Monday, August 18, 2014

Mwigulu:Nimeombwa kugombea urais 2015

  Adai kutumiwa ujumbe na wazee kutoka Butiama
  Pia wapo vijana wa kutoka vyuo vikuu
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
Wakati baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kupigana vikumbo kuwania urais wa 2015, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amesema ameombwa na watu mbalimbali wakiwamo wazee na wasomi kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo, Nchemba amesema kwa sasa hafikirii suala hilo kwani amebanwa na utekelezaji wa jukumu alilokabidhiwa na Rais.

Nchemba, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini.
Alisema amekuwa akipokea ujumbe mwingi kutoka kwa wazee wa kijiji cha Butiama, mkoani Mara na kutoka kwa vijana wa vyuo vikuu wakimuomba awanie urais mwaka 2015, lakini suala hilo haliwekei umuhimu.


Badala yake, alisema anatekeleza jukumu kubwa alilopewa na Rais la Naibu Waziri wa Fedha.

Wakati Nchemba akitoa kauli hiyo, zipo taarifa kuwa aliwaalika makatibu wa CCM wa wilaya kutoka mikoa 11 kuhudhuria mkutano aliokuwa ameundaa jijini Mwanza siku ya Idd Mosi na Idd pili.

Pia mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa mkoa wa Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba, na mkutano mwingine wa ndani uliofanyika katika hoteli moja maarufu jijini Mwanza usiku, inadaiwa kwamba aliigharimia yeye.

Nchemba anadaiwa kulipia gharama za makatibu hao kutoka vituo vyao vya kazi kwa maana ya usafiri na posho.

Mbali na mkutano wa Mwanza, Nchemba anadaiwa kuwaalika tena makatibu wa CCM 51 mjini Dodoma wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu na kuwagharimia usafiri, posho na malazi.

Wakati akilipa gharama hizo, kwa miezi ya Juni na Julai, vyama vya siasa vilikuwa havijapewa ruzuku na kwa kiasi kikubwa watendaji wote wa CCM kama walivyo wa vyama vingine vya siasa, walikuwa hawajalipwa mishahara yao ya Juni na Julai.

Makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya Tanzania Bara kimsingi wanawajibika kiutendaji kwa Nchemba kama Naibu Katibu Mkuu CCM Bara.

Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE katika mahojiano kwa simu jana, alisema kimsingi kila kazi nzuri inayofanywa na kiongozi inawafanya watu waone ni harakati za kutaka urais 2015 japo ndiyo kipimo cha kuaminiwa.

“Nilichosema wakati nahojiwa na kituo cha televesheni nilisema sitangazi, lakini nafanya kazi niliyopewa ya Naibu Waziri wa Fedha hivyo lazima nihakikishe bajeti ya serikali inatekelezwa,”alisema.

Nchemba alisema yeye ni kiongozi wa chama anayepaswa kuwa mfano wa kuheshimu kanuni na taratibu za chama hivyo hawezi akakurupuka na kutangaza kwamba atawania urais.

“Mwanza nilifanya mkutano wa hadhara ambao msingi wake ilikuwa ni kusisitiza masuala ya kodi na ajira,”alisema.

Pia alisema hakulipia gharama za makatibu waliosafiri hadi Mwanza, kwa kuwa chama kina taratibu za kulipia watendaji wake gharama kama hizo.

Nchemba anakuwa kiongozi wa pili ndani ya CCM na serikali kutamka hadharani ama anautaka urais au anasukumwa na watu kujitokeza kuuwania mwaka 2015.

Mwingine ni Naibu Waziri wa Sayansi na Tekinolojia, January Makamba, ambaye alisema kwamba amekwisha kufanya kazi ya kujiandaa kwa asilimia 90 na kilichobaki ni kuonana na viongozi wa dini tu.

Wapo wanachama kadhaa ambao wameonyesha nia ya kutaka kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM.

Miongoni mwao ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Akizungumzia suala la ajira, Nchemba alisema kuna haja kwa wananchi kuachana na fikra kuwa ajira pekee ni ile ya kuajiriwa serikalini.

Alisema ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini, halmashauri za wilaya na majiji zinatakiwa kuhakikisha zinapopima viwanja vya makazi, zinafanya hivyo kwa kutenga maeneo ya uwekezaji ambako kutajengwa viwanda vitakavyotoa ajira kwa vijana.

Alitaka kuwapo na muda maalum kwa mwekezaji anayepewa eneo la uwekezaji na anaposhindwa kuliendeleza, anyang’anywe na kupewa mwingine.

Alisema hilo litasaidia kuondokana na tatizo la baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo ya uwekezaji na kushindwa kuyaendeleza kwa muda mrefu.

Nchemba alisema kumekuwa na tatizo la ukosefu wa uadilifu na bidii ya kufanya kazi kwa baadhi ya wananchi wanaopewa fursa ya kazi.

Alisema hali hiyo wakati mwingine inawafanya wawekezaji hususan nchini, kuchukua hatua ya kuajiri watu kutoka nje ya nchi.

“Kuna baadhi ya nchi kama Marekani, mfanyakazi anapokuwa kazini, haruhusiwi hata kuongea na simu au kusoma gazeti. Lakini hapa kwetu watu hawaonyeshi bidii ya kufanya kazi kwa lengo la kuongeza uzalishaji,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

  1. Wagombea CCM mbona kazi - pick one and start campaigning as usua
    1. January Makamba
    2. Mwigulu Nchemba
    3.Sitta
    4. Lowassa
    5. Sumay
    6. Ngeleja

    ReplyDelete
  2. Sitta, lowassa, sumaye.Muda wao umepita

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake