Thursday, August 14, 2014

SERIKALI YATAKIWA KUTIMIZA AHADI ZA UJENZI WA ZAHANATI KWA KILA KATA

DSC_0534
Diwani wa kata ya Ololosokwani na Mkurugenzi wa Irkiramat Foundation (RAMAT) Bw. Yannick Ikayo Ndoinyo akiangalia kitanda cha kujifungulia wakimama kwenye Zahanati ya Sero ambayo kwa siku inatibu wagonjwa 50 na zaidi ikiwa na daktari mmoja huku wakazi wanaofuata huduma hiyo kutoka kata hiyo na ya jirani Soitosambu kutembea umbali mrefu kwa Kilometa 7-15 kupata huduma ya afya.(Picha Zainul Mzige wa MOblog)

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
Wakazi wa vijiji vya Ololosokwan, Soit-Sambu, Njoroi na Loipir kata za Ololosokwana na Soit-Sambu wilayani Ngorongoro wanakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya Afya kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo kwenye kijiji cha Sero huku waathirika wakubwa ni kinamama na watoto.
Umbali wa zahanati hizo imekuwa sababu kubwa ya vifo hususani kwa akina mama wajawazito wanaotaka kwenda kujifungua na watoto halikadhalika wanapozidiwa hufia njiani kutokana na umbali wa zahanati kutoka kijiji kimoja kwenda kingine wanapotakiwa kuwahishwa hospitalini hali inayowafanya kutembea umbali mrefu kilometa 15 hadi kuipata huduma ya zahanati .
Akizungumza na waandishi wa habari Diwani wa kata ya Ololosokwani na Mkurugenzi wa Irkiramat Foundation (RAMAT) Yannick Ikayo Ndoinyo waliotembelea miradi inayofadhiliwa na Shirika la Elimu na Sayansi (UNESCO) wilayani humo alisema serikali haina budi kutimiza ahadi yake ya kujenga Zahanati kwa kila kata nchini Tanzania kuwapunguzia wagonjwa hususan akina mama waja wazito na watoto adha ya kutembea au kusafiri mwendo mrefu kutafuta huduma za afya.
Ndoinyo alisema kuwa tatizo kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya afya lipo na kwamba vifo ya wamama na watoto na kutopata huduma zinazotakiwa kwa wakati. Wananchi hupata huduma za afya kutoka Sero ambayo ina umbali mrefu kutoka Ololosokwang au wakati mwingine mgonjwa hupata rufaa rufaa hadi Hospitali ya wilaya ya Waso na iwapo mgonjwa atakuwa katika hali mbaya ni tatizo.
DSC_0532
Gari la wagonjwa lilitolewa na serikali likiwa limeharibika kutoka na miundo mbinu ya barabara na kushindwa kufanyiwa matengezo kwa muda mrefu hali inayomfanya daktari wa Zahanati hiyo kuwafuata majumbani wagonjwa mahututi kwenda kuwapatia huduma za afya.

“Utakuta wagonjwa inabidi watembee umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya kwenye zahanati ya Sero hili ni tatizo tunaiomba serikali yetu kuliangalia ili kuokoa vifo vya mama na mtoto”alisema diwani.
Ndoinyo alisema kuwa pamoja na daktari kuwatembelea akina mama na watoto ili kutoa huduma za afya majumbani kwao kumekuwa na changamoto mbalimbali hususan vifaa vya vipimo vya kupima magonjwa mbalimbali.

Nae Mkunga wa jadi Mama Naani alisema mtihani mkubwa unakuja pale wakati mama mjamzito anapotaka kujifungua na anahitaji huduma ya ziada, hakuna vifaa na kumlazimu mgonjwa au mama mjamzito kuembea umbali mrefu kupata huduma hiyo hospitalini.
Madhumuni ya ziara hiyo inayowashirikisha wawakilishi kutoka Kampuni ya Samsung na mwakilishi kutoka ubalozi wa Uswiss hapa nchini ni kujionea miradi mbalimbali inayoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inayotekelezwa na redio ya Jamii Loliondo wilayani Ngorongoro.
Miongoni mwa miradi inayofadhiliwa wilayani humo ni pamoja na Redio Loliondo ambayo pia inafadhiliwa na kampuni ya simu za mikononi ya Airtel kwa kurusha matangazo yake kupitia mnara wa kampuni hiyo na Mradi wa Maktaba unaolenga kuwapatia wanafunzi uelewa wa mambo mbalimbali yanayohusu masomo ya sayansi.
DSC_0540
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph, akishanga kitanda cha kujifungulia wakinamama kwenye zahanati hiyo ambayo ina uhaba wa vifaa mbalimbali vya matibabu huku halmashauri ikishindwa kumalizia majengo ya wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa ambapo imeonyesha wakina mama na watoto wamekuwa wakifia njiani kutokana na kutembelea umbali mrefu kufuata matibabu.
DSC_0544
Vifaa vinavyotumika kwenye zahanati hiyo wakati wakinamama wanapojifungua, jingine ni Friji kwa ajili ya kuhifadhia chanjo mbalimbali za watoto na kinamama linalotumia umeme wa jua.
DSC_0559
Daktari wa Zahanati ya Sero kata ya Ololosokwani Dkt. Veronika Nyoni (katikati) akielezea changamoto mbalimbali anazokumbana nazo katika kutoa huduma ikiwemo Umeme na kupelekea kutumia tochi wakati wakinamama wanapojifungua ambapo ameiomba serikali kupitia wafadhili mbalimbali kuwasogezea hata huduma ya umeme jua ili kukabiliana na changamoto hizo.Kulia ni Mwanahabari wa gazeti la Zanzibar leo, Mahmoud Ahmad na kushoto ni Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph wakimsilikiliza kwa makini Dkt. Nyoni.
DSC_0583
Diwani wa kata ya Ololosokwani na mkurugenzi wa Irkiramat Foundation (RAMAT) Bw. Yannick Ikayo Ndoinyo akiwa na wadau wa maendelo wakiongozwa na UNESCO waliofanya ziara katika kata ya Ololosokwani wilayani Ngorongoro. Katikati ni Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph na kulia ni Meneja Mauzo wa Kampuni ya Samsung tawi la Tanzania, Bw. Slyvester Nteere.
DSC_0585
Nyumba ya Daktari Mstaafu aliyekuwa akitoa huduma katika zahanati ya Sero zaidi ya miaka 25 kama inavyoonekana ikiwa na Umeme wa jua pamoja na Dish ikiwa ni maendeleo katika eneo hilo lililopo karibu na pori tengefu la Loliondo.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake