washindwa kuafikiana
Mjadala wawekwa kiporo
Washindwa kuafikiana
Mjadala wawekwa kiporo
Wajumbe waliotofautiana na kulazimika kuziweka kando ibara hizo ili kuendelea kujadili ibara nyingine za Rasimu ya Katiba kuwa ni wa kamati namba 10 inayoongozwa na Anna Abdallah.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Salmin Awadh Salmin, alisema jana kuwa suala linalohusu madaraka na majukumu ya Rais limesababisha wajumbe wake kuvutana na kuamua ibara hizo ziwekwe kando hadi watakapoamua tena na kwamba wataendelea nazo baadaye.
“Katika maeneo ambayo yameleta mvutano ni suala la madaraka na majukumu ya Rais pamoja lile la utekelezaji wa madaraka yake, na tuliona watu wamechoka na wamevutana mno kwa hiyo tukaamua tuliache ili tuwape wajumbe fursa ya kutafakari zaidi na baadaye tukaendelea na ibara nyingine,” alisema.
Ibara hiyo ya 72 inafafanua kwa upana madaraka na majukumu ya Rais katika nafasi zake tatu, akiwa mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Ibara hiyo inaweka masharti kwa Rais kuepuka kujinasibisha kwa namna yoyote na chama chochote cha siasa au kundi lolote la jamii kwa namna ambayo itaathiri umoja wa wananchi wakati akiwa madarakani.
Ibara ya 73 inafafanua utekelezaji wa madaraka ya Rais ya uteuzi wa nafasi mbalimbali za viongozi na watendaji wakuu wa serikali ambao utathibitishwa na Bunge. Pia inaeleza kuwa katika kuanzisha au kufuta nafasi za madaraka, Rais atapaswa kuzingatia ushauri wa Mamlaka za Serikali, Bunge na Mahakama.
Mvutano huo wa madaraka ya Rais, pia uliibuka katika kamati namba 12 inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti ambayo wajumbe wake, wamevutana kwa muda mrefu katika eneo la uteuzi wa Rais, wakitaka wapate nafasi ya kuliangalia vizuri zaidi kabla ya kulipeleka katika Bunge Maalum la Katiba.
“Tumeona kwa nini tumpe Rais mzigo mzito wa uteuzi kwa sababu yeye pia ni binadamu, anaweza kumteua mtu akidhani atamsaidia kumbe wenzake wanamtazama vibaya na baadaye wakamkataa. Tumesema hili tutalipeleka kwenye Bunge Maalum tukalijadili wote kwapamoja," alisema na kuonya kuwa:
"Wajumbe wa kamati yangu wengine wanataka Rais apunguziwe madaraka yake na wengine wanataka aachiwe kama ilivyo kwenye Katiba ya sasa…ndugu zangu, ukifanya makosa katika suala la uongozi utakuwa umeitumbukiza nchi yako katika maangamizi.”
Nazo taarifa zilizopatikana kutoka kamati namba 5 inayoongozwa na Hamad Rashid Abdallah zinaeleza kuwa suala la umri wa Urais limezua mjadala mkali huku baadhi ya wajumbe wakitaka kuongezwa kwa kipengele cha afya ya mgombea.
Wajumbe wa kamati hiyo wanataka katiba ijayo itamke kwamba mgombea Urais atakuwa ni mtu mwenye afya njema huku baadhi ya wajumbe wakipinga kwa madai ya kutopata tafsiri halisi ya mtu mgonjwa na mzima.
WENGINE WARIDHIKA
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa kamati namba 11, Almas Maige, alisema kuwa wajumbe wote wameridhika na mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kuhusu madaraka na majukumu ya Rais na kupendekeza yabaki kama yalivyo.
“Sisi tumeridhika na mapendekezo yaliyopo katika Rasimu kuhusu madaraka na majukumu ya Rais na kwenye kamati yetu hapakuwa na mvutano mkubwa sana. Na sisi hatujabadili chochote,” alisema Maige.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Editha Majura na Salome Kitomari.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake