Capt. John Chiligati ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Kamati mpya ya Uongozi ya Mkurabita
“NIMSHUKURU Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete kwa kuniona na kuniamini na hivyo, kuniteua ili niweze nami kuvaa kiatu anachokiacha Mheshimiwa makinda”. Anasema, Kapteni Mstaafu wa John Chiligati ambaye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika hafla ya uzinduzi wa Kamati mpya ya Uongozi wa Mpango wa Kuratibu na Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) na kuwapongeza wajumbe wa Kamati hiyo waliomaliza muda wao. Katika hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Dar es Salaam Serena jijini Dar es Salaam, Chiligati ambaye ameteuliwa na Rais Kikwete hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Uongozi ya Mkurabita akichukua nafasi iliyotumikiwa kwa takriban miaka 10 na Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, akasisitiza, “Kwa mtazamo tu wa haraka, kiatu hiki ni kikubwa kweli kweli, lakini naamini kwa ushirikiano kutoka kwa wajumbe wenzangu, watendaji wa Mkurabita, Waziri na Ikulu yote pamoja na wadau wote na wapenda maendeleo, tutaweza kutekeleza kazi hii kwa ushindi mkubwa.” Anaongeza, “Hii ni kwa kuwa kweli nimeona nia thabiti ya Serikali ya kutaka kuinua uchumi wa nchi yetu kupitia rasilimali ardhi na biashara halali zinazoendeshwa na Watanzania…” Mwenyekiti huyo (Chiligati) alisema katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Kamati mpya kuwa, endapo Mkurabita utaeleweka zaidi kwa umma na malengo yake kutekelezwa ipasavyo, uchumi wa nchi utaimarika. Akasema, “Naomba Mungu atusaidie mimi na wenzangu ili nia hii ya kusisimua uchumi wa nchi yetu kupitia urasimishaji iweze kuwa ya kweli.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mkurabita inayomaliza muda wake, Anne
Makinda akasema lengo la Serikali kuanzisha Mkurabita ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia rasilimali na biashara zao ambazo ni rasmi. Akasema, “Mkurabita imepewa wajibu wa kuhakikisjha rasilimali na biashara zinazoendeshwa nje ya mfumo unaotambulika kisheria zinakuwa rasmi na hivyo, kutambulika kisheria.” “Matokeo ya tathmini ya sekta isiyo rasmi iliyofanywa na mtaalamu kati ya mwaka 2004 na 2005 yalionesha kuwa, asilimia 89 ya ardhi na asilimia 98 ya biashara hazikidhi matakwa ya kisheria. Thamani ya rasilimali hizi ni jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 29. 3 alizozitaja kuwa ni mtaji mfu.” Kwa mantiki hiyo, Makinda alisema kazi ya kurasimisha rasilimali hizo inategemewa kufufua mtaji huo mfu na kuufanya kuwa mtaji hai utakaochangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa taifa. “Kamati ya Uongozi imepewa mamlaka na wajibu wa kuzisimamia kazi hizi zinazofanywa na Kitengo cha Uongozi kwa kuzingatia mpango kazi ulioidhinishwa na sera na miongozo mbalimbali ya Serikali,” akasema Makinda. “Naishukuru Ofisi ya Rais Ikulu kupitia Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo ambao kwa kweli, wamekuwa wazazi wema kwa Mkurabita. Pia, niwapongeze wajumbe wapya na kuwakaribisha katika gurudumu hili ambalo Watanzania wengi wangependa wafanye, lakini jukumu hili muhimu limewaangukia ninyi kwa niaba ya Watanzania wote. Hivyo, naomba tafadhali sana muifanye kazi hiyo kwa moyo na kwa umakini kubwa maana ni kazi inayohitaji kujituma kwelikweli.” Akawasisitiza wajumbe wa Kamati mpya akisema, “Anzeni kwa kuielewa dhana yenyewe ya urasimishaji na nafasi yake katika kupunguza umaskini na kukuza uchumni wa taifa. Mtakapoielewa dhana hii vizuri, ndipo mtaweza kuongoza vema na hata kuwa washauri kwa Serikali.” Makinda mbele ya walioshiriki hafla hiyo alisema Watanzania wana kiu ya kupata mnaendeleo ili watoke katika lindi la umaskini uliokithiri. “Tuwasadie kutii kiu yao ya maendeleo kwa kuwezesha rasilimali na biashara zao kutambulika kisheria,” alisema. Mwenyekiti Mstaafu huyo akasema kazi ya kuwajengea uwezo Watanzania kuzitumia rasilimali zilizopo ambayo Mkurabita wameianza, ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu ya Nne ya mipango inayohusu utunzaji wa mitaji na utawala bora. Akaasa, “Lisimamieni hili ili kazi ya urasimishaji iweze kupata thamani sahihi kwa watu kupata mitaji zaidi.”
