ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 16, 2014

Yanga yabadili refa mechi vs Simba

Kamati ya Waamuzi nchini imemuondoa refa msaidizi namba moja, Ferdinand Chacha kuchezesha mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, na nafasi yake sasa inachukuliwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha ambaye atasaidiana na John Kanyenye kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambao mwamuzi wa kati atakuwa Israel Nkongo.

Hata hivyo, mabadiliko hayo yaliyofanywa na kamati hiyo yalichelewa kufika katika sekretarieti ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambayo juzi ilimtangaza Chacha na Kanyenye wa Mbeya kuwa watamsaidia Nkongo katika mechi hiyo namba 27 itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini jana kutoka kwa chanzo chetu muhimu ndani ya kamati hiyo, zinaeleza maamuzi ya kumuondoa mwamuzi huyo yametokana na 'shinikizo' kutoka kwa viongozi wa klabu ya Yanga ya jijini ambao wanadaiwa kumkataa Chacha ambaye pia aliwachezesha katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar iliyofanyika mkoani Morogoro.

Taarifa zaidi zinadai kwamba Yanga iliwasilisha maombi ya kumkataa Chacha kwa kamati na hatimaye mwamuzi huyo mwenye beji inayotambuliwa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa) kuondolewa.

Habari zaidi kutoka kwa chanzo chetu ziliendelea kueleza kwamba baada ya Yanga kumkataa, mwamuzi huyo alitakiwa kuandika barua ya kuomba aondolewe kuchezesha mechi hiyo lakini Chacha hakuwa tayari kufanya hivyo.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa juu wa TFF anadaiwa naye kushiriki katika mabadiliko hayo ya kumuengua Chacha kwa kumueleza kwamba asilazimishe kuuchezesha mchezo huo wa watani wa jadi kwa sababu unaweza kuharibu rekodi yake.

Mwenyekiti wa Kamati wa Waamuzi nchini, Salum Chama, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kuwa ni kweli kamati hiyo imefanya mabadiliko lakini hayatokani na shinikizo lolote.

Chama alisema sababu kubwa ni kubaini kuwa Chacha alichezesha mechi kati ya Mtibwa Sugar na Yanga ambayo ilimalizika kwa kikosi cha Mbrazil Marcio Maximo, kuchapwa mabao 2-0.

"Kamati ndiyo yenye maamuzi ya kupanga na kubadilisha mwamuzi, tumepangua kwa sababu tumeona si vyema mwamuzi mmoja kuambatana na timu moja ndani ya muda mfupi, hakuna sababu nyingine kama ulivyoniuliza," alisema Chama kwa kifupi.

Lakini kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura, alisema shirikisho halihusiki na mabadiliko hayo.

Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, hakuwa tayari kuelezea madai hayo.

Rais wa Simba, Evance Aveva, alisema "yote sawa, kama wameamua kumbadilisha sisi kwetu mpira ni dakika 90".
CHANZO: NIPASHE

No comments: