Wamo Lembeli,Kessy,Ester Bulaya

Kadhalika, wametakiwa kutowazungungumzia wajumbe wa Ukawa wakati wa mijadala ndani ya bunge hilo.
Msimamo huo ambao ulitolewa juzi usiku, unaonekana kuwalenga baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kupitia CCM ambao wamekuwa wakitamka bayana kwamba Bunge la Katiba lisitishwe kutokana na hofu ya kutotimia idadi ya theluthi mbili wakati wa upigaji kura kutokana na Ukawa kususia bunge hilo.
Baadhi ya wajumbe hao wa CCM ambao wamekuwa wakitamka hivyo ni pamoja na Mbunge wa Iramba Magharibi na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara ambaye pia Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Nkasi Mashariki, Ally Kessy, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aishi Hilal.
Wajumbe hao wa Bunge Maalum la Katiba kupitia CCM, walikutana kwa lengo la kujipanga kwa ajili ya mijadala juu ya masuala yaliyoleta mvutano mkubwa wakati wa mijadala ndani ya Kamati za bunge hilo na kushindwa kufikia mwafaka.
Kikao hicho kilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema msisitizo mkubwa uliowekwa na Pinda kwa wajumbe hao, ni juu ya masuala hayo.
Chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya kikao hicho kililiambia NIPASHE kuwa kikao hicho kiliitishwa kutokana na kuwapo kwa kauli za kukinzana kutoka kwa wajumbe hao juu ya Bunge la Katiba na jinsi ya kushughulikia masuala yaliyokwama kwenye kamati.
“Pinda alitutaka kuwa makini na kauli hasi tunazotoa kuhusiana na Bunge la Katiba kwani zinaweza kuathiri kupatikana kwa Katiba mpya. Pia alitutaka kuweka utaifa mbele wakati wa mijadala hasa katika mambo yaliyoleta mvutano kwenye kamati na kushindwa kupatikana mwafaka,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, wajumbe hao walitakiwa kujadili kwa kina na kwa umakini mkubwa Rasimu ili Katiba itakayopatikana iwe bora na yenye manufaa kwa wananchi na kuepuka kuwazungumzia Ukawa ili kutotoa nafasi kwa watu wasiotaka Bunge hilo liendelee kuwashambulia.
Hata hivyo, chanzo hicho hakikutaka kwenda kwa undani zaidi juu ya kikao hicho ambacho kilifanyika wakati Bunge Maalum la Katiba likiwa linapokea taarifa za kamati mbalimbali kabla ya kuanza kwa mijadala.
Akizungumza na NIPASHE juzi kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, mmoja wa wajumbe hao alisema walikuwa wakikutana kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na Bunge hilo, ikiwamo kujitokeza kwa mgawanyiko mkubwa miongoni mwao.
Alisema kinafanyika kufuatia kuibuka kundi la wajumbe wanaopinga kuendelea kwa Bunge hilo, wakitoa hoja kwamba halina uhalali kwa sababu halitatoa Katiba mpya kutokana na kukosa theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar watakaopitisha katiba hiyo.
“Ukweli kuna wajumbe wenzetu wamejitokeza kupinga Bunge hili, msimamo wao unatushangaza na kutuletea maswali mengi ambayo hatuna majibu ya kutosha, huko watakuwa na uhuru kueleza kile wanachokiamini,” alisema mjumbe mmoja kuhusiana na kikao hicho.
Mjumbe huyo alisema kwamba wanachoamini wajumbe wengi wa CCM kuwa kundi hilo limechanganyikiwa kutokana na sababu za kisiasa hasa wakati huu wanapoelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kwa upande wa Mwigulu, amekuwa akitaka Bunge hilo kujiridhisha kwanza kama litapata theluthi mbili kwa pande zote Tanzania Bara na Zanzibar wakati wa kupiga kura ya kufanya maamuzi.
Alionya kuwa endapo Bunge hilo litaendelea na mwisho wa siku kushindwa kufanya maamuzi, litakuwa limefanya matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na wananchi watachukizwa na kitendo hicho.
Kwa upande wa Filikunjombe, amekuwa akitaka Bunge hilo liahirishwe ili kutafuta maridhiano kwanza baada ya wajumbe wa Ukawa kususia ili Katiba itakayopatikana, ikubalike na Watanzania wote.
Aeshi kwa upande wake, amekuwa akitaka Bunge hilo lisitishwe ili kutoa nafasi kwa kufanyiwa marekebisho mfumo wa uchaguzi ikiwamo kurekebishwa kwa Sheria ya Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani, kwani Katiba mpya itakayopatikana itaanza kutumika mwaka 2018.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment