ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 15, 2015

Asilimia 84 ya wananchi wanaunga mkono kifungu cha sheria ya upatikanaji wa habari

15 Juni 2015, Dar es Salaam: Asilimia 84 ya wananchi wanaunga mkono kifungu cha sheria ya upatikanaji wa habari. Wananchi nane kati ya kumi wanaamini taarifa za mamlaka za umma zinapaswa kupatikana kwa wananchi wa kawaida (77%). Wengi wanaamini upatikanaji wa taarifa utasaidia kupunguza ama kuzuia rushwa na vitendo vingine viovu vinavyofanywa na viongozi wa umma (80%).

Haya ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Twaweza wenye jina, Machoni mwa Umma: Maoni ya wananchi kuhusu upatikanaji wa habari. Taarifa za utafiti huu zimekusanywa na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika unaofanywa kwa njia ya simu za mkononi. Utafiti huu una uwakilishi wa nchi nzima. Matokeo ya utafiti huu yamejikita kwenye taarifa zilizokusanywa kutoka kwa wananchi 1,330 wa Tanzania Bara (Zanzibar haikushiriki katika utafiti) kati ya mwezi Machi na Aprili 2015.

Wananchi wanaunga mkono uwepo wa kifungu katika sheria ya upatikanaji wa habari ambacho kitatoa adhabu kwa viongozi wasiozingatia sheria. Aslimia 47 wameonyesha kifungu hicho ni cha muhimu kwenye sheria hiyo. Mwananchi mmoja kati ya watano (21%) anataka sheria hii izilazimishe mamlaka za umma kutoa taarifa. Pamoja na hayo, washiriki wametaka watoa habari walindwe (18%).

Upatikanaji wa habari pasipo malipo siyo jambo la muhimu sana, ila ni mwananchi mmoja tu kati ya kumi aliyeona umuhimu wa kipengele hiki. Vilevile, muda unaotumika kujibu maombi ya kupatiwa taarifa/habari umetajwa na asilimia 5 tu ya wananchi.

Wananchi wanaeleza kuwa wanapotafuta taarifa kutoka kwa watoa huduma wa umma huwa wanazipata. Asilimia 95 ya wale waliotembelea mamlaka za maji (44% ya wananchi wote) walipatiwa taarifa walizohitaji. Sawa sawa na mashuleni, asilimia 43 waliulizia taarifa na asilimia 84 yao walipewa taarifa hizo. Upande wa huduma za afya nao wanafanya vizuri japokuwa wananchi wanaohitaji taarifa hizo ni walikuwa wachache. Asilimia 19 ya wananchi ndiyo walioomba taarifa na asilimia 84 yao ndio waliopewa taarifa hizo.

Hata hivyo serikali za mitaa na vyama vya siasa havina mwamko wa kutoa taarifa. Katika ngazi ya serikali za mitaa, asilimia 76 ya wananchi walioomba taarifa walijibiwa. Na katika vyama vya siasa ni aslimia 39 tu ya maombi ya taarifa yaliyojibiwa.

Wananchi wana matarajio tofauti kabisa kuhusu upatikanaji wa taarifa. Mwananchi mmoja kati ya kumi (12%) anaamini atapata taarifa anazohitaji mapema pindi akizihitaji huku idadi hiyohiyo ikiamini haitapata.

Wananchi waliobaki wamegawanyika katika makundi mawili wakiamini inaweza kuwachukua kipindi cha kati ya wiki moja mpaka miezi mitatu kupata taarifa. Huku kumlinda mtoa taarifa ikionekana kutokupewa kipaumbele, asilimia 62 ya wananchi wanasema wapo tayari kutoa taarifa ya vitendo viovu pindi wakivishuhudia. Mwananchi mmoja kati ya kumi alionyesha kutokuwa tayari kutoa taarifa ya vitendo kiovu (11%) na alipoulizwa kwanini – asilimia 37 ya wananchi (au 4% ya wananchi wote) walijibu kuwa ni “hatari”.

Elvis Mushi, Mratibu wa Sauti za Wananchi alisema: “Wananchi wanaunga mkono sheria ya upatikanaji wa habari, lakini wana mahitaji maalumu hasusani katika suala la uwajibikaji”

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, aliongeza “Taarifa hizi zinaonyesha kuungwa mkono kwa sheria ya upatikanaji wa habari. Kinachohitajika ni viongozi kutoa habari/taarifa pindi zinapoombwa. Tofauti na inavyodhaniwa na wengi, watoa huduma za umma huwa wanatoa taarifa ndani ya muda mfupi. Kinachoshangaza ni kuona vyama vya siasa vikiminya taarifa. Sheria ya upatikanaji wa habari imefikishwa bungeni hivi karibuni ikiashiria utekelezwaji wa matakwa ya wananchi ya kuwarahisishia kupata habari. Sasa ni wananchi wenyewe kuhakikisha wanautengeneza mswada huu kwa namna itakayowapatia haki yao ya kikatiba ya kupata habari.”

No comments: