ANGALIA LIVE NEWS
Monday, November 24, 2014
Mabadiliko ya mara kwa mara ya Mitaala shule za Msingi inawachanganya wanafunzi.
Fikra Pevu
BAADHI ya Walimu wa Shule za Msingi katika jiji la Dar es Salaam wamelalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala kwa shule za msingi pamoja na idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa madarasa yote na kwamba yamekuwa yakiwachanganya wanafunzi na kuwafanya washindwe kumudu masomo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na FikraPevu jijini humo Novemba 17, 2014 walimu hao wamesema mabadiliko ya mara kwa mara kwa mitaala yanayofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bila maandalizi yamekuwa chanzo na kikwazo kikubwa cha kutofanya vizuri kwa sekta nchini.
Walimu Wakuu katika shule hizo wamesema mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara inawachanganya wanafunzi pamoja na walimu kutokana na walimu kutoandaliwa vyema na kushirikishwa katika uanzishwaji wa mitaala hiyo na hivyo kuwa kikwazo kufikisha ujumbe kwa hadhira.
Kwa mujibu wa walimu hao ambao baadhi yao (hawakutaka majina yao yatajwe) wameshauri kuwepo na maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha walimu ambao ndio wanakabiliana na hali ya kufikisha elimu hitajika kwa wanafunzi. Wanataka washirikishwe kwani sekta ya elimu ni muhimu na kwamba kabla ya mabadiliko ya mitaala hiyo haijaanza kutumika itasaidia kuwepo kwa usawa katika masomo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mashujaa ya Sinza ‘B’, Triphonia Kahwili, amesema pamoja na hali hiyo mabadiliko ya vitabu vya masomo bila utaratibu mahususi ni tatizo pia katika mafanikio ya sekta hiyo kitaaluma.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbuyuni, Dorothy Malecela, ameema utofauti uliopo kwa mtaala unaotumika hivi sasa na ilivyokuwa hapo awali, amesema mitaala ya sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo ambalo linawachanganya walimu na hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya vizuri.
“…Hii mitaala haieleweki kwamaana tangu mwaka 2005 ilipoanza kutumika unakuta mwalimu mmoja katika mkoa au wilaya ndiye aliyepewa mafunzo ya mabadiliko ya hii mitaala kwahiyo ni vigumu kumfundisha mwanafunzi masomo kama ya Tehama nawakati mwalimu mwenyewe hata komputa haijui” alieleza Mkuu wa shule moja wapo ya shule zilizopo jijini humo.
Hata hivyo, wamelalamikia baadhi ya masomo kuwa yamekuwa changamoto kwa wanafunzi yakiwemo masomo ya Tehama na Stadi za Kazi kutokana na mwalimu kukosa elimu au mafunzo ya kuelewa teknolojia inayotakiwa kutumika na kufanya shule hizo kushindwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya Kitaifa.
Masomo yanayofundishwa katika shule za msingi hivi sasa ni masomo 10 ambayo ni Hisabati, Kiswahili, Tehama, Historia, Jiografia, Kiingereza, Uraia, (Haiba na Michezo), Sayansi na Stadi za Kazi.
Wanafunzi waeleza
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wanafunzi wa shule hizo akiwemo, Brayan Simon, mwanafunzi wa shule ya Msingi Tandale, amefafanua kuwa mbali na mchanganyiko juu ya suala la vitabu vya masomo mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya masomo kubaki kama ‘kiini macho’ jambo ambalo ni tatizo kwao pamoja na walimu wanaowafundisha.
“Nadhani unakumbuka kuna kipindi baadhi ya masomo yaliunganishwa kama Jiografia, Historia na Uraia wakaita maarifa ya jamii……..kipindi hiki wanafunzi tumeambiwa tunafanya vifanya vibaya sana hivyo ikabadilishwa ili tufanye vizuri tofauti” alieleza mmoja wa wanafunzi jijini humo.
Wasiojua kusoma na kuandika kuendelea na masomo ya juu
Taarifa zinasema wanafunzi waliojiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za Serikali na baadaye kubainika kuwa hawajui kusoma na kuandika kwa ufasaha wanaendelea na masomo yao.
Uchunguzi wa FikraPevu katika baadhi ya shule za sekondari kwa wilaya za Temeke na Kinondoni umebaini wanafunzi hao kuendelea na shule licha ya walimu kuwachuja na kutoa taarifa sehemu husika kama walivyo elekezwa.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Afisa Elimu Sekondari katika halmashauri ya Kinondoni zinaonyesha kuwa kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya kubaini wanafunzi wanaofaulu kujiunga na sekondari (wasio na sifa) jumla ya wanafunzi 13 walibainika kutokuwa na sifa hizo katika kipindi cha mwaka 2013/2014.
Taarifa zinasema wanafunzi hao walishindwa kabisa kufanya vizuri katika mtihani waliopewa jambo ambalo lilionesha ulakini katika kujiunga kwao na masomo ya sekondari, japokuwa wanaendelea na shule hadi sasa.
Uchunguzi uliofanywa katika Wilaya ya Kinondoni pia ulibaini wanafunzi walioshindwa kufaulu katika mchujo uliotolewa na Serikali wameendelea na masomo ya kidato cha kwanza, licha ya shule kadhaa za sekondari kupeleka majina hayo kwa viongozi wa idara husika ambazo zingetakiwa kuchukua hatua stahiki kutokana na mapungufu hayo.
Wakizungumzia hoja hizo, Ofisi ya Afisa Elimu Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Kinondoni, wamesema mabadiliko yanayofanywa na wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na changamoto kadhaa katika maeneo tofauti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment