ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 22, 2014

MILIONI 16/- ZATOLEWA NA CIP TRUST UJENZI WA MADARASA

IMG-20141017-WA0009
Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi, (mwenye mgorore wa bluu) akishiriki kutoa burudani na kikundi cha uhamasishaji cha kijiji cha Kinyamwenda kwenye sherehe ya kukabidhi vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu wa shule ya kijiji hicho.

Na Nathaniel Limu, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Community Initiatives Promotion Trust Fund (CIP Trust), limetumia zaidi ya shilingi 16 milioni, kugharamia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu, katika shule ya msingi Kinyamwenda kata ya Itaja.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa shirika la CIP Trust,Affesso Ogenga,wakati akitoa taarifa ya ujenzi huo kwenye hafla ya kukabidhi vyumba hivyo na ofisi ya walimu ambayo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi.
Alisema fedha hizo zimetolewa na serikali ya Austria kupitia asasi ya Sister Cities Singida Salzurg (SCSS).
Ogenga alisema asasi yao iliombwa na uongozi wa shule ya msingi Kinyamwenda kusaaidia kukamilisha mradi huo ambao tayari wananchi waliisha changia nguvu kazi.
IMG-20141017-WA0012
Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi,akiwa amevikwa nguo na kukabidhiwa zana za ushujaa na wananchi wa kijiji cha Kinyamwenda,kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mchapa kazi wa kupigiwa mfano katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“Tunatarajia kwamba baada ya uzinduzi wa majengo haya, tatizo la msongamano wa wanafunzi darasani,litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.Pia walimu watakuwa na ofisi nzuri kwa ajili ya kazi zao za kila siku”,alifafanua Ogenga.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika makabidhiano hayo,mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi,aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Kinyamwenda chini ya mwenyekiti wao na madiwani wa kata ya Itaja kwa kuupokea mradi huo na kuchangia nguvu kazi.
“Nitumie fursa hii kuipongeza asasi ya CIP Trust kwa msaada wao wa kuijengea shule ya msingi Kinyamwenda vyumba viwili vya madarsa na ofisi ya walimu.Hongereni sana kwa kuiunga mkono serikali katika juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu”,alisema Mlozi.
IMG-20141017-WA0014
Aidha,DC huyo aliangiza uongozi wa serikali ya kijiji kumaliza uhaba wa madawati 25 kabla ya januari mwakani.
Dc Mlozi aliendesha harambee kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara ya sekondari ya kata ya Itaja na kufanikiwa kukusanya shilingi 450,000.Fedha hizo zilitumika kununulia mifuko 25 ya saruji.
IMG-20141017-WA0015
Vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Kinyamwenda wilaya ya Singida.Vyumba hivyo na ofisi moja ya walimu,ujenzi wake umegharamiwa na shirika la Community Initiatives Promotion Trust Fund kwa gharama ya shilingi 16 milioni.(Picha na Nathaniel Limu).

No comments: