Advertisements

Monday, November 24, 2014

Lissu ahoji Werema kuwafumbia macho vigogo wanaotajwa Escrow

Baada ya kumshambulia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wapinzani sasa wamemshukia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na kumbana, wakidai ameshindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya vigogo wa serikali waliotajwa kuhusika katika kashfa ya kampuni ha IPTL ya uchotwaji wa Sh. bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Vigogo hao ni pamoja na mawaziri wa sasa na wa zamani, mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani, majaji wa mahakama kuu na Gavana wa BoT.

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema hayo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, uliowasilishwa na Jaji Werema, bungeni juzi.

Lissu alisema hayo akipinga kauli ya Jaji Werema ya kuunga mkono na kutetea muswada wa sheria inayomruhusu AG kuingilia suala lolote au kesi yoyote mahakamani kwamba, hufanya hivyo kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Jaji Werema anadaiwa kutoa kauli hiyo katika kikao kati yake na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wa Bunge, mjini hapa juzi.

"Haya ni majigambo ya bure, kwani katika matukio mengi na makubwa, ambayo yameliingiza taifa hili hasara ya mamia ya mabilioni ya fedha na kulichafua taifa letu mbele ya jumuiya ya kimataifa, mwanasheria mkuu amekuwa mhusika muhimu kama siyo mhusika mkuu," alisema Lissu.

Aliongeza: "Kwa mfano, katika kashfa inayoendelea sasa ya akaunti ya Escrow, mwanasheria mkuu huyu huyu ameshindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya mawaziri wa sasa na wa zamani wa serikali hii ya CCM, mwanasheria mkuu wa zamani, majaji wa mahakaka kuu na gavana wa benki kuu ambao wametajwa kuwa miongoni mwa waliovuna mabilioni ya fedha za akaunti hiyo."

Alisema pia mtangulizi wa Jaji wa Werema, Johnson Mwanyika, katika Ofisi ya AG, naye alishindwa kuchukua hatua yoyote kwa mawaziri na watendaji wa ngazi za juu serikalini 'waliovuna' mamia ya mabilioni ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans mwaka 2007/2008.

Lissu alisema kabla ya hapo, Mwanyika alishindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya AG mtangulizi mwenzake, Andrew Chenge, 'aliyekatiwa' mgawo wa 'vijisenti' vya ununuzi wa rada ya Tanzania.

Alisema Chenge alifanya hivyo wakati mwanasheria mkuu mwenzake wa Uingereza kupitia Taasisi ya Kushughulikia Makosa Makubwa (SFO) ya nchi hiyo, akiwashughulikia mafisadi wa Kiingereza waliohusika katika kashfa hiyo iliyoliingizia taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma na kuwapaka Watanzania matope ya ufisadi duniani kote.

Alisema kupitishwa kwa baadhi ya sehemu ya muswada huo kama ilivyokuwa inaombwa na serikali, kungepanua uwanja zaidi kwa AG kuendeleza hujuma dhidi ya maslahi halisi ya nchi kwa kuyaingiza mashirika na taasisi nyingine za umma katika makucha ya sheria ya mashauri ya serikali.

Awali, muswada huo ulikuwa unapendekeza marekebisho ya sheria mbalimbali 33, lakini baada ya majadiliano kati ya kamati hiyo ya Bunge na AG, serikali ilikubali kuondoa baadhi ya sehemu zake (muswada huo).

Lissu alisema sehemu zote za muswada zilizoondolewa zilikuwa na mapendekezo, ambayo yangesababisha matatizo makubwa katika uendeshaji wa mashauri yanayohusu mashirika na taasisi za umma zinazojitegemea na kuathiri haki za wananchi katika maeneo mengi.

Alisema sehemu hizo zimeondolewa kwa sababu ya umakini, weledi na ujasiri mkubwa ulioonyeshwa na wajumbe wa kamati hiyo.

Alisema sheria ya mashauri ya serikali ni ya kibaguzi kwa kuwa inapendelea serikali wazi wazi.

Alisema endapo Bunge lingepitisha mapendekezo ya muswada huo kama ilivyokuwa inaombwa na serikali, ubaguzi huo ungeingizwa katika kesi zote zinazohusu mashirika na taasisi zote za umma.

Pia maneno ya ibara ya 13 (1) ya katiba ya nchi kwamba: " watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria" yangeendelea kuwa ahadi hewa.

Alisema vilevile, nyaraka zinazothibitisha ufisadi serikalini au matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyotokea wakati wa kashfa ya Richmond/Dowans, au akaunti ya Epa, au ufisadi wa sasa katika Tegeta Escrow zisingeweza kutolewa mahakamani endapo kutakuwa na amri ya mahakama wakati wa ugunduzi, ukaguzi au hojaji.

Lissu alisema endapo Bunge lingeridhia maombi ya serikali na kuupitisha muswada huo, kifungu ambacho kimekuwa ndio kimbilio la mafisadi serikalini, sasa kingekuwa ni kichaka cha mafisadi katika mashirika na taasisi za umma.

Sehemu nyingine za muswada huo zilizoondolewa ni pamoja na iliyokuwa ikipendekeza kuweka masharti yanayomwezesha AG kuingilia kati katika hatua yoyote shauri lolote lililopo mahakamani dhidi ya serikali au taasisi yoyote iliyoanzishwa na sheria.

Lissu alisema pendekezo hilo halikustahili kwa kuwa AG amekuwa na mamlaka hayo tangu mwaka 2005 na kwamba, hajawahi kuyatumia katika kesi au mashauri yanayohusu mashirika au taasisi za umma.

Alisema kama mapendekezo ya marekebisho yaliyoko kwenye sehemu zilizoondolewa yangebaki katika muswada huo, kusingekuwa na uwezekano wowote ule wa mtu yeyote yule, au shirika, au taasisi au kampuni yoyote binafsi kupata haki, endapo serikali au taasisi au mashirika yake yote yaliyotajwa kwenye muswada huo yatashtakiwa mahakamani na kushindwa kesi.

Awali, Jaji Werema akiwasilisha muswada huo bungeni, alisema unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria 32 kwa lengo la kuimarisha matumizi na kuongeza masharti mapya katika sheria hizo.

Pia kufanya masahihisho ya kiuandishi na lugha katika tafsiri ya baadhi ya vifungu, kuainisha masharti ya sheria hizo na sheria nyingine ili kuleta utekelezaji madhubuti wa sheria husika.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

Tusiwaachie hao jamani hata kama chama tawala ni chama TWAWALA!! kipindi hiki hatukubali, Mheshimiwa MNYIKA nakuaminia najua una la kusema hebu tupe habari hatutavumilia hili warejeshe hiyo fedha haraka wakijiuzulu na kuchukuliwa hatua. Raisi KIKWETE tunamsubiri kusema neon haraka akirudi ughaibuni NO MAtter what?!!