ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 2, 2015

Salamu za Mbunge wa Nzega -CCM Dr. Hamisi Kigwangalla kwa Watanzania , Mwaka Mpya 2015


 Mbunge wa Nzega -CCM Dr Hamisi Kigwangalla
-
Ni Mwaka Mpya Tena! Dr. Hamisi Kigwangalla, MB.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Kwa heshima na taadhima na kwa moyo wa kiutumishi, najisikia furaha kuwatumia salamu za Mwaka mpya 2015. Kwa hakika Mungu amekuwa mwema sana kwangu na kwako mwaka 2014 kwa namna nyingi mbalimbali, ila kwa kiasi kikubwa kwa kutujalia zawadi ya uhai, mafanikio kwenye kazi zetu, uvumilivu tulipoanguka, nguvu tulipokutana na changamoto mbalimbali, na uwezo wa kupambana nazo tulipolazimika kufanya hivyo, na zaidi kwa kutusimamisha pamoja kwenye kamba ya mshkamano wa kitaifa kwa sisi sote kama watanzania.

Kwa niaba ya wanaNzega, familia yangu, marafiki na ndugu zangu wa‪#‎TeamBelieve‬, naomba nitumie fursa hii kuelezea hisia na fikra zangu za Tanzania tunayoitaka kwa Taifa letu zuri, ambalo mimi na wewe tunaita nyumbani kwetu.

Naomba niambatane kwenye majonzi na masikitiko makubwa na familia ya marehemu Dkt. William Mgimwa (MB), aliyekuwa Waziri wetu wa fedha, ambaye kifo chake kilituacha kwenye mtikisiko mkubwa. Naomba Mwenyezimungu ampumzishe kwa amani huko aliko.
Tunaposherehekea hizi sekunde chache za kuanza kwa mwaka 2015, naomba nianze kumtakia heri na fanaka za mwaka mpya Rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, zaidi ya yote, nakutakia afya njema, maisha marefu na nakuombea dua upone haraka kutokana na upasuaji uliofanyiwa siku za karibuni. Namuomba Mungu akuzidishie hekima, busara, nguvu zaidi, ari zaidi na kasi kubwa zaidi ya kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu.

Naomba pia nitumie fursa hii kumtakia kila la kheir Makamu wetu wa Rais Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (MB), na Mawaziri wote, Naibu Mawaziri wote, Wakuu wote wa Mikoa, Makatibu wakuu wote na maofisa wote wa serikali. Dua zangu kwenu ni kuwa Mungu awajaaliye afya tele, nguvu, furaha na mafanikio katika kutekeleza majukumu yenu, na zaidi ya yote namuomba Mungu awajaalie ubunifu, moyo wa huruma na bidii ya kulitumikia Taifa letu kuelekea safari yetu ya kuijenga Tanzania mpya tuitakayo.
Kwa namna ya kipekee kabisa, ninawatakia heri na fanaka ya mwaka mpya wabunge wenzangu, nikianza na Spika wetu wa Bunge, Mhe. Anne Semamba Makinda (MB.), Naibu Spika, Mhe. Job Yustino Ndugai (MB.), Wenyeviti wenzangu wa Kamati za Bunge, Makamu Wenyeviti wa Kamati za Bunge, Makamishna wa Bunge, Wabunge wenzangu wote, Katibu wa Bunge, na Dkt. Thomas Didimu Kashililah na watumishi wote wa Bunge. Mungu atujaalie sote afya njema, busara na hekima katika kulitumikia Taifa letu, atujaaliye mijadala yenye amani, utulivu na ustahimilivu, mwangaza wa mawazo wakati tukitunga sharia na kufanya maamuzi yenye haki na sahihi kwa niaba ya watanzania wenzetu.

Mwaka 2014 ulikuwa mwaka mgumu sana. Tulikuwa na changamoto nyingi za kitaifa, tunamshukuru Mungu tulipambana nazo kwa uwezo wake tukavuka kwa hekima, busara na uvumilivu mkubwa tuliopata kutoka kwake.

Kazi ya kuandika Katiba mpya ilikuwa kubwa na nzito sana kwetu, tulifanya kazi usiku na mchana, na mijadala ndani ya nchi ilikuwa mikali sana. Pamoja na vikwazo hapa na pale, pamoja na tofauti zetu hapa na pale, mchakato wa mapatano ulitusaidia sana kupata ‘Katiba inayopendekezwa’ ambayo ninaamini kwa kiasi kikubwa ni nyaraka bora na ya kisasa zaidi ilinganishwa na Katiba ya mwaka 1977. Katiba inayopendekezwa inatarajiwa kupigiwa kura Aprili 30, niwasihi watanzania tuzingatie falsafa ya umoja wetu ndiyo ushindi wetu, tushikamane kuipigia kura ya ndiyo tupate Katiba mpya tufanye mabadiliko makubwa katika Taifa letu. Mimi ninaamini kwamba kinachojaribu kututenganisha kinatupa nguvu zaidi kuliko kinachotuunganisha pamoja kama watanzania.

Mchakato wa kuandika Katiba mpya haujawahi kuwa wa rahisi hata siku moja. Na kwa hakika hautegemewi uwe wa rahisi hata siku moja. Na hii ni kwa sababu kila watu, mmoja mmoja na kwa makundi yao mbali mbali, wana maslahi yao ambayo wangependa yaingie kwenye katiba, na kila mmoja anajua wazi kabisa kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya unatoa fursa ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye namna nchi inavyoongozwa hivyo kila mtu anakaa macho kuona jambo lake halisahauliki akizingatia kuwa mchakato wa kuandika katiba mpya hautegemewi kujirudia siku za usoni.
Hata hivyo, jambo moja la muhimu kuzingatia ni ukweli kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya ni mchakato wa kujenga muafaka wa kitaifa kwenye mambo ambayo yanakuwa yalikuwa kwenye mjadala mkali na ama wa muda mrefu. Mchakato wa kuandika katiba mpya unatoa fursa ya mjadala mpana wa kitaifa na mwishowe mabadiliko makubwa yenye muafaka kutokea.
Kwa hapa tulipofikia tunalazimika kutazama wapi tulipotoka na vipi turekebishe. Mawazo yangu ni kwamba, bado hatujachelewa kujadiliana na wenzetu wachache wenye hoja zao, tujue tunatofautiana wapi, tunarekebishaje. Tanzania ni yetu sote, ni busara tukakubaliana mambo ya kurekebisha sasa, tukaenda kwenye kura ya maoni tukiwa wamoja, tukaipitisha katiba yetu, na kisha tukafanya hayo marekebisho, kama yatakuwepo, baada ya kuwa na Katiba mpya.

Katiba inayopendekezwa haina umakini wa kimungu kama ilivyo Qur’an ama Biblia kwa sababu imeandikwa na wanadamu wenzetu, inaweza kuwa na makosa hapa na pale, mapungufu hapa na pale, na hivyo tukiwasikiliza wenzetu tutajua nini tufanye. Naomba sana wakubwa wenye mamlaka watafakari ushauri wangu na waufanyie kazi. Hata siku moja hakuna kuchelewa kwenye kufanya jambo zuri. Ni jambo lisilokubalika kusema kuwa Katiba inayopendekezwa haina mapungufu na vile vile si sahihi kusema kuwa Katiba inayopendekezwa ni mbaya kuliko ya mwaka 1977 inayoishi sasa. CCM, kama Chama chenye dhamana ya kuliongoza Taifa letu kina wajibu, kwenye mazingira kama haya, kutoa uongozi unaohitajika kwa Taifa kwa kuwasikiliza wachache, kushauriana nao kama wabia na kutafuta namna ya kuyafanyia kazi matamanio na matarajio yao.
Jambo lingine kubwa lililogusa nyoyo za watu wengi lilihusu kashfa ya kuchotwa kwa fedha kwenye akaunti ya escrow ya Tegeta. Kwenye hili, nilipata fursa ya kualikwa kama mjumbe wa Kamati ya hesabu za serikali iliyokuwa imejigeuza kama kamati ya uchunguzi. Mwanzoni nilitaka kukataa mwaliko huu, lakini mwishoni niliamua kukubali na kumuomba Mungu sana aniongoze kwenye kutekeleza majukumu yangu kama mjumbe mwalikwa kwenye kamati hii nyeti. Tulichokibaini na kukichambua kiko wazi kwa umma. Sintokirudia hapa. Kutokana na hili, somo la muhimu zaidi hapa kujifunza ni namna gani tunahitaji uzalendo miongoni mwa watumishi wetu wa umma na ni namna gani tunaweza kuwatia uzalendo kwa taifa letu kiasi cha kustawisha misingi ya uwajibikaji na kuweka nidhamu ya kazi.