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mkurabita, Seraphia Mgembe alimpongeza Makinda akisema amejituma kwa mwili na roho kuhakikisha shughuli za Mkurabita zinafanyika na kutimizwa ipasavyo. Mgembe akamwmbia Makinda katika hafla hiyo, “Tangu mwaka 2004 Mkurabita ilipoanza umekuwa mstari wa mbele kutuongoza, kutuelekeza na hata kututafutia fursa pale uipoona inafaa. Ilipobidi kututetea, ulifanya hivyo kwa nguvu zako zote.” Mgembe akakumbusha namna Makinda alivyomtia moyo alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mratibu wa Mkurabita, “Nakumbuka siku nilipoteuliwa na Rais kusimamia shughuli za Mkurabita nilisema hivi kiatu hiki nitakiweza kweli? Mbona naona ni kikubwa?... Nyie mlinitia moyo mkisema, nitaweza tu na hata ikiwezekana, mtaniwekea vitambaa kwenye kiatu ili kinitoshe… Ninawashukuru sana na ninaamini ndiyo sababu tumeweza kufanya yote tuliyoweza kufanya.” Akamgeukia Kapteni Chiligati na kumwambia, “Tunatambua uzalendo wako kwa taifa hili na tunaamini kwa pamoja tutatimiza nia ya Serikali ya kujenga uchumi rasmi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria. Mheshimiwa Rais hakukosea kutupatia wewe. Niwapongeze pia wajumbe wako na niahidi kuwa Wana-Mkurabita ni majembe ya uhakika na wako tayari kabisa kufanya kazi usiku na mchana…” Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utaribu na Mahusiano) Stephen Wasira kabla ya kuzindua rasmi kamati hiyo, aliipongeza Mkurabita akisema weledi, ubunifu, nidhamu na moyo wa kujituma, ndio umeiwezesha kufanya kazi zake katika halmashauri 50 kwa ajili ya ardhi vijijini, halmashauri 11 kwa ajili ya ardhi mijini na halmashauri 12 kwa ajili ya biashara. Katika pongezi zake, Waziri Wasira alizipongeza kamati zote akisema, “Nianze na Mwenyekiti Mh. Kapteni John Chiligati ambaye ameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kupokea kijiti kilichoshikwa na Anne Makinda toka 2004 hadi sasa. Si kazi nyepesi, lakini tunaamini uteuzi wako ni sahihi kabisa na kwamba Ofisi ya Rais, Ikulu, pamoja na Mkurabita wenyewe, tutakupa ushirikiano unaohitajika ili kukuwezesha kutekeleza wajibu huu mkubwa wa kitaifa.” Akaongeza, “Nikirudi kwa wajumbe ambao ni wateule wangu, nina imani hamtaniangusha na hamtamuangusha Mwenyekiti wenu. Katika uteuzi tumejitahidi kuzingatia uhusiano wa kisekta wa kazi zenu na malengo ya Mkurabita. … Ajenda ya urasimishaji ni pana na ni matamanio ya Serikali kufanya Mkurabita sasa iangalie urasimishaji wa uchumi kwa ujumla wake na si rasilimali na biashara tu.” Waziri huyo amewataka wanakamati kuijua vema Mkurabita ili waitumikie vema zaidi, “… Mkijue vema chombe hiki mahususi mlichokabidhiwa. Mkibaki tu ofisini, hamtaijua Mkurabita na hivyo hamtaweza kuiongoza ipasavyo.” Akatoa ushuhuda wake mwenyewe akisema, “Nimetembelea maeneo mengi ambako Mkurabita imefanya kazi na hili, limeniongezea uelewa kwa kiasi kikubwa sana na ninawahikikishia kwamba Mkurabita imefanya na itaendelea kufanya kazi kubwa ambayo ni vizuri mkiiona kwa macho. Hivyo nimuombe Mratibu wa Mkurabita (Mgembe) ahakikishe anaweka mipango sawa ili muweze kutembelea maeneo mbalimbali.” Waziri Wasira akazitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Kamati ya Uongozi na Mkurabita kwa jumla kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha pamoja na Mkurabita kutokuwa na nguvu ya kisheria. Akasema, “Michakato mbalimbali inaendelea ikiwemo kuanzisha chombo chenye nguvu ya kisheria kitakachosimamia agenda na urasimishaji nchini na lipo lile la uanzishwaji wa mfuko endelevu wa urasimishaji utakaoendeshwa kila wilaya.” Waziri Wasira akasisistiza, “Haya yote ni sehemu ya mkakati wa miaka mitano unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Ni imani yangu kuwa utekelezaji wa mkakati huu utapunguza sana changamoto zilizopo ama kuziondoa kabisa. Aidha, utekelezaji wa mpango huu unatarajiwa kugeuza rasilimali mfu zenye dhamani ya Dola za Marekali bilioni 29.3 kuwa mtaji hai. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya tathimini iliyofanywa na Taasisi ya Demokrasia na Maendeleo (ILD), ya Peru mwaka 2004 -2005. Kutokana na manufaa yaliyoonekana ya urasimishaji, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mwalimu Naomi Nnko anasema, “Kwa kujua faida za urasimishaji tangu nikiwa wilayani Mpanda, nilihakikisha Mpango huu unafika katika Halmashauri ya Magu na hadi sasa, tayari vijiji viwili vya Shinembo na Kitongosima vimekwishafanya urasimishaji wa ardhi na mashamba.” Nnko anaishukuru Mkurabita kwa kuiwezesha Magu kwa shilingi milioni 44 zilizowezesha upimaji ardhi baada ya mafunzo katika mwaka wa fedha wa 2014/ 15.
1 comment:
Huyu mama inabidi avae kile chuma cha kunyosha meno. Otherwise, I like her smile!!!
Post a Comment