Rais Jakaya Kikwete.
Eric Shigongo
Nianze kwa kumtukuza Mungu muumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana, hakuna wa kumuabudu ila yeye tu.Nianze makala yangu kwa kusema kuwa bado hakuna mwafaka kuhusu hatima ya Katiba Mpya, baada ya kuahirishwa kwa upigaji kura ya maoni iliyopaswa ifanyike Aprili 30, mwaka huu kama alivyowahi kutangaza Rais Jakaya Kikwete.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisema Kura ya Maoni itafanyika wakati wowote mwaka huu baada ya kukamilika uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR), wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani, wanaamini kuwa hauwezi kufanyika kutokana na matatizo ya kisheria na wakati.
Hata hivyo, kuna wanaharakati wengine wanasema kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, kungetoa fursa ya mchakato huo kurudi kwenye Bunge Maalum la Katiba ili ukajadiliwe upya.
Wapinzani na wanaharakati haohao wanasema hili litasaidia kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa Bunge la Katiba ambako kundi la wabunge wa upinzani lilisusa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).Hata hivyo, wapo wanaoamini pia kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, ndiyo mwisho wa Mchakato wa Katiba Mpya licha ya mabilioni ya shilingi za walipa kodi kupotea, hasa baada ya rais aliyeanzisha mchakato huo kumaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu.
Nec iliahirisha Kura ya Maoni iliyopaswa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kutokana na kudorora kwa shughuli ya kuandikisha wapiga kura kwa kutumia BVR na sasa haijulikani lini zoezi hilo litafanyika.Hakuna ubishi kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na mabadiliko yake yaliyofanyika mwaka 2012 na Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, ziko kimya juu ya nini kinafuata baada ya kuahirishwa kwa Kura ya Maoni.
Sheria zimeeleza nini kitafuata kama kura ya ‘Ndiyo’, haitafika zaidi ya asilimia 50 kutoka pande zote za Muungano.
Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Kura ya Maoni na Kifungu cha 36(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinasema kama kura za ndiyo hazifiki zaidi ya nusu ya wapiga kura wote Bara na Zanzibar, Tume ya Uchaguzi (Nec), na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa makubaliano maalumu na baada ya tangazo la serikali, watachagua njia nyingine ndani ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo hayo.
Ikifikia hapo mchakato wa upigaji Kura ya Maoni utaanza upya. Sheria zote zimempa rais mamlaka ya kuitisha tena Bunge la Katiba kubadili vipengele vilivyokataliwa wakati wa upigaji kura.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria ya Kura ya Maoni pamoa ja na Kifungu cha 36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vinasema, kama kura za ‘Hapana’ zitakuwa nyingi ikilinganishwa na kura ya ‘Ndiyo’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.
Naamini kuwa siyo sahihi kuendelea na mchakato wa Kura ya Maoni, kabla ya kupitia upya maeneo yaliyoleta mpasuko kwenye Mchakato wa Katiba. Haya mambo yanawezekana yakajadilika na tusiruhusu yatufarakanishe.
Kwa maoni yangu, Kura ya Maoni isifanyike mwaka huu kwa sababu ya mazingira ya kisiasa yaliyopo. Bado kuna haja ya kukaa meza moja na kujadili suala la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na kupinga matokeo ya rais mahakamani.
Rais ajaye naamini ataendeleza tulipofikia ili tupate katiba inayokubalika na wote.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
GPL
1 comment:
Muda Huu ni wa Majeruhi au "Funfulia Mbwa" . Hivyo rais labda ukikamilisha ahdai tu , kamavile Meli huko ziwa Victoria au Kuruhusu wawekezaji waweke Chombo ziwa Victira na ziwa Tanganyika: Hachana na Katiba, maana utatuletea vurugu!
Wewe Tundika "Buti lako Octoba"
Asante kwa kutuachia Amani.
Post a Comment