Kwenye escrow, kamati imefanya kazi yake, na haikuingiliwa na mtu, Bunge nalo likatimiza wajibu wake likamaliza. Sasa jambo hili liko mikononi mwa Rais, na nadhani ni busara kumwacha Rais naye alifanyie kazi namna atakavyoona inafaa.
Kama Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI, naomba nitumie fursa hii kuipongeza serikali kwa kuendesha kwa mafanikio makubwa uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na maandalizi ya muda mfupi na changamoto zilizojitokeza. Pia naomba niipongeze serikali kwa kuamua kuuhamishia uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye tume ya taifa ya uchaguzi, na pia kwa kuchukua hatua za kuwawajibisha wakurugenzi wa halmashauri zilizovurunda kwenye uchaguzi huo. Tunawajibika kuilinda misingi hii kwa ajili ya kulinda amani na utulivu katika taifa letu.

Mwaka 2014 ulikuwa ni wa kipekee kwangu kwa kuwa niliamua kuweka wazi kuwa nitagombea Urais mwaka 2015.

Nilipoamua kutangaza nia kuutaka Urais nilisema kwenye hotuba yangu kuwa nchi yetu inahitaji namna mpya kabisa ya kufikiri na kufanya mambo, namna ambayo itatufanya sisi tukimbie wakati wengine wakitembea. Namna ambayo itaifanya nchi yetu ipate maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kasi.

Nilisema kwamba nina IMANI kubwa katika ndoto za waasisi wa taifa letu ambao walikuwa na imani kubwa kwa Tanzania na kwa watanzania, na uwezo wetu wa kusimama imara kujenga taifa letu kwa staili yetu, na kwamba ninaamini katika misingi na itikadi ambazo zilianzisha vyama vya ASP na TANU, na baadaye CCM, na kwamba amani na utulivu vitadumu tu endapo tutaendelea kuheshimu ubinadamu na utu wa kila mmoja wetu, na kama sisi viongozi tutaimarisha utawala bora na tutawajibika kwa watu wa nchi yetu. Na kwamba tutatoa fursa sawa kwa watu wote bila kujali hali zao za kiuchumi ama kijamii, rangi za ngozi zao, jinsia na au umri.

Tanzania ni kati ya nchi ambazo, tulipokuwa tunakua, kijana mdogo kama mimi aliyezaliwa na kukulia katika familia maskini ambapo mama yake mzazi alilazimika kufanya biashara ya kuuza vyakula kwa wachimba dhahabu wadogo wadogo kwenye migodi midogo, aliweza kufaidika na mfumo wa elimu sawa kabisa na mtoto wa Mkuu wa Mkoa ama wa Waziri, mfumo imara wa afya ya msingi, na fursa ya kutamani kuwa mtu yeyote katika ukubwa wake ikiwemo kutamani kuwa Rais wa nchi yake. Hii ni Tanzania ya waasisi wetu, nchi nzuri ambayo tumerithi, na pamoja na ukweli kwamba dunia imebadilika sana, namna ya kufanya mambo pia imebadilika, baadhi yetu tunaamini kwamba mawazo ya waasisi wetu bado yako sahihi. Fikra na itikadi zao bado ziko sahihi na ni lazima tuzilinde.

Moja ya vitu vinavyonisukuma kuamini katika NDOTO yangu ya kuliongoza Taifa letu ni IMANI yangu kwa Tanzania na watanzania wenyewe, kwamba tunaweza kuota vitu vikubwa zaidi, tunaweza kufanya kazi kwa bidii zaidi, na tunaweza kufanikisha mambo yetu kwa haraka zaidi. Kama baba wa Taifa letu, Mwl. J, K, Nyerere, alivyowahi kusema ‘tukimbie wakati wengine wanatembea’.

Fikra hizi ziko kwenye sakafu ya moyo wangu, tunahitaji kukimbia wakati wengine wanatembea. Ninaamini tunahitaji kuwa na muafaka wa kitaifa, kwamba tunafungua mlango wa mapinduzi kwenye uchumi wetu kwa ajili ya mustakabali wetu na watoto wetu, na kwamba tunaazimia kufanya mambo makubwa ya kupigiwa mfano na wenzetu, na kwamba tunaamua kuwa watu wenye kufanya mambo yao kwa ubora wa ajabu na kwamba yeyote asiyeweza kwenda na sisi hana nafasi baina yetu. Hii ndiyo Tanzania yetu ya baadaye.

Nilipotangaza nia yangu kuwania Urais nilisema, kwamba mengi yameishafanywa na viongozi waliotutangulia, wameandaa mazingira, na kwamba ni jukumu letu sasa kukimbiza harakati za mabadiliko kwa spidi ya mwanga, kwa kuwa tunajua kinachopaswa kufanywa, maana tuna zaidi ya miaka hamsini toka tujaribishe hili ama lile, leo hatutegemewi tukosee, kama ilivyokuwa kwa wazee wetu. Tunachohitaji kwa sasa ni jitihada za maksudi na za haraka.

Na kwamba NINAAMINI katika uwezo wa chama changu, CCM, kukubali na kuongoza MABADILIKO katika staili ya uongozi, fikra za kuongoza, na hata mawakala wa mabadiliko tunayoyataka, kwa kuwa CCM ilijengwa kwenye msingi wa mapinduzi. Haijawahi kuwa chama cha kihafidhina, CCM ni chama cha kimapinduzi. Ni chama cha mabadiliko. Siku zote CCM kimekuwa ni chama kinachowaunganisha na kinachowaongoza watanzania kwenye mapinduzi ya maisha yao, kwenye mabadiliko ya nchi yetu. Kama CCM itasahau misingi iliyokijenga, nchi itaparaganyika na boti litakwenda mrama katika siku si nyingi.

Watanzania siku zote wamekuwa na matumaini makubwa na imani kali juu ya CCM, sera zake na viongozi wake. CCM ina wajibu wa kuyatilia maanani matumaini, ndoto na imani za watanzania. Maluteni wake ni lazima tufanye kazi ya umma tukiwa na matumaini, ndoto na imani ya watanzania moyoni. Tukiwa na matumaini, ndoto na imani ya watanzania kwenye moyoni, na kwenye vichwa vyetu ni lazima tuongoze mapinduzi ya kiuchumi na kijamii katika taifa letu. Ni jukumu letu, sisi, maluteni wa CCM, kuikumbatia falsafa ya ‘e pluribus unum’ na tuishi na kufanya kazi kwa faida ya wote na si kwa faida yetu binafsi. Na wakati ni sasa.

Ni lazima tuamke kutoka kwenye imani kuwa CCM ni chama kikubwa na kikongwe na tutaendelea kutawala tu, na tukumbuke kuwa hizi ni zama nyingine, na namna watu wanachukua madaraka imebadilika pia. Ni lazima tuamke kutoka kwenye raha ya kujiamini. Tusipoamka sasa, tusijeshangaa kuangukia pua ghafla bila kutegemea.
Na baada ya kusema haya, nawatakieni nyote Mwaka Mpya wenye Neema. Karibu mwaka 2015. Tutaandika historia pamoja mwaka huu.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

Hamisi Kigwangalla (MB),
Jimbo la Nzega,
Mwenyekiti, TAMISEMI. 
January 1st, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

angalia sana na wewe wasije wakakubwaga na elimu yako umesomea udoctor unaona bora uwe mwanasiasa siyo?watch out hicho chama ni cha ufisadi tuu