Advertisements

Saturday, November 22, 2014

Dk. Magufuli: Fedha za kukabiliana na mafuriko Dar zinatafutwa

Serikali imesema inatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza utafiti uliofanywa na Wizara ya Ujenzi ili kukabiliana na mafuriko yanayotokea jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema).

Mdee alisema watafiti wa Wizara ya Ujenzi, walishauri kujengwa kwa mifereji ya chini mikubwa kutoka Ubungo hadi Kawe ili kukabiliana na mafuriko.


Alisema zoezi zima la ujenzi wa mifereji hiyo ulipangwa kugharimu Sh. bilioni 5.5.

“Ni lini serikali yako itatekeleza utafiti uliotolewa na chombo chako ili wananchi wa jiji la Dar es Salaam wasiathirike tena na mafuriko kama wataalam walivyosema yanaweza kutokea?”alihoji.

Akijibu swali hilo, Dk. Magufuli alisema mafuriko hayatokei Dar es Salaam tu bali hata Marekani yanatokea.

“Wizara imejipanga ndiyo maana kila inapotokea matukio tunafanya mipango mbalimbali. Sasa tunachukua hatua mbalimbali ikiwamo pale May-Fair katika barabara ya Moi Kibaki tunaipanua,”alisema.

Dk. Magufuli alisema katika upanuzi wa barabara ya Mwenge kwenda Tegeta wamejenga madaraja makubwa ili kukabiliana na mafuriko.

“Tuko kwenye hatua mbalimbali kupata fedha za kutosha ili kuweza kushughulikia utafiti uliofanyika,”alisema.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Betty Machangu (CCM), alitaka kujua ni kwanini serikali isitoe waraka wa halmashauri za wilaya kutaka ushauri wa mameneja wa Mkoa wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), wanapotaka kutengeneza barabara za halmashauri.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, alisema ujenzi na matengenezo ya barabara za halmashauri hufanyika chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), na mameneja wa TANROAD mkoa wanasimamia barabara kuu za mkoa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: