Na Mwandishi Wetu
KIUNGO mkabaji wa Azam FC, Salum Abubakar”Sure Boy”aliyeibuka Mchezaji Bora wa Oktoba juzi alikabidhiwa zawadi ya shilingi milioni 1/= na kombe dogo makabidhiano hayo yalifanyika muda mfupi kabla ya mechi ya raundi ya saba kati ya mabingwa watetezi Azam FC na Costal Union katika mechi ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara iliyochezwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika uwanja wa Chamanzi, ambapo Azam FC waliichapa Coastal Union 2-1.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam juzi,Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Kelvin Twissa,alisema kampuni yake itakuwa ikitoa zawadi kila mwezi kwa mchezaji anayefanya vizuri.
“Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu ina ushindani mkubwa, nasi (Vodacom Tanzania) kwa kushirikiana Bodi ya Ligi(TPLB)tumejipanga vizuri tutakuwa tunatoa zawadi kwa mchezaji anayeng’ara kila mwezi na mwezi uliopita tulitoa zawadi kama hii kwa Antony Matogolo wa timu ya Mbeya City,” alisema Twissa.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Salum aliyeonekana mwenye furaha, alisema; “ninawashukuru wachezaji na mashabiki wa Azam FC kwa ushirikiano wanaonipa, hii ni zawadi kwa timu nzima na mashabiki wa timu yetu.”
Aidha, Shabiki wa Azam FC Hassan Kihelelo wa kawe jijini Dar es Salaam alisema anaunga mkono juhudi zinazofanywa na mdhamini mkuu wa ligi”Vodacom Tanzania”na kusema kampuni hiyo imeonesha ukomavu na ubunifu wa hali ya juu katika kuleta maboresho ya ligi msimu huu kwa kweli inastahili pongezi kwani inafanya wachezaji wetu wanaoshiriki ligi kuu kuwa na moyo wa kucheza na kuonesha vipaji vyao vizuri na kujituma zaidi wakiwa uwanjani,alisema Kihelelo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake