ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 21, 2014

IPTL yambabua Pinda

  Pinda asema ikithibitika hata yeye haachwi
  Wabunge waja juu, waipinga mahakama
  Wahoji mabilioni kulipa vikao vya harusi
  Wakumbuka Richmond, Operesheni Tokomeza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kubanwa na wabunge ambao waliweka pembeni tofauti za vyama vyao vya siasa na kuungana kupinga vikali njama zinazodaiwa kufanywa na Mahakama ya Tanzania za kuingilia uhuru wa Bunge kwa kulizuia kujadili ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL ya uchotwaji wa Sh. bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hoja za wabunge hao zilionekana kulitikisa Bunge jana, kiasi cha wabunge kutotaka kusikiliza kauli ya serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwani alipotoa ufafanuzi walisikika wakitoa matamshi yaliyoashiria kutokukubaliana naye.

Kutokana na hali hiyo, wabunge hao wametaka uhuru wa Bunge uheshimiwe na ripoti hiyo iwasilishwe bungeni, wabunge waijadili ili kuondokana na ‘makandokando’ yaliyogubika suala hilo, wahusika wa wizi wa fedha hizo wajulikane na kila mtu abebe msalaba wake.

Ripoti hiyo inatokana na ukaguzi wa hesabu kwenye akaunti hiyo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuhusiana na kashfa hiyo.

Wabunge hao waliyasema hayo kwa hisia kali kwa nyakati tofauti bungeni baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutoa fursa kwa wabunge kukishauri Kiti cha Spika na Kamati ya Uongozi ya Bunge, kutokana na ukubwa na unyeti wa suala hilo.

Ndugai alitoa fursa hiyo kwa wabunge wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Katika mwongozo wake, Kafulila alitaka kiti kieleze kama kuna uhakika wa ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni, kutokana na kuwapo kwa taarifa zinazodai Mahakama ya Tanzania kutaka kutumika kama kichaka kulizuia Bunge kujadili suala hilo.

Wakati hayo yakijiri, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, aliliambia Bunge jana kuwa kamati yake imekwisha kuchambua ripoti hizo, ikiwa ni pamoja na kumhoji CAG, Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivyo iko tayari kuwasilisha bungeni kama watakavyoelekezwa na wabunge.

Wabunge waliotumia fursa hiyo iliyotolewa na Ndugai na kuzungumza kwa hisia kali dhidi ya njama hizo bungeni jana, ni Kafulila, Ester Bulaya (Viti Maalumu-CCM) na Michael Lekule Laizer (Longido-CCM),Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), James Lembeli (Kahama-CCM) James Mbatia (Kuteuliwa-NCCR-Mageuzi) na Kaimu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema).

KAFULILA
Kafulila alisema Bunge ndicho chombo cha mwisho katika maamuzi kuhusu nchi na kwamba kashfa ya akaunti hiyo ni jambo zito na nyeti na njama zinazodaiwa kufanywa na Mahakama ya Tanzania kujaribu kuwazuia wabunge kujadili ni mtihani kwa Bunge.

Alisema hashangazwi kusikia njama hizo kufanywa na Mahakama ya Tanzania, kwani tangu hapo zipo taarifa zinazodai kuna baadhi ya majaji waliopata mgawo wa fedha zilizochotwa kifisadi kutoka kwenye akaunti hiyo na hivyo kupoteza imani na uadilifu kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alisema suala hilo bado linahitaji maamuzi ya Bunge, hasa ikizingatiwa kuwa ukaguzi wa hesabu katika akaunti hiyo uliofanywa na CAG kwa niaba ya Bunge.

Alihoji sababu za Mahakama ya Tanzania kwa kipindi chote kukaa kimya na kuliacha Bunge hadi likamuagiza CAG kufanya kazi hiyo wakati ikijua kuwa suala hilo liko mahakamani.

“Tusiruhusu nchi kuingia kwenye machafuko...hoja ya Mahakama knakoaa uhalali...Tuonyeshe kwamba tunatosha kuisimamia serikali, mamlaka ya Bunge yaheshimiwe,” alisema Kafulila.

BULAYA
Bulaya alisema ni lazima Bunge liheshimiwe kwa sababu nalo pia mhimili wa dola na kwamba, siku zote limekuwa ni sikivu sana kwa kisingizio halina mamlaka ya kuingilia mhimili mwingine, huku kukiwapo na mhimili unaoonekana una nguvu kuliko mwingine kwa makusudi.

Alisema amekuwa akizungumzia mara kwa mara tabia ya Mahakama ya Tanzania kutumika vibaya na anaamini haina mamlaka ya kulizuia Bunge kujadili taarifa ya CAG kwani kinachotaka kujadiliwa na wabunge siyo namba ya kesi yoyote, bali ripoti ya CAG kwa mujibu wa kanuni.

“Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti hii imekabidhiwa kwa Bunge siyo kwa serikali. Ripoti hii ni ya Bunge. Bunge lina mamlaka ya kujadili na kufanya maamuzi,” alisema Bulaya.

Alisema wabunge wanapoambiwa kuna kesi mahakamani, fedha za Tegeta Escrow zilitoka Oktoba 5, mwaka huu, wakati kulikuwa na kesi za mwaka 2006 na 2012 za kimataifa, lakini bado mahakama ikaamuru kesi hizo zitoe mkanganyiko.

Bulaya alisema pia kulikuwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK) na wakati huo huo kesi mahakamani, lakini bado mahakama hiyo hiyo ikaruhusu BMK.

“Mheshimiwa naibu spika, hatuwezi kukubali mahakama moja ikawa inatoa maamuzi tofauti kwa sababu, ambazo wanazitaka wao,” alisema Bulaya na kuongeza kuwa:
“Tumeambiwa kuna baadhi ya majaji wamehusika, wamepewa milioni mia nne kwa ajili ya msiba na harusi. Sasa Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kukubali mambo kama hayo.

Mheshimiwa waziri mkuu ameongea vizuri. Bunge kama hili halipo kwa ajili ya kumuonea mtu. Tuko kwa ajili ya kuondoa hii mikanganyiko hii, ambayo fununu zinazoongelewa un necessary hatuwezi kukubali fununu hizi zikaendelea, kupakwa matope watu wengi wasiohusika.”

“Kama suala hili Bunge lilikuwa lina taarifa jambo hili lipo mahakamani, mmetoa ratiba, wabunge tumelipwa mpaka tarehe 29.Tunatakiwa tukae tufanye kazi, tumalize kazi yetu. Kwa hiyo,...mimi ninachoshauri kiti kiendelee, kifuate ratiba tuijadili. Hatuwezi kukubali Chama Cha Mapinduzi kipakwe matope kwa sababu ya watu wachache katibu wetu mkuu anafanya kazi kwa ajili ya kujenga chama.”

“Hili halikubaliki, hili halikubaliki mheshimiwa naibu spika halikubaliki, hatutakubali, hatutakubali. Kila mtu atakula kulingan na urefu wa kamba yake, kila mtu ahukumiwe kwa kile alichokifanya, asiyefanya hatahukumiwa. Na mimi nitachangia kama kuna mtu hajahusika katika hili, hatahukumiwa. Bunge lako sasa litumie mamlaka yake mambo ya mahakama kutumika kwenye dawa za kulevya, kutumika kwenye ujangili, kutumika kwenye Escrow marufuku.”

LAIZER
Alisema licha ya yeye kutolielewa vizuri suala hilo, anaona limekuwa kubwa na linaumiza vichwa vya watu wengi.

“Hapa tumegawanyika kwa sababu kuna watu wanaoelewa jambo hili vizuri na tupo wengi, ambao hatuelewi jambo hili na tunasikia tu minong’ono minong’ono na orodha ya wezi leo hawa, kesho hawa, hawajulikani ni kina nani. Lakini niseme tu. Kama kuna wezi humu ndani walioiba fedha za wananchi, kama wapo nje ya Bunge hili, wote naomba tusifiche ugonjwa,” alisema Laizer.

MSIGWA
Alisema anachokiona ni kuwa muda uliopo kwa sasa ni wa ukweli na maamuzi dhidi ya njama zozote za kutaka kulihamisha taifa kutoka mahali, ambako Watanzania wamepazoea kwenda kwingine.

“Kama Bunge tuna uzoefu, mara nyingi serikali inakuja hapa inafunika kombe mwanaharamu apite. Juzi hapa nilisema sasa hivi mwanaharamu hapiti tunachotaka,” alisema Msigwa.

Alisema Kafulila alipopeleka hoja hiyo bungeni, walitaka kuamulia ugomvi kati ya Kafulila na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, baada ya mmoja wao kuitwa tumbili na mwingine mwizi.

Aliongeza: “Tusimung’unye maneno. Wananchi wametuamini sisi kama Watanzania. Kama kuna mtu ameiba, abebe msalaba wake. Na kama kuna mtu hajaiba, abebe msalaba wake. Mpaka sasa kila kitu hakieleweki. Sisi ndiyo nyumbani hapa. Tujadili kama wabunge. Vyombo vya habari vimewataja majaji.

Taifa linapofika mahali chombo kikubwa kama mahakama inakosa imani kwa wananchi kwamba, kuna majaji wamepokea hii pesa, idhihirike hapa,” alisema Msigwa.
“Taifa linapita mahali tunaambiwa na maaskofu nao wamepokea hii pesa, idhihirike hapa, wasidanganye kondoo za Mungu huko barabarani. Kuna mawaziri wanaonekana wamepokea pesa tunawaona kwenye mitandao

watu wanasema I receive in good faith, tunataka ijulikane if they can bring back our money in good faith lazima haya mambo yajulikane hapa haya mambo yapo wazi asionewe mtu yoyote tunataka tuyaweke hadharani na nimesema bahati mbaya Bunge letu limekuwa likipuuzwa...na nikushukuru kwa hekima yako, ambayo umeionyesha mi nikupongeze sana kwa sababu hili ni Bunge la sisi sote.
Na sisi tumeona tunaweza kujadili hekima uliyoitumia leo ni ya busara sana, usikie mawazo yetu na naona mwelekeo, naona wabunge wote tunataka hii kitu ije hapa. Mara nyingi serikali imekuwa inajitahidi kuficha.”

LEMBELI
Lembeli alishauri kila Mtanzania, wezi na viongozi wote wenye lugha za kukashifu wenzao wabebe misalaba yao, kwani nchi imefika njiapanda kuamua kuingia kwenye amani au vurugu.

Alisema hivi sasa nchini, taasisi pekee zinazoaminika ni Bunge na mJeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Lembeli alisema Tanzania siyo kisiwa na kuna uwezekano mkubwa wa Bunge kuingia kwenye rekodi mbaya iwapo njama hizo za Mahakama ya Tanzania zitapewa nafasi na kuhoji iweje kwenye kashfa ya Operesheni Tokomeza iliyowawajibisha mawaziri watano wabunge walikubaliana , lakini la Escrow washikwe na kigugumizi.

Alisema fedha za Escrow zimeliwa na baadhi ya watu ndani ya Bunge, hivyo kushauri jambo hilo liwekwe wazi na kumweleza Ndugai kuwa kama atalisimamia vizuri historia itamkumbuka.

MBATIA
Mbatia alisema nchi ilipofika, inayumba kutokana na udhaifu wa serikali, ambayo imekuwa haichukui maamuzi kwa wakati na kushauri kuwa Bunge lisikubali kuruhusu kuyumba, kwani litahukumiwa na historia.

“Tutumie hekima na busara, jambo hili lijadiliwe kisha tutulie. Kwa sababu akili yote ya Watanzania ni Escrow. Tusiruhusu watu wachache waharibu taifa. Wahisani wamekataa kutoa misaada kwa sababu ya jambo hili. Tuache miswada mingine yote tujadili hili,” alisema Mbatia.

LISSU
Lissu alisema hakuna utaratibu wa kikanuni, unaoruhusu mahakama kumuandikia Spika wa Bunge kumuelekeza, pia katiba haijaruhusu kumfundisha kazi ya uspika, pia sheria yoyote inayoiruhusu mahakama kulielekeza Bunge kujadili jambo lolote.

“Kama kuna barua ya kuingilia uhuru wa Bunge, naomba ukatae, pili, barua hiyo iwekwe mezani Bunge limjadili huyo jaji au kiongozi wa mahakama aliyeingilia uhuru na kulifundisha Bunge. Kama haipo tuendelee na shughuli zetu. Bunge la tisa litakumbukwa kwa Richmond.

Ni wewe peke yako (naibu spika) utaubeba msalaba na siyo kusaidiwa na Simon Mkirene. Hatuwezi kuwa toilet paper ya kusafisha uchafu wa watu. Ripoti ya Escrow iletwe hapa ijadiliwe, wa kusuka na wa kunyoa ajulikane,” alisema Lissu.

PINDA
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hata yeye anapenda suala hilo lijadiliwe na kuisha, lakini akashauri busara itumike kuhakikisha kila mhimili wa dola unatekeleza jukumu kwa mujibu wa Katiba.

NDUGAI
Ndugai aliungana na Pinda akisisitiza mahitaji ya busara kutumika katika kujadili suala hilo na kwamba, wakiwa viongozi hawawezi kutengeneza umoja katika maovu. "...na mimi nimelishika sana neno hili, yaani haiwezekani yaani tu eti Bunge tukala njama katika maovu, haiwezekani, haiwezekani hata kidogo.

Baadhi yetu inawezekana, lakini hatuwezi kwa sisi viongozi tuliopewa dhamana tukafanya hilo. Kwa hiyo, linatuweka kwenye mtihani mkubwa. Tumesikia uongozi, kamati ya
uongozi, tumesikia moddy ya Bunge, tunaiona ilivyo. Niwahakikishieni tutatenda haki katika jambo hili. Kwa hiyo, tumepokea ushauri," alisema Ndugai.

MACHALI, Pinda
Awali, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, katika maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu, alitaka kauli yake baada ya taarifa ya CAG na Takukuru kwamba, fedha za Escrow kama ni za serikali baada ya Pinda siku za nyuma kutamka kwamba, siyo za serikali.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema msingi wa kauli yake huko nyuma ulitokana na uelewa wake kwamba, kipindi kile chote Tanzania ilitumia umeme uliokuwa unazalishwa na IPTL na kwamba, katika maelewano ya awali yaliyokuwa yameshakubalika alijua kwamba fedha zinazotolewa ni kwa sababu ya matumizi ya umeme nchini.

Alisema kwa sababu jambo hilo lilikuwa chini ya uchunguzi wa Takukuru na CAG, utabainisha kama upande wa serikali kuna kiasi cha fedha ambacho ilitakiwa ilipwe na kwamba, anaamini utaratibu huo utafuata ili kiasi hicho kirudishwe.

Pinda alisema kwa uelewa wake anajua kwamba, ziko kesi zaidi ya 10 mahakamani hivi sasa zinazohusu malumbano ya wadau katika suala la IPTL wakidaina fedha hizo za akaunti hiyo.

"Sasa kwa mfumo na misingi ya utawala wa sheria katika nchi yetu, unapokuwa na jambo ambalo sasa linaendelea mahakamani, utaratibu wa kikatiba unatutaka sisi upande wa chombo, ambacho ni mhimili mwingine, tusianze na sisi kujadili jambo hilo kwa sababu tutaji-overdise kile kinachoendelea," alisema Pinda kauli ambayo iliwafanya wabunge kutoa matamshi ya kuipinga na yeye kusisitiza kuwa: "Mi nasema kweli, najaribu kueleza. Najaribu kueleza."

Aliongeza: "Lakini haya ni maoni yangu mimi, lakini bado ofisi ya spika, inaweza kupata ushauri mzuri na tukajua wanasema nini. Hii si mara ya kwanza mambo kama haya kuwapo na wote tumekuwa tukiheshimu kilichokuwa kinaendelea mahakamani."

PINDA AKUTANA NA MAWAZIRI
Taarifa tulizozipata wakati tunakwenda mitamboni jana, zinasema kuwa Pinda alikuwa anakutana na mawaziri katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma. Haikujulikana kilikuwa ni kwa ajili ya kujadili ajenda zipi.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hizi tunazofanya ni kelele tu. hakuna adhabu yeyote itakayo tolewa kwa wizi wa fedha zetu kwani bungeni ni kumshitaki panya kwa panya na karibu wote mle ndani ni uzao wa panya buku.

na tutatengenezewa story ili tusahau mara sijui hivi na hivle watazania walivyo mbububu/mburulaaz wataacha kashfa hii watashabikia story iliyotengenezwa na mambo yatapita tu. ni upepo tu huu utapita kwa wanaotafuta nchii hii.

sakala la IPTL mmelisahau mbona limepita tu.
nchi ya kifisadi mnachcagua mafisai ndo mnayapata haya.

ukoo wa panya wanazaa panya bukuu.