ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 9, 2014

Siku za Bunge la Katiba sasa zinahesabika

Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba huenda likaahirishwa kati ya sasa na Oktoba 4, mwaka huu bila kufikia kwenye hatua ya kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.
Kuahirishwa kwa Bunge hilo kunalenga kupisha mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2015 wa rais, wabunge na madiwani.
Habari kutoka ndani ya kikao baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), zinasema wajumbe waliafikiana kuitishwa Bunge la Muungano ili kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria zinazosimamia uchaguzi.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alipoulizwa na wanahabari nje ya Ikulu ndogo, Dodoma jana, alisema mazungumzo yalikwenda vizuri na kwamba mambo waliyamaliza kindugu.
Hata hivyo, Cheyo alikataa kueleza nini kilichojiri katika mkutano huo na kusema leo atakutana na wanahabari kuelezea walichokubaliana katika kikao hicho kilichodumu kwa takriban saa tatu.
“Tumefikia makubaliano, hatuna tofauti. Hoja ambazo tulikuwa tumekwenda nazo tumekubaliana… Waambieni wananchi kikao kimekaa, kimekwenda vizuri na viongozi wa vyama wameondoka na msimamo mmoja,” alisema Cheyo.
Alipoulizwa kuhusu kuahirishwa kwa Bunge la Katiba, Cheyo alisema: “Kwa nini mnanitengenezea maneno nitakayozungumza na wanahabari kesho (leo)?, Hebu niacheni tukutane kesho. Unajua nazungumza juu ya watu wengi, si ndiyo? Ni draft (niandike) vizuri niwapelekee na wenzangu wakubali, ndipo nitakuja kuwasomea hiyo taarifa ambayo mimi sitaki kutoa mambo mengine ambayo watakuja kusema umetoa mambo ambayo hayaridhishi.”
Alisema hoja katika kikao hicho zilikuwa ni kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwakani na mchakato wa Katiba unaoendelea.
Alipoulizwa kuhusu kurejea bungeni kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Cheyo aling’aka: “Sasa unaona wewe ndiyo ajenda yako, niache niende, asante sana.”
Cheyo alitoa taarifa hiyo akiwa ndani ya gari baada ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kumsimamisha ili awape muhtasari wa kile kilichojiri kwenye kikao hicho ambacho ni mwendelezo ya kile kilichofanyika Agosti 31, mjini hapa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa waligoma kuzungumza chochote wakimrushia mpira Cheyo.
Hata Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipotafutwa alisema wamekubaliana kuwa Cheyo ndiye atakayezungumza na wanahabari kwa niaba yao kama ilivyokuwa pia kwa Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Kusitishwa kwa Bunge
Habari kutoka ndani ya kikao zilisema baada ya majadiliano kati ya Rais na viongozi hao wa TCD, ilikubaliwa kuwa kwa hali ilivyo na mazingira yalivyo, Bunge Maalumu haliwezi kufika mwisho na kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa.
“Makubaliano ni Bunge la Katiba liahirishwe lakini kujua ni kesho au keshokutwa hiyo siwezi kujua, lakini walichokubaliana ni kwamba liahirishwe lisifike mwisho wake,” kilidokeza chanzo chetu.
Alipoulizwa njia gani zitatumika kusitisha Bunge hilo wakati hakuna mwanya wa kisheria, mtoa taarifa huyo alisema utaratibu utakaotumika na uleule uliotumika baada ya kuisha siku 70 za awali.
“Kwani baada ya kwisha kwa siku zile 70 za mwanzo Bunge liliahirishwaje? Ni kwamba baada ya siku hizi 60 za nyongeza kwisha, Rais hataongeza tena siku na automatically (moja kwa moja) Sitta atakuwa hana njia nyingine zaidi ya kuliahirisha,” alisema.
Chanzo hicho kilisema kwa msingi huo, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977 ambayo baadhi ya vipengele vyake vitafanyiwa marekebisho mapema.
“Imekubaliwa Bunge la Jamhuri liitishwe ili kuifanyia marekebisho Katiba ili kuruhusu kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na sheria nyingine za uchaguzi nazo zirekebishwe,” kilidokeza chanzo hicho.
Hata hivyo, chanzo kingine ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 8.00 mchana hadi saa 10.40 alasiri, kilipasha kuwa kimsingi wamekubaliana kuwa kipaumbele cha sasa ni Uchaguzi Mkuu wa 2015, hivyo Bunge Maalumu litaahirishwa Oktoba 4, mwaka huu.
“Tumekubaliana Bunge la Katiba liendelee na vikao vyake hadi Oktoba 4 kama ilivyo kwenye ile Government Notice (GN) namba 254 ya Agosti Mosi inavyosema. Baada ya hapo liahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu,” kilidokeza chanzo hicho.
Mwananchi

No comments: