
1. Omari Mgwabati wa Kijiji cha Makalamo:
Wakati wa kampeni za kuwania ubunge uliwaahidi wananchi kuwa wakikuchagua utafikisha umeme Kijiji cha Mkalamo, umefikia hatua gani?
Jibu: Tayari mkandarasi; Kampuni ya Sengerema Electrical Works amepatikana kwa ajili ya kushughulikia suala hilo na ameshafanya kazi ya kutafiti njia za kupitishia nguzo za umeme.
Kupitia usimamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), mkandarasi huyu amesaini mkataba wa kupitisha umeme Kitongoji cha Mbulizaga kabla ya kufika Mkalamo na chini ya mradi huo, umeme utafikishwa Kitongoji cha Choba na Kijiji cha Kimang’a.
2. Hadija Ramadhani wa Pangani Magharibi.
Uliahidi kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Pangani kwa kuyatoa katika Mto Pangani, umefikia wapi?
Jibu. Mshauri elekezi kutoka Kampuni ya Arab Constraction amefanya utafiti na kutoa majibu kwamba mradi huo utagharimu kiasi cha Sh15 bilioni. Nimeomba Wizara ya Maji wametupatia Sh630 milioni katika bajeti ya mwaka 2013/14, kazi yake kubwa ni kuongeza visima vya maji eneo la Boza, kuweka mitandao ya mabomba mapya na kukarabati ya zamani pamoja na kujenga matanki mapya ya kuhifadhia maji.
3. Mausi Mtoo, mvuvi wa Pangani Magharibi.
Uliahidi kuwasaidia wavuvi vifaa ili waweze kuvua kisasa na uhakika zaidi, ni kwa kiwango gani umetekeleza ahadi hii?
Jibu.Chini ya mradi wa Macemp, tayari wavuvi wa Funguni wamepata boti, lakini wanawake waliounda vikundi tumepanga kutoa fungu kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya kuwanunulia nyavu za kuendeshea uvuvi.
4. Lucas Titus wa Kijiji cha Mivumoni.
Kuna mgogoro wa ardhi unaoendelea baina ya wakazi wa Kijiji cha Mivumoni na mwekezaji, ukiwa mwakilishi wa wananchi umewasaidiaje?
Jibu. Kama itakumbukwa, nimekuwa nikishughulikia mgogoro huu uliodumu kwa kipindi kirefu tangu mwaka 2005, nimeuliza swali bungeni na hata Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara Wilaya ya Pangani Julai 12, mwaka huu nilimuuliza, lakini ahadi ya Rais Kikwete ni kuwa shamba la Mivumoni ndani yake kuna kijiji.
Tayari mgogoro huu umeshughulikiwa na kitengo cha uwekezaji na uwezeshaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na mapendekezo ya Serikali kama alivyoshauri Rais ni kuwa, nusu ya shamba iwe chini ya miliki ya kijiji na nusu nyingine ibaki kwa mwekezaji, kwa hiyo tunasubiri maoni ya mwekezaji.
5. Method Mkali, dereva wa bodaboda Pangani. Bandari ya Pangani haina gati hadi sasa kitu ambacho kinachangia kukosekana kwa mapato, umeshughulikia vipi suala hili?
Jibu. Mwaka 2012 nilipeleka maombi Wizara ya Uchukuzi nao wakapeleka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), nafurahi kuwafahamisha wananchi kwamba Mamlaka imeshampata mkandarasi wa kujenga gati ambayo ni Kampuni ya Alpha Logistics.
6. Haruna Mohamed, mfanyabiashara Pangani mjini.
Uliahidi kumtafuta mwekezaji atakayeweza kupeleka meli Pangani kwa ajili ya kufanya safari kati ya Pangani na Zanzibar, umefikia wapi?
Jibu. Kampuni ya Songolo Marine ilishaileta Pangani boti za safari kati ya Pangani - Pemba - Unguja lakini kutokana na kukosekana kwa gati ililazimika kupelekwa Bandari ya Tanga.
7. Haruna Mohamed, mfanyabiashara Pangani Mjini.
Madiwani wenzako wanakutuhumu kwamba huhudhurii vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, unalisemeaje hili?
Jibu. Sijui swali hili linatokea wapi kwa sababu nahudhuria. Mara nyingine vikao vya madiwani wa jimbo langu hugongana na vikao vya Kamati za Bunge au Bunge lenyewe. Nilishawahi kushauri viwe vikipangwa kwa kuzingatia ratiba ya vikao vya Bunge, kwa sababu ifahamike kuwa nikikosa bungeni pia nakuwa nimewanyima haki wananchi ya kuwawakilisha.
8. Mwajuma Fundi wa Pangani Mashariki. Wanawake wa Pangani wamekuwa wakihangaika kufanya biashara ndogondogo kutokana na kukosa mitaji, umeweza kuwatafutia mashirika ya fedha ya kutoa mikopo isiyo na riba?
Jibu. Wilayani Pangani yapo mashirika ya mikopo kama Finca, lakini kupitia mfuko wa jimbo tumewapa wanavikundi wa Kata ya Kipumbwi fedha za kuendeshea vikoba.
Nimetoa ng’ombe wa maziwa 24 wenye thamani ya Sh16 milioni kwa vikundi mbalimbali vya wanaume na wanawake, nimesaidia Umoja wa Vijana Saccos Sh3.5 milioni, pia Miembeni Saccos na Madanga Saccos wamepewa fedha kupitia mfuko wa jimbo.
9. Method Mkali, dereva wa bodaboda.
Rais Jakaya Kikwete alipofanya mkutano wake wa kampeni katika Viwanja vya Bomani ulimwomba daraja na barabara ya lami lakini hakuna kinachoendelea, nini tatizo?
Jibu. Julai 12 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara Wilayani Pangani aliwahakikishia kuhusu ujenzi wa barabara ya lami ya Tanga - Pangani - Makurunge - Bagamoyo ya urefu wa kilomita 178 ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
10. Haruna Mohamed, mfanyabiashara Pangani Mjini: Ni kwa kiasi gani umefuatilia ahadi alizotoa Rais juu ya jimbo letu?
Jibu: Nimefuatilia kila ahadi iliyotolewa na utekelezaji unaonekana. Hivi karibuni nimefuatilia suala la ujenzi wa barabara ya lami na hadi sasa kazi za usanifu wa kina na upembuzi yakinifu zimeshafanywa kilichobaki ni kupatikana mkandarasi ili kazi ya ujenzi iweze kuanza lakini kutokana na kulinda Hifadhi ya Taifa ya Saadani, barabara hii itachepushwa na itapita Pangani - Mkange - Makurunge – Bagamoyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake