Anna Marcus, wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs) akishangilia bendera za Tanzania.
Mwanasaikolojia, mtafiti na mtetezi wa haki za waliokeketwa, Anne-Marie Wilson(kulia kabisa) akijadiliana na wanachama wengine wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs), ukumbi wa Central Hall, Westminster baada ya hotuba yake. Alisisitiza kila sekunde kumi , msichana fulani hukeketwa ulimwenguni. Kati kati ni mweka hazina wa BTs, Bw. Robert Gibson na Jonathan Cape, mwendeshaji wa hafla.
Janet Chapman & Jonathan Cape Waingereza wanaojali maendeleo ya Watanzania. Wameendesha maonyesho matatu mwaka huu mjini London, kusaidia mchango wa fedha za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana wanaokimbia ukeketaji , Mugumu, Mara.
Mheshimiwa Jeremy Lefroy, Mbunge wa jimbo la Stafford, Uingereza. Atasimamia jopo la Jumatano ijayo. Picha toka tovuti yake
Bi Rhobi Samwelly (katikati) akiwa na mkewe Balozi wetu Uingereza, Mama Joyce Kallaghe(kushoto) na Bi. Mariam Kilumanga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania, Uingereza (TAMWA). Hafla ya kukusanya fedha kusaidia ujenzi wa kituo cha wasichana wanaokimbia ukeketaji Mugumu, Mara.
Rhobi akiwa na Fahma (kushoto) mzungumzaji mwingine toka Afrika aliyekemea Ukeketaji.
Bango linalotumika kuchangia makutano na hafla mbalimbali za fedha za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana Mugumu, Mara
Wasikilizaji wa kilichokuwa kikiongelewa. Pichani ni Tony Janes aliyefanya kazi Tanzania miaka ya zamani. Siku hizi kastaafu.
Na Freddy Macha
Jumatano
ijayo tarehe 15 Oktoba, 2014...kundi la kina mama watatu akiwemo Mtanzania litashiriki
jopo la ukeketaji na Wabunge, London, Uingereza.
Mtanzania,
Rhobi Samwelly, mama wa watoto wanne, ni mzawa wa Butiama, Mara. Wenzake ni
Comfort Momoh, toka Nigeria, anayetibu wanawake waliokeketwa hospitali mbili za
Guy’s na St Thomas, London na Ann-Marie Wilson mkurugenzi wa “28 Too Many.” Shirika hili lenye tovuti yenye
http://28toomany.org/ ni maktaba kubwa yenye habari, picha, utafiti na
uchunguzi wa ukeketaji duniani.
Mwaka1997
Comfort Momoh alianzisha msururu wa shughuli za kuwasaidia akina mama
waliokeketwa likiwemo shirika la African Well Women’s Clinic. Bi Momoh mwenye
shahada ya uzamili (MA) ni mshauri wa shirika la Afya duniani (WHO) kuhusu adha
ya ukeketaji.
Mtanzania
Rhobi na Ann-Marie walikuwa baadhi ya
wazungumzaji kwenye hafla iliyofanywa Alhamisi na Jumamosi iliyopita kuchanga
fedha za kujenga nyumba ya hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji, Mugumu,
Mara.
Hafla
hiyo iliendeshwa na shirika la urafiki baina ya Tanzania na Uingereza (British
Tanzania Society) na Shirika la Misaada ya Kimaendeleo Tanzania (Tanzania
Development Trust Fund). Fedha zilizokusanywa zinaendelea kusaidia ujenzi wa
nyumba ya kuwahifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji jimbo la Mara.
Nilimuuliza
Dada Rhobi je hawa wasichana hawatadhurika? Je, wazazi husika hawatawafuata? Akajibu
kwa sasa kuna vyombo vingi husika kikiwepo polisi, serikali na kanisa la
Anglican ambalo yeye ni mjumbe pia.
Rhobi ni
mratibu wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya akina mama vijiji vya Mara.
Mbali na ukeketaji anaangalia pia maslahi ya unyanyasaji wa kijinsia. Baada ya
Bi Neema Wambura kupigwa na mumewe majuma kadhaa yaliyopita, Bi Rhobi alikuwa
mmoja wa waliomhudumia kwa kuhakikisha anapata matibabu. Neema alimwagiwa maji
moto na kuunguzwa kifuani na mkononi.
Kufuatana
na maelezo ya dada Rhobi na Ann-Marie leo hii wastani wa wasichana wanaokeketwa
ni miaka minane hadi kumi na nne. Ila wapo wazazi wanaowapeleka watoto wenye
miaka miwili.
Nchi 29
duniani ikiwemo Tanzania bado zinakeketa wasichana. Licha ya kufanywa vilema, kujifungua
kwa shida, kupata maumivu ya daima
wakati wa haja ndogo na hedhi, baadhi ya wasichana hufa.
Dada
Rhobi Samwelly: “Msichana anapokufa mwili hutupwa tu vichakani na kuliwa na
wanyama. Huwa siri. Wanaficha. Mama aliyefiwa huwambiwa asilie, asiwaambie
watu. Ni aibu. Asiomboleze. Asilie. Ni mkosi. Balaa.”
Kawaida
kipindi cha ukeketaji ni miezi ya Novemba na Desemba, kila miaka miwili.
Wasichana wanaokimbia adha hii wamekuwa wakilindwa na kanisa na sehemu nyingine.
Yumkini nyumba inayojengwa Mugumu itakuwa mkombozi wao. Gharama zake
zimekadiriwa kuwa takribani paundi 60, 000 za Uingereza. Paundi moja na
shilingi elfu mbili na kitu.
Ukeketaji
ambao unajulikana dunia nzima kwa jina FGM (female genital mutilation) huwa wa
aina nne. Aina iliyoenea ni kuondoa kinembe,
kuondoa midomo ya uke, tatu kuondoa kinembe na midomo. Aina hizi tatu za
kukeketa zina lengo za kupungusa kabisa hisia za ngono na mapenzi ya mwanamke.
Desturi iliwekwa ili wanawake wasitembee ovyo nje ya ndoa, wawe tu wazazi na mali
za waume zao. Ya nne ni kuondoa kila kitu na kubakisha tundu la haja ndogo na
mfereji wa damu siku za hedhi.
Mwanamke
anapojifungua hupasuliwa akishamaliza hushonwa tena. Utaratibu huo huendelea
maisha yake yote ya uzazi. Wanawake husika hutembea na maumivu usiku na mchana
maisha yao yote. Ngono, mapenzi, uzazi vyote si furaha kwao.
Si kweli
ukeketaji ni suala la dini. Ulikuwepo kabla ya dini tunazofuata toka Mashariki
ya Kati zilipoingia.
Moja ya
kazi za muuguzi Comfort Momoh ni kusaidia wanawake hawa. Licha ya nchi 29 za
Kiafrika, Mashariki ya Kati na bara Asia, nchi za Kizungu za Ulaya, Marekani,
Canada na Australia pia zinao wahamiaji wanaoendesha shughuli hizi. Kisheria
ukeketaji unakatazwa lakini utekelezaji haujawa makini.
Mwezi
Juni, Kamishna wa Haki za Binadamu, Umoja wa Mataifa Navi Pillay alisisitiza
ukeketaji hauna faida zozote za kiafya. Ukeketaji alifafanua Bi Pillay,
“unaathiri maisha na kuhatarisha maisha ya watoto waliozaliwa na kina mama
walioupitia.”
Bi Pillay
alisisitiza kwamba vita au mapambano dhidi ya ukeketaji ni kazi yetu sote
wanaume, wanawake, watoto, vijana kwa wazee.Bila kuchagua umri, jinsia au
rangi.
Jopo la
Jumatano, Bungeni Uingereza, litakuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo la
Stafford, Jeremy Lefroy, ambaye anawakilisha chama cha Conservatives. Bwana
Lefroy pia huendesha shirika la ufadhili wa maendeleo Equity Africa lenye
dhamira ya kupunguza umaskini barani.
Wazungumzaji
wengine ni Lynne Featherstone, Mbunge
anayewakilisha serikali kwa ajili ya shirika la Kimaendeleo ya Kimataifa
Uingereza (DFID).Mwaka jana DFID ilijitolea kiasi cha paundi 35 milioni
kupunguza ukeketaji duniani kwa asilimia 30.
-London, 10 Oktoba 2014.








Hawa kwenye picha nafikiri na wao walikeketwa.
ReplyDeleteHii agenda yetu ama ya Wazungu? Hivi kweli hili hatuwezi tukalikemea wenyewe mpaka wazungu watupatie fedha? Shule sawa lakini kuihusisha na fedheha ya ukeketaji hapa nami nipelekwe shule. Wakati mwingine tunejifedhehesha wenyewe kwa kutafuta fedha kwa njia yeyote ile.
ReplyDeletemaana ya kukiketwa ni nini?naomba nifahamisheni please.
ReplyDelete