Friday, November 7, 2014

Mbowe: Tabora ni kama vile wamepewa limbwata na CCM

Igunga/Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wananchi wa Mkoa wa Tabora ni kama wamepewa limbwata na CCM na kuendelea kutoa majimbo yote 10 kwa chama hicho licha ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa maskini nchini.
Mbowe alisema hayo jana katika Kijiji cha Choma wilayani Igunga akiwa ziarani katika mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Morogoro na Dodoma.
Jana, Mbowe akitumia chopa, alifanya mikutano mitano katika maeneo ya Bukene Mjini, Mwamali katika Wilaya ya Nzega na maeneo ya Choma, Igulubi na Igunga Mjini.
“Wana-Tabora ni kama vile mmepewa limbwata na CCM, majimbo yote 10 ya uchaguzi mmewapa CCM lakini mnaendelea kuwa maskini siku hadi siku, badilikeni,” alisema Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Mkoa wa Tabora una majimbo ya Tabora Mjini, Igunga, Nzega, Bukene, Sikonge, Igalula, Tabora, Tabora Kaskazini, Urambo Mashariki na Urambo Magharibi ambayo yote yanaongozwa na wabunge wa CCM.
Alisema wakulima wa Tabora wanaolima mpunga bado wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi kwa sababu CCM inakumbatia matajiri kwa kuwapa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje ya nchi.
“Mchele wa nje ukiingizwa nchini unauzwa kwa bei rahisi wakati mchele wenu unakosa soko na kusababisha hali ngumu, hiyo ndiyo CCM yenu mnayoipenda,” alisema.
Alisema vyama vya ushirika vilivyopo ambavyo baadhi vinaongozwa na vigogo wa CCM, vinawadhulumu wakulima wa Mkoa wa Tabora... “Wakulima wa nchi hii mna msiba mkubwa, msiba huu utakuwa wa milele kama hamtaungana kuing’oa CCM madarakani.”
Alisema CCM ina wenyewe na kwamba wenyewe hawaishi Igunga, bali Dar es Salaam katika maeneo ya Oystebay, Masaki na Mikocheni.
“Lakini kila wakija CCM mnawapa kura, Mbunge wa Igunga, Peter Kafumu mlimchagua mkamwacha wa Chadema, je, ametimiza ahadi zake?” alihoji Mbowe.
Aliwataka wananchi kuacha kuchukiana kwa misingi ya itikadi zao za vyama na kusema vyama vyote vishirikiane kuangalia namna vitakavyotokomeza umaskini.


“Nashangaa watu mnachukiana kwa misingi ya vyama wakati wote maskini, ichukieni CCM iliyoshindwa kubadilisha maisha yenu kwa muda mrefu,” alisema.
Mbowe alisema wananchi wasifanye makosa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 kwa kuwachagua wagombea wa Chadema.
“Novemba 22 hadi 30, wananchi wajiandikishe katika daftari la makazi ili kupata sifa ya kupiga kura bila kukosa, watendaji wa chama naomba muwahamasishe wananchi kujiandikisha,” alisema Mbowe.
Kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi alisema kushindwa kujiandikisha na kutopiga kura ni kuendelea kukumbatia umaskini.
Awali, akiwa jimboni kwake Hai juzi jioni, Mbowe alipinga agizo la Rais Kikwete kupiga marufuku vyama vya siasa na asasi za kiraia kufanya kampeni mapema za kuhamasisha wananchi kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa maelezo kuwa tayari CCM na Serikali wameanza kampeni hiyo.
Katika mkutano wake uliofanyika katika Kata ya Hai Mjini, Mbowe alisema kitendo kilichofanywa na Rais Kikwete kupiga marufuku elimu na kupunguza muda wa kampeni kutoka siku 60 hadi 30 ni njama za kuzuia wananchi wengi kupata elimu ya Katiba.
Mbowe ambaye alikabidhi greda kwa ajili ya ukarabati wa barabara za jimbo hilo, lori la taka pamoja na magari mawili ya wagonjwa kwa ajili ya Wilaya ya Hai, alisema kwa kuwa CCM na Serikali yake imeanza kushinikiza kura ya ‘ndiyo’, Chadema nayo imeanza kuzungumza na wananchi na haiwezi kuacha kuendelea kufanya hivyo licha ya tamko la Rais.
Mbowe alisema inatakiwa kutengeneza Katiba bora ya kuongoza Taifa kwa miaka 100 ijayo na kufikiria maisha zaidi ya siasa, lakini CCM inaangalia Katiba kama nyanja ya kuendelea kubaki madarakani.
Mbowe alisema Rasimu ya Jaji Warioba ilikuwa na mapendekezo mazuri ikiwamo kutaka viongozi wote wa kisiasa ndani ya nchi wachaguliwe na wananchi lakini CCM imeona ndiyo fursa ya kuchaguana, huku ikiendelea kumpa rais madaraka makubwa ya kuteua karibu viongozi wote wa ngazi za juu.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu 2015, Mbowe alisema CCM imekuwa ikishinda kutokana na vyama vya upinzani kutokuwa na umoja, hivyo kutumia udhaifu huo kushinda kirahisi lakini si safari hii.
“CCM wamekuwa na jeuri kwa kuwa tulikuwa tumegawanyika na sasa tusikubali kugawanywa kwa ukabila, kisiasa, dini wala itikadi zetu. Tutawaunganisha watu wa madhehebu yote na wasiokuwa na dini hadi tuweze kuiondoa CCM madarakani asubuhi,” alisema.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake