ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 3, 2014

KIWANJA CHA NDEGE CHA KIGOMA KUTANULIWA

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Bw. Joseph Nyahende (Wapili kushoto) akitoa maelezo kuhusu Kiwanja cha Ndege Kigoma kwa Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia). Wanaosikiliza ni Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha (Kushoto) na Bw. Julius Edward (Wapili kulia).Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha (Kushoto) akifafanua jambo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mara walipofika kujionea shughuli za maendeleo kiwanjani hapo.
Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Bw. Joseph Nyahende (Aliyenyanyua mikono) akitoa maelezo juu ya sehemu zitakazoendelezwa kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akiangalia tabaka za udongo uliotumika katika kujengea Kiwanja cha Ndege Kigoma. Anayemuonesha ni Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Bw. Joseph Nyahende (Kulia).
Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha (Wapili kulia) akionesha eneo likaloboreshwa katika Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma.

Na Saidi Mkabakuli, Kigoma
Serikali imeazimia kuanza kufanya utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma ili kuweza kukidhi mahitaji yanaongeza siku baada ya siku ya kiwanja hicho.
Azma imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka  Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya  ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa  Kigoma.
Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege 
nchini ipo kwenye mkakati wa kuuendeleza uwanja huo ili uwe wa kiwango 
kizuri kwa kuhudumia watumiaji wa wa kiwanja hicho. “Kama munavyokumbuka Serikali katika mwaka ujao wa fedha imepanga kuendeleza  na kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi; na  kuendelea na kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika  maeneo ya kimkakati ikiwamo Kiwanja cha Ndege cha Kigoma,” alisema.
Kwa mujibu wa Bibi Mwanri, uendelezaji wa Kiwanja hicho utajumuisha ujenzi  wa jengo la abiria pamoja na miundombinu yake (maegesho ya ndege,  maegesho ya magari na barabara ya kuingia na kutoka) na kurefusha 

 barabara ya kuruka na kutua ndege.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya uwanja huo, Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja  cha Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha alisema kuwa mpaka sasa Mamlaka ya  Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini imekamilisha taratibu za kumpata  mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa usalama na eneo la maegesho ya ndege.
“Kwa sasa tunaendelea na kazi ya utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa  ajili ya kazi za ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani, maegesho ya 
magari, na usanifu wa kina kwa ajili ya upanuzi wa maegesho ya ndege 
pamoja na usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege,” alisema.
Mhandisi Neema aliongeza kuwa wapo kwenye mchakato wa kumpata Mhandisi Mshauri  wa kufanya usanifu wa jengo la abiria uwanjani hapo.
Naye Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Bw. Joseph Nyahende alisema  kuwa katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa wakati, Mamlaka ya  Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini kwa kushirikiana na Mkoa wa Kigoma vimeainisha na kufanyia tathmini eneo litakalotumika kwa ajili ya kazi  hiyo.

No comments: