Advertisements

Thursday, September 11, 2014

DAUDA NA PROF JAY (www.shaffihdauda.com )

Na Shaffih Dauda
MUZIKI wa ‘Hip Pop’ unazidi kuchanua nchini Tanzania na kumekuwa na mabadiliko makubwa sana kwa miaka ya karibuni, lakini huwezi kuuzungumzia muziki huu bila kutaja jina la Joseph Haule.
Huyu ni msanii maarufu na amedumu kwa muda mrefu katika muziki huu wa kizazi kipya. Jina lake la kisanii linalofahamika na wengi ni Proffesor Jay ‘Mzee wa Mitulinga’.
Tusemapo ni mkongwe, kweli ni mkongwe, kwasababu historia yake inaonesha alianza harakati za muziki miaka 1990 akipitia makundi mbalimbali, kabla ya kuwa msanii binafsi mwaka 2001 na kuendelea.
Akijitegemea, Professor Jay amefanya vizuri na kushinda tuzo mbalimbali za muziki nchini.
Lengo si kuzungumzia mafanikio ya mwanamuziki huyo kwani ana historia ndefu na ameshinda tuzo nyingi kutokana na ubora wake, lakini leo maisha ya upande wa pili yanaangaliwa zaidi.
Ni kawaida kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutumia muda wao wa ziada kufuatilia michezo mingine ndani na nje ya nchi, hususani mpira wa miguu.
Kuna wasanii wengi maarufu nchini wanashabikia timu za ndani na nje ya nchi, lakini walio wengi kwa soka la ndani ni Simba na Yanga.
Dauda TV kama kawaida imeendelea kukutana na wasanii tofauti wa muziki wa kizazi kipya. Hili ni kundi la watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii yoyote duniani kama wanaweza kutumika vizuri na wadau ili kufikisha ujumbe.
Professor Jay ni mmoja wa Wasanii wanaopenda sana soka. Unajua anashabikia timu gani ndani na nje ya nchi? Jibu ni Simba na Liverpool.
Katika mahojiano maalumu na Dauda TV, Professor Jay amefurahishwa sana na jinsi timu yake ya Simba inavyoimarika chini ya kocha Patrick Phiri na Liverpool chini ya Brendan Rodgers.
Mkali huyo wa ‘Hip pop’ alisema ujio wa Emmanuel Okwi kwa mara ya pili umempa faraja sana na ni ukweli Simba itakuwa hatari. Pia alikiri kumpenda Paul Kiongera aliyesajiliwa kutoka Kenya majira ya kiangazi mwaka huu.
Professor Jay alisema: “Okwi, kiongera nawapenda wote. Unajua sahizi Simba inatia hamu. Napendaa ‘football’ kwa sababu inafurahisha, jinsi inavyocheza napenda sana,”.
“Napenda sana muziki, lakini napenda sana mpira wa miguu. Kuna wachezaji nimeanza kuwafuatilia toka zamani na natamani wasingestaafu, mtu kama Mohamed Mwamweja, namkubali sana”.
Katika mahojiano hayo, Professor Jay aliongeza kuwa ujio wa Okwi Simba ni jambo jema na umemrudisha nyuma hususani kipigo walichotoa cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga mwaka 2012.
Professor alisema mechi hiyo kamwe hawezi kuisahau kwasababu ilikuwa raha kwake ambapo Okwi alifanya kazi nzuri kuimaliza Yanga, hivyo kurejea kwakwe anaona kipigo kingine kipo njiani.
“Okwi karudi, Simba imekuwa safi. Natamani sana hizo mechi za ligi kuu zianze”. Aliongeza Professor Jay.
Kuhusu Liverpool, mwamba huyo wa ‘Hip Hop’ alisema kwa miaka mingi sana klabu hiyo haifanyi vizuri, lakini msimu uliopita ilikaribia kutwaa ubingwa.
Aidha, alisema Liverpool iko vizuri hususani kwa usajili wake akiwemo mshambuliaji mtukutu aliyesainishwa kutoka AC Milan, Super Mario Balotelli.
“Liverpool tumefungwa sana, lakini sahizi tunakuja vizuri. Balotelli (Mario) yupo pale, tutafanya vizuri. Liverpool kama kawaida sahizi, Balotelli kaingia pale”. Professor Jay alisisitiza ujio huo wa Balotelli
Mwisho wa yote, mtu hapotei asili yake. Ghafla Professor Jay katika mazungumzo yake alirejea katika muziki.
Alisema kuna wimbo mkali amefanya na Diamond Platinumz unaitwa ‘Kipi Sijasikia’.
Huu ni wimbo maarufu sana kwa siku za karibuni na umekuwa ukipigwa sana kwenye vituo vya redio na TV, kuandikwa kwenye mitandao na magazeti na kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Professor Jay alisema: “Nimefanya wimbo mzuri na Diamond, umesikika sana, umepigwa sana na nilichokifanya sasa ni kutengeneza video yake. Siku ya Jumamosi maeneo ya Makunbusho Victoria nitafanya uzinduzi wa video hiyo. Kuna video mbili kali nazindua siku hiyo. Pia nitazindua tovuti yangu inaitwa www.professorjay.com”.
Wakati mahojiano yanaendelea, msanii mwingine anaangalia kwa mbali. Mwandishi analazimika kumuita ili atoe lake la moyo.
Jamaa alianza kwa kusalimia, ghafla mwandishi kamtupia swali akisema Professor Jay ni shabiki wa Simba na Liverpool, wewe je”
Jamaa kafunguka: “ Mimi kama kawadia Simba, Man United ingawa mmetusema sana , lakini ndio hivyo. Brazil ingawa tumefeli mwaka huu, sio kesi, Real Madrid kama kawaida.
Bila shaka una hamu ya kumjua ni msanii gani, huyu ni msanii mwingine wa muziki wa kizazi kipya, Cpwaa.
CREDIT:SHAFFIHDAUDA

No comments: