Sunday, August 17, 2014

MWANAFUNZI WA TANZANIA AIBUKA MSHINDI WA KWANZA TUZO YA INSHA SADC

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wakuu na wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika SADC muda mfupi baada ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa jumuiya hiyo uliofanyika katika hoteli ya Elephant Hills mjini Victoria Falls Zimbabwe leo.Katikati ji mwenyeji wa Mkutano huo Rais Robert Mugabe na Dkt Stergomena Tax [katibu mkuu wa SADC] na kwa upande wake wa kushoto ni Nkosazana Dlamini-Zuma (Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika)

Mtoto wa Kitanzania, msichana Neema Steven Mtwanga, ameibuka kinara katika Mashindano ya Utunzi wa Insha katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa washindani 39 waliowania Tuzo ya Utunzi wa Insha hiyo kwa Mwaka 2014.
Msichana Neema Steven Mtwanga, 16, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe.
Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland.
Kwa ushindi huo, Neema Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya mawasiliano na habari.
Mashindano hayo ya Insha ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: “Climate Change is having adverse effect on the socio-economic development in the Region. What should the Education Sector do to mitigate the impact on the youth” – Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye kupunguza athari hizo kwa vijana?
Insha 39 zilipokelewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai, mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani washindi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa SADC umepokea kwa furaha ushindi wa msichana Neema ukieleza kuwa ushindi huo umeiletea Tanzania heshima kubwa katika eneo la SADC na nje ya eneo hilo. 

Imetolewa na; 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, 
Ikulu – Dar es Salaam. 
17 Agosti,2014

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake