Monday, August 18, 2014

MPISHI: Huikabili homa hivi

Wiki iliyopita tuliona jinsi mpishi anavyoweza kuukabili ugonjwa wa kisukari kwa uhakika kabisa. Mpishi bado ana nafasi kubwa sana ya kuokoa maisha ya walaji wake tena katika hali ya hatari ya kufa kwa maradhi yasiyoeleweka kama homa. Kila mtu anaijua kwa uhakika sana homa. Hakuna hata mmoja wetu ambaye hawahi kuugua homa kote ulimwenguni na kibaya zaidi homa hutukumba zaidi watu tulioko kusini mwa jangwa la sahara na hushambulia zaidi akina mama na watoto wenye umri chini ya miaka 15 Watanzania tukiwemo kundini.
Nikushangaze msomaji wangu kuwa homa sio ugonjwa! Ndio, homa ni maumivu tu au ‘shabiki’ wa maradhi mengine yanayotukumba binadamu. Kwa kawaida mwili ukikutana na shambulio lolote liwe la bacteria, virusi au hata kisaikolojia basi joto litapanda na mtu atajisikia maumivu na hali hiyo ndio kitaalamu inaitwa ‘Homa’

Ukiwa na homa, protini na virutubisho vingi sana hupotea mwilini huku hamu ya kula nayo hukata na kupotea kabisa. Hii humfanya mgonjwa kupoteza uzito na ikimlaza kwa muda mrefu hupooza na baadaye anaweza akapoteza maisha asipotibiwa. Hali hii hutokana na kupoteza vitamins B complex na vitamin C kwa wingi sana kupitia mkojo wa njano ambao wote tukiugua hukojoa hivyo.
Mgonjwa anapofikia hatua hii, Mpishi husaidia kuokoa maisha yake kwa kumpa vyakula vyenye protini kwa wingi japo mgonjwa husumbua kidogo kutokana na homa kumpotezea hamu ya kula ila kama atakuwa anatapika pia basi kazi itakuwa ngumu sana na mpishi anaweza akaagiza mgonjwa apewe ‘vitamins supplements’ za vidonge ili kujazia mlo wake kwa usahihi na haraka apone. Bado Mpishi atatakiwa ahakikishe mdomo wa mgonjwa ni safi muda wote maana homa huzalisha taka mdomoni na kumfanya mgonjwa akate hamu ya kula pia. Mpishi anaweza akampa kachumbari mara kwa mara na akaona maajabu!

Homa huwa za muda mfupi, zipo za muda mrefu na zipo homa za kujirudia mara kwa mara pia. Kwa homa za muda mfupi kama vile malaria, typhoid, kuharisha n.k. Mpishi atampikia mgonjwa wake vyakula vya kimiminika tu kwa siku mbili mfululizo ili kwenda sambamba na upotevu wa maji mwilini na pia mgonjwa ataweza kula kwa urahisi. Juisi, maziwa, uji, supu, mtori n.k. vitamfaa sana mgonjwa na endapo atakojoa mkojo kiasi cha lita mbili ni dalili wazi kuwa anapona.


Kwa homa za muda mrefu zinazojishabikia katika maradhi kama vile kifua kikuu, ukimwi, majeraha ya upasuaji, saratani, na hata ajali pia Mpishi atahakikisha mgonjwa anapata vyakula laini na kidogokidogo walau milo mitano kwa siku ili mgonjwa aweze kwenda sambasamba na uharibifu unaosababishwa na homa. Msisitizo upo katika vyakula vyenye maji zaidi kwa sababu homa hupoteza maji mengi kupitia jasho la stress, mkojo, kutapika nap engine hata kuharisha pia. Hivyo Mpishi humpa mgonjwa vimiminika kwa wastani wa lita 2 hadi 3 katika mfumo wa lishe ili arudishe madini, vitamin na virutubisho vingine pia na uhakika wa mgonjwa kupona ni mkubwa na uhakika.
Nadhani tumeelewa vizuri namna anavyoweza kuikabili homa. Bado mpishi ana uwezo wa kuyakabili maradhi kibao! Usikose makala hii kila jumanne kwani bado tunaendelea kukuletea pilikapilika za mpishi jikoni akiwapikia wagonjwa wa maradhi tofauti. Unaweza ukawa na swali, hoja, maoni au ushauri wa kina juu ya Mpishi. Usisite kutupigia na kutembelea tovuti yetu hapo juu.
John Haule
0768 215 956

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake