Enjo, kama alivyojitambulisha kwangu hivi karibuni, anasimulia kisa cha kusisimua.
“Nilikutana naye kwenye daladala, baada ya kunisalimia tukapiga stori hadi alipokaribia kushuka katika kituo chake, akaniomba namba ya simu. Kwa kuwa tulikuwa tumeshazoeana kidogo sikuona taabu, nikampa.
“Aliposhuka tukaendelea kuwasiliana kwa kutumiana sms, kwanza ilikuwa ni maneno ya kawaida tu, lakini baadaye akabadili na kuanza kunitongoza. Sikukataa wala kukubali, kwa sababu mtu mwenyewe nilikuwa simjui.
“Kwa muda kama wa siku mbili hivi tuliendelea kuwasiliana na hatimaye nikaona acha tu nimkubali. Basi alifurahi sana. Akataka siku tuonane nikamwambia sawa, tukapanga siku. Kama mara mbili hivi nilimuomba vocha na alishanirushia ya shilingi elfu tanotano.
“Siku ya ahadi nikamwambia anitumie nauli, akatuma shilingi elfu kumi, nikaenda sehemu tukakutana. Tukapiga stori sana, tukanywa, tukala, lakini akanishangaza eti siku hiyohiyo anataka tukafanye mapenzi. Yaani mtu tumekutana tu leo, hapana, nikamwambia siku nyingine, basi akalalamika sana na tulipoachana, hakunitafuta tena.”
Simulizi yake iliishia hapo, akaingia Innocent, kijana wa kisasa:
“Nilimuona facebook, nikamuomba urafiki akakubali, tukawa tunachat, kwanza ilikuwa kawaida lakini baadaye nikamchomekea, akakubali. Basi tukapeana namba za simu na mawasiliano yakaendelea.
“Siku ya pili tu akaniomba vocha, nikamwambia aache haraka, mambo mazuri hayataki haraka. Akasema eti alihitaji kuwasiliana na mama yake aliye mkoani, nikamwambia atafute maarifa mengine, mimi nafikiria namna ya kumfanyia mambo makubwa zaidi, hayo madogomadogo kama vocha yatatue mwenyewe.
“Akaniambia eti kama nashindwa vitu vidogo kama vocha, hivyo vikubwa nitaviweza wapi, nikamwambia subiri utaona. Basi spidi ya mawasiliano ikapungua, nikimpigia na kumwuliza kwa nini hatumi sms kama zamani, akaniambia simu yake haina salio.
“Basi na mimi nikanyamaza, baada ya siku mbili tatu nikampigia na kumwomba tuonane, akasema kama nitamtumia nauli atakuja, nikamwambia dada mbona unakompleini vitu vidogovidogo, kama vipi kopa kwa mtu uje nitakurudishia, akakataa, nikamwambia kama hana nauli basi apotezee. Nikaachana naye.”
Hizi ni simulizi mbili zenye ujumbe tofauti, lakini zinazowahusu vijana katika mahitaji yao ya kimapenzi. Wasichana wote wawili wanaonekana kufanana mahitaji, tofauti na wavulana.
Mvulana wa kwanza alijitahidi kutimiza mahitaji ya mwenza wake akiamini siku ikifika naye atapewa anachostahili. Lakini yule wa pili hakuweza kutoa mahitaji ya mwenza wake kwa wakati.
Maisha ya kisasa yameifanya dunia ya kimapenzi kubadilika sana. Wapo baadhi ya wasichana wanaoamini mwanaume anayewapenda, lazima ataonyesha kuwajali kwa kuwapa fedha na mahitaji yao mengine hata kabla hawajakutana kimapenzi.
“Mwanaume gani anashindwa kukutumia hata vocha, mtu anashindwa kukutimizia mahitaji yako sasa hivi ndiyo ataweza baadaye?” Hili ni swali unaloweza kukutana nalo kutoka kwa wasichana wengi, wanapozungumza kuhusu mwanaume wanayemhitaji.
Lakini pia baadhi ya wanaume wamekuwa wagumu kutimiza mara moja mahitaji ya wasichana. “Yaani hata hajanielewa vizuri, ashaanza kuleta matatizo yake, kwani kabla hajakutana na mimi vocha alikuwa anapata wapi. Nimtumie nauli? Kwani si anakuja kwa mpenzi wake anashindwa kujilipia elfu moja?”
Haya pia ni maswali unayoweza kukutana nayo kutoka kwa baadhi ya wavulana wanapozungumza juu ya tabia ya wasichana wanaotanguliza mizinga.
Kuna jambo tunalopaswa kuliangalia vizuri na ikibidi kujifunza, kitu gani kinatakiwa kutangulia wakati wa uhusiano katika hatua zake za mwanzo?
Mifano hiyo miwili hapo juu inaweza kuwa mwongozo mzuri kukupeleka kwenye aina ya uhusiano uupendao. Lakini kwa wasichana, ni vyema sana kuepuka kutanguliza mahitaji yako yanayohusu fedha, kwani wakati mwingine wanaweza kujikosesha bahati ya kumpata mtu mwenye malengo ya maisha kwa vile atamuona ni mtu mwenye kujali pesa badala ya upendo.
GPL
1 comment:
mwanamme pesa,sifa ya mwanamme ni pesa hakuna zaidi ya hicho; sura yake tutastahamiliana.no money no love.
na usithani ukitoa pesa utapata game au mtonyo mtonyo siku hiyo,no way its takes time;vumilia kuna siku utapata tu but not the same day.
habari ndo hiyo usiwe bahili utakosa mengi ya raha na furaha.
Post a Comment