Wanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Nyamarere mkoani Geita wakiwa darasani. Picha na Jackline Masinde.
Na Jackline Masinde, Mwananchi
Ni ‘majanga’ ya elimu katika baadhi ya shule za msingi mkoani Geita ambako hadi leo wanafunzi wanasomea chini ya miti, wanaketi kwenye mawe.
Geita. Tunaweza kusema ni majanga ya elimu. Tunasema hivi maana ni kama hakuna lugha rahisi ya kuelezea hiki kinachoonekana katika shule mbili za msingi; Nyamarere na Bweya zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita au Geita Vijijini kama ambavyo wengi hupenda kutamka.
Wanafunzi katika shule zote mbili wanaishi katika mazingira ya enzi za ujima kwani wengi wao wanasomea nje kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na baadhi yao chini ya miti ili kusaka kivuli, wakati wale wanaopata fursa ya kuingia katika madarasa wanakalia mawe kutokana na ukosefu wa maadawati.
Kuna nyakati ambazo wanafunzi wa madarasa mawili au matatu wanalazimika kutumia chumba kimoja na hapo mwalimu akiingia, huwafundisha walio wake kwa maana ya darasa husika na wale wa madarasa mengine huwa watazamaji iwe kwa dakika arobaini au themanini za somo.
Shule ya Msingi Nyamarere yenye madarasa ya kwanza mpaka sita, ina wanafunzi 742; wasichana 315 na wavulana 427 pamoja na walimu 12. Shule hii ina madarasa mawili tu na ofisi moja ya mwalimu mkuu ambayo pia hutumika kama maktaba na stoo.
Hii inamaanisha kuwa kwa idadi ya wanafunzi waliopo, chumba kimoja cha darasa kinapaswa kukaliwana wastani wa wanafunzi 371. Kwa upande wake, Shule ya Msingi Bweya yenye wanafunzi 401 ina vyumba vitatu, hivyo wastani wa wanafunzi katika darasa moja ni 134.
Niliwasili katika Shule ya Nyamarere muda wa saa 04:00 asubuhi na ilikuwa ni asubuhi tulivu huku anga likiwa limefunikwa na mawingu yaliyoashiria kwamba huenda mvua ingenyesha siku hiyo.
Nilipokewa vyema na mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Neema Martine ambaye alinikimbilia baada ya kuniona.
Mwanafunzi huyo aliyeonyesha nidhamu ya hali ya juu, aliniamkia kisha kunipokea mizigo yangu akiamini pengine kuwa mimi ni mwalimu mpya.
Baada ya kusalimiana, Neema aliwaongoza wanafunzi wenzake waliokuwa wameketi katika moja ya makundi mengi yaliyokuwa katika eneo hilo la shule akisema: “Heshima kwa mwalimu toa.”
Wanafunzi walisimama na kupiga saluti wakisema kwa pamoja: “Shikamaoo mwalimu”. Baada ya tukio hili waliketi na kuendelea na kile ambacho walikuwa wakifanya, ambacho kwa wakati huo sikufahamu kilikuwa ni kitu gani.
Kadiri nilivyokuwa nikiingia katika mazingira ya shule hii ya Nyamarere nilianza kuhisi kwamba makundi kadhaa ya wanafunzi niliowaona wakiwa wameketi nje, ni madarasa na walimu wao walikuwa wakiendelea kufundisha.
Wapo waliokuwa wameketi sehemu za wazi, wengine pembezoni mwa kuta za vyumba vya madarasa vilivyopo, wengine waliketi chini ya miti mikubwa ya miembe na wengine walikuwa wakiendelea na masomo katika boma la jengo ambalo halijaezekwa.
Katika eneo hili pia niliona walimu wakiwa wameketi kwenye madawati chini ya mti huku, hukuwa wakiwa wamepanga vitabu na madaftari ya wanafunzi juu ya madawati hao.
Baadaye pia nilibaini kwamba wapo wanafunzi waliokuwa kwenye madarasa mawili ambayo yameezekwa kwa bati nao wakiendelea na masomo.
Miongoni mwa mambo niliyoyaona kwa haraka ni kwamba wanafunzi wengi walikuwa wamekalia mawe, matofali na mifuko yao ya madaftari. Kwa maana nyingine hapa Nyamrere miti mikubwa ni madarasa na madawati ni mawe, matofali na mifuko ya madaftari ya wanafunzi.
Ufundishaji wa ishara, imla
Ilikuwa kama miujiza, kwani sikuamini kile nilichokiona kwa dakika chache kabla sijakutana na wenyeji wangu. Walimu walikuwa wakifundisha, lakini wengi walitumia ishara (kuchora au kuumba herufi hewani) na wengine walikuwa wakifundisha kwa kuwasomea wanafunzi (njia ya imla).
“Andika ‘a’, nasema andika ‘a’ unajua inavyoandikwa? inaandikwa hivi: (alionyesha ishara) umeelewa?” alionekana mmoja wa walimu ambaye baadaye nilikuja kubaini kuwa anaitwa Richard Kabadi na wale aliokuwa akiwafundisha chini ya mwembe ni wanafunzi wa darasa la kwanza.
Kadhalika nilisikia sauti nyingine: “Pangeni mawe na matofali yenu vizuri tuanze kipindi”. Baadaye nilikuja kubaini kwamba sauti hiyo ilikuwa ya mwalimu aitwaye Pascal Kanyerema.
Wakati huo pia nilishuhudia wanafunzi wakiinama ardhini kuandika au kunukuu yale waliyokuwa wakiambiwa na walimu wao. Hali hii inatokana na kukosekana kwa madawati hivyo madaftari yaliwekwa chini (ardhini) ili kuwawezesha kuandika.
Wananfunzi waliokosa mawe au matofali ya kukalia, walikaa chini, nguo zao zilichafuka. Walimu wao walionekana kukaa chini ya mti wa mwembe ambao wanautumia kama ofisi ya walimu.
Ufundishaji huu kwa njia ya imla na ishara ni matokeo ya shule hiyo kutokuwa na mbao za kufundishia. Upo ubao mmoja ambao ni siling board. Ubao huo huamishwa kutoka darasa moja kwenda jingine na kuegeshwa kwenye mti au ukuta tayari kwa mafunzo.
Baadhi ya walimu walilalamika kwamba ukosefu wa miundombinu unakwaza kazi yao ya kutoa elimu kwa watoto. Mwalimu aliyejitambulisha kwa jina la Ombeni sanga alisema: “Tukitaka kufundisha tunatumia ubao wa kuhamisha hususan kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili ambao hawajajua kusoma vizuri.”
Mwingine ni Paschal Kanyerema ambaye alisema: “Kama unavyoona hali ya shule hii, hatuna madarasa, hatuna ubao, hatuna madawati hatuna vyoo, hatuna ofisi za walimu.”
Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Esther Masalu anasema: “Haya ndiyo maisha yetu, tunakalia mawe, matofali na miti ndiyo madarasa yetu, tukiwa darasani hatuelewani kwani wengine wanapiga kelele.”
“Tunaandika vibaya, kwani tunaweka madaftari chini, tunachafuka kutokana na kukaa chini, mvua ikinyesha tunarundikana darasa moja madarasa matatu au manne,” alisema Masalu.
Omary Ramadhani anayesoma darasa la tano anasema: “Ebu jifikirie kweli tunasomea chini ya miti tena nje kabisa, mvua ikinyesha kwetu ni likizo, utaingia kwenye darasa la nani, ubao wa kudumu wenyewe hakuna,” Ramadhani.
Ramadhani analalamika hali hiyo inamuathiri kitaaluma, kwani wakati mwingine mwalimu anapokuja kufundisha hasa somo la hesabu hakuna ubao anafundisha kwa kusoma namba yaani imla.
“Hii huwa linaniathiri wakati mwingine najikuta sielewi kitu chochote, pia wenzangu ambao hawajui kusoma mwalimu akitusomea wanaandika vibaya,” alisema Ramadhani.
Maisha ya walimu
Ndani ya ofisi ya mwalimu mkuu ambayo pia hutumika kama maktaba na stoo, kuliliwekwa majembe ya shule, mabati, mbao, makabati ya vitabu na mafaili mbalimbali.
Baadhi ya wanafunzi walisema ikitokea mvua ikanyesha wakati wakiwa shuleni, hujikuta wakirundikana kwenye madarasa mawili yaliyopo na kutokana na wingi wao wengine huingia katika ofisi hii ya mwalimu mkuu paoja na walimu wao.
Upande mmoja wapo lilionekana jengo lililojengwa kwa nyasi na miti. “Hii ndiyo ofisi ya mwalimu wa taaluma, lakini ofisi hii pia hutumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza pale mvua zinaponyesha,” alisema mwalimu mwingine katika shule hii, Shaban Ally.
Mazingira haya ni kinyume cha sera ya elimu na mafunzo ya 2010 ambayo inasema kuwa mazingira bora na yenye usalama yatakuwa ni lazima katika utoaji wa elimu, pia miundombinu stahiki inayokidhi mahitaji yote katika ngazi zote za elimu na mafunzo ni lazima.
Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Seif Deusi anakiri kuzifahamu shule hizo na kudai Serikali kwa sasa haina fedha kwa ajili ya ujenzi.
“Nazitambua shule hizo kama shule za Serikali na matatizo hayo yanajulikana, lakini tatizo lililopo nikwamba kwa sasa bajeti haipo,” alisema Deusi.
No comments:
Post a Comment