Wednesday, August 12, 2015

Lowassa: Anayejua Richmond ni Kikwete


Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, kwa mara ya kwanza amemtaja Rais Jakaya Kikwete ndiye anayefahamu kwa kina mkataba wa Kampuni ya Richmond uliosababisha nchi kupata hasara ya mamilioni.
Lowassa anasema, “mamlaka ya juu” ukiachilia mbali yeye aliyekuwa waziri mkuu wakati huo mkataba ukisainiwa ilikuwa inajua kila hatua na kwamba ndiye alikuwa akimaanisha Rais ambaye kwa sasa ni Jakaya Mrisho Kikwete.

Anayetafsiri mamlaka ya juu ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antipas Lissu, aliyezungumza na JAMHURI mambo mbalimbali hasa linalohusiana na nyadhifa na kuhamia kwa Lowassa Chadema.

Akizungumza kwa utaratibu na kupangilia maneno na sentensi, Lissu anasema kwamba ni ngumu kwa mkataba ule wa Richmond uliogharimu uwaziri mkuu wa Lowassa kushirikisha kiongozi mmoja tu katika mfumo wa uongozi.

“Kashfa ile kubwa haiwezekani kumhusisha Lowassa peke yake,” anasema Lissu na kuongeza: “Lowassa ametoa majibu, amesema kilipoanza kunuka aliwaambia makatibu wakuu…jamani eeeh tuvunje huu mkataba.

“Sasa Philip Luhanjo ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi wakati huo akawaambia kwamba amezungumza na Rais (Jakaya Kikwete), Rais amekataa. Tuendelee. Wakati huo Rais Kikwete alikuwa safari.

“Si Luhanjo pekee. Hata Gray Mgonja wakati ule akiwa Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha, alimwamba, mkataba uendelee maana mamlaka ya juu imeamua hivyo,” anasema.

“Aliporudi Rais Kikwete nchini. Maana hakuwako. Mheshimiwa Lowassa alimfuata akamwambia kimenuka, tuvunje huu mkataba…Rais akasema nimeshauriwa na makatibu wakuu wangu, tusivunje huu mkataba. Tuendelee nao. Sasa Lowassa akawajibika kisiasa.”

Lowassa anamtaja Rais Kikwete hivi karibuni wakati anakaribishwa Chadema ambako yeye na mkewe, Regina Lowassa walipewa kadi mpya za kutambulika kuwa wanachama halali wa chama hicho.

Lowassa alisema hayo baada ya kuhojiwa na mmoja wa waandishi ambako katika majibu ya kukana kuhusika kwake, alikwenda mbali akisema, anayedhani kwamba ana ushahidi, apeleke mahakamani.

“Nipende tu kusema mimi kama waziri mkuu. Kwa kawaida ya sheria huwa ninaletewa mkataba muda wa mwisho kuupitia na kuupitisha… huwa sihusiki na kuandaa mikataba…

“…Mwenye mamlaka ni waziri husika, hivyo baada ya kuletewa mkataba husika wa Richmond niliupitia na kiukweli niliuwekea shaka kwa sababu nilishawahi kuwa waziri wizara ya maji nina uzoefu na kuandaa mikataba.

“Nilishauri mkataba huo uvunjwe lakini, waziri wa nishati na akawasiliana na ngazi ya juu na kulazimishwa kuupitisha mkataba huo,” anasema Lowassa.

Baada ya kugundua mkataba huo kuwa na upungufu mwingi, anasema: “Nilichukua maamuzi magumu (uamuzi mgumu) na kubeba mzigo wote ndio maana hadi leo wanasema mimi ni fisadi wa Richmond.

“Nipende kumaliza kwa kusema kwamba mwenye ushahidi wa Richmond aende Mahakamani. Vinginevyo watu wafunge midomo yao na kukaa kimya,” anasema.

Hii si mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumzia kashfa hiyo kwani Mei, mwaka huu wakati anatoa taarifa kuwa ana safari ya kwenda Arusha, kutangaza nia ya kuwania urais, Lowassa alizungumzia hilo akiwa Dodoma.

Huko Lowassa alisema kwamba chuki na roho mbaya dhidi yake hasa katika nafasi ya uwaziri mkuu ilikuwa ajenda iliyosababisha kujiuzulu kutoka kwenye wadhifa huo miaka saba iliyopita.

Kadhalika, Lowassa alipata kulisema hilo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Novemba, mwaka 2011 baada ya kushutumiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa ni fisadi.

Kwenye kikao hicho, Lowassa alipopewa nafasi ya kusema, alinukuliwa na baadhi ya wajumbe akisema, “Mwenyekiti (akiwa na maana Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete) utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema…

“…Lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo (siku hiyo ya kikao) hii ninahukumiwa na kuitwa fisadi kwanini?”.

“Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo (siku hiyo ya kikao) nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wanaCCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?

Taarifa zinasema hoja ya Lowassa ilizimwa mara moja baada ya kutoa kauli ifuatavyo, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo.”

Akizungumza namna ambavyo Chadema wamempokea Lowassa, Lissu anasema kwamba mapendekezo ya chama chao ilikuwa ni kushawishi hatua za kisheria, kitu ambacho hakikufanywa na Serikali ingawa mwanasiasa huyo mkongwe aliwajibika kisiasa.

“Hatujawahi kusema kwamba wasipowajibishwa, basi hatutawapokea. Tunataka watoke kwenye CCM, ili tuiwajibishe CCM na tujenge nchi upya kwa misingi ya isiyokuwa ya ki-CCM,” anasema Lissu.

Anasema kwamba katika hali ya kawaida na mazingira ya sasa ya siasa inayohitaji mabadiliko ni ngumu kumkwepa Lowassa kwa sababu ana nguvu ndani na nje ya CCM pamoja na kwenye mfumo unaotawala.

Anasema kwamba Chadema wamefanya utafiti wa kutosha na kupata majibu ya utafiti wa kampuni kadhaa zinazopata nafasi za usimamizi huru, wamewaambia kwamba wakipata mtu mwenye nguvu kama za Lowassa, watashinda uchaguzi.

Anakiri kwamba kuna wanachama wenye hofu ndani ya Chadema ambako Lissu anatumia nafasi hii kuwatoa hofu akisema, “Kamati Kuu ya chama ina watu wenye maarifa sana. Ina watu wenye kufanya uamuzi mzito baada ya kupokea ushahidi na kuujadili kwa kina. Haikufanya uamuzi rahisi.

“Uamuzi mgumu umefanyika baada ya mjadala mkali na wa muda mrefu. Hakuna kiongozi wa juu wa chama ambaye hakushiriki kwenye process (mchakato huu) hii,. Mwenyekiti na makamu wake wa bara na visiwani, katibu wa chama na wasaidizi wake na wajumbe wa Kamati Kuu. Tumefanya uamuzi si wa kushitukiza.

“Tumefanyia kazi sana kwa siku nyingi. Tulianza siku nyingi. Tulianza kufikiria hiki kinachotokea kwenye CCM maana yake nini? Hizi alama za nyakati zinatuambia nini? Na tujipangaje, kwa hiyo tulifanya tafakuri ya kina,” anasema.

Chadema kwa sasa wako kwenye vikao vya kupitisha jina la Lowassa ambako juzi Jumapili kiliketi kikao cha Kamati Kuu, Baraza Kuu pia liliketi na na leo wanatarajiwa kuendelea na mkutano mkuu.

Lowassa anatarajiwa kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambako Mwenyekiti Mwenza wa umoja huo, James Mbatia, amebainisha kwamba Lowassa akipewa majukumu ataweza.

Kadhalika Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anasema kumekuwepo na propaganda nyingi zikidai kuwa Chadema tunapokea mafisadi, lakini chama hicho kimeangalia mahitaji ya sasa ili kuleta mageuzi ya kweli nchini.

Naye, Profesa Lipumba anasema kwamba anampongeza Lowassa na kwamba anamuunga mkono kwa sababu uzoefu wake tangu aanze kuwania urais 1995, CCM imekuwa “Ikitupindua, lakini mwaka huu kazi imekwisha.”

Aidha wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, wamesifu hatua ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuamua kuachana na chama chake tawala na kuamua kujiunga na upinzani wakisema ni hatua kubwa na inaonyesha namna siasa za Tanzania zinavyozidi kukua.

Itakumbukwa kwamba kwa Afrika Mashariki, Tanzania na Zimbabwe ndizo zilizokuwa hazijatikiswa kisiasa, lakini historia hiyo imejidhihirisha kwa Tanzania Julai 28, mwaka huu baada ya Lowassa kuandika historia hiyo.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Kitila Mkumbo anasema Lowassa anapaswa kupongezwa kwa hatua aliyofikia kuamua kujiunga na upinzani.

“Kitendo cha waziri mkuu wa zamani na kada wa CCM ambaye kwa kweli hafahamu maisha mengine yeyote zaidi ya kufanya kazi CCM na serikali yake kukuamua kuingi upinzani ni jambo kubwa na kwa kweli haijawahi kutokea na kwa kitendo hiki ni wazi kwamba siasa za Tanzania zimebadilika kwa kiasi kikubwa.

Profesa Mkumbo anasema kwa muda mrefu hasa tangu katika mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1995 ikiwa mgombea atawania urais husubiri kuapishwa kuwa rais hivyo ikiwa atateuliwa kuwania urais kupitia upinzani ni wazi kwamba Dk. John Magufuli (mgombea urais wa CCM) ana kazi kubwa ya kufanya.

Hata hivyo upinzani (Ukawa) hasa Chadema wana kazi kubwa kwa sababu kabla hawajampokea Lowassa siku za nyuma walimchafua kwa kumtupia kashfa nyingi kwamba ni fisadi na hivi sasa wana kazi kubwa ya kuwaeleza wananchi vinginevyo kwamba waliyosema siku zilizopita kuhusu Lowassa hazikuwa za kweli na itategemea wananchi watalipokea vipi.

Profesa Mkumbo amesema pia katika hilo mshindi wa pili ni Chadema, kwa sababu katika hali ya kawaida ingekuwa linazungumzwa kuhusu usajili wa timu ni wazi kwamba hakuna kocha mwenye akili sawa sawa angekataa kumsajili Lowassa.

Pamoja na hilo, Profesa Mkumbo anasema katika hilo Chadema wamesajili mchezaji maarufu ambaye katika hali ya kawaida ingekuwa ngumu kwa kocha mahiri kukataa kumsajili.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Onesmo Kyauke, amesema hatua hiyo imeonyesha namna demokrasia na mfumo wa vyama vingi unavyozidi kukua.

Amesema kwa kitendo cha Lowassa kuamua kujiunga na upinzani umezidi kuvipa nguvu vyama vya upinzani.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya Kisiasa Julius Mtatiro amesema hatua ya Lowassa kujiunga na upinzani ni pigo kubwa kwa CCM kwani uondokaji wake umekiacha chama hicho kuwa na tumbo joto.

Kwa mujibu wa Mtatiro ikiwa Lowassa atateuliwa kugombea urais kupitia Ukawa; nchi itarajie kupata kampeni zenye ushindani mkubwa ikizingatiwa kwamba amekuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi.

Amesema pamoja na mambo ambayo Lowassa ametajwa nayo likiwemo la Richomond ambalo ameshalizungumzia hivi karibuni lazima nchi ikubali kwamba Lowassa ni mtu mwenye nguvu hivyo kwa hali hiyo amekiacha CCM katika hali ngumu.

Mtatiro ameongeza kwamba kwa siasa za Tanzania hali inayoonekana kwa sasa ni kwamba hilo ni hitimisho la mpasuko kwa CCM kwani chama hicho hakijaanza kukosolewa leo hivyo hatua ya Lowassa ambaye ni mwanasiasa mwenye nguvu kukihama chama chake ni kiashirikia kikubwa,

Kwa mujibu wa Mtatiro, Lowassa ana nguvu kubwa kwani karibu robo tatu ya wanachama wa CCM wanamuunga mkono.
Taarifa zinasema kwamba kwa sasa Lowassa ana amani moyoni tangu ahamie Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako anatarajiwa kupitishwa kuwania urais.

Watu wa karibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, wameliambia JAMHURI kwamba “Hali ya woga na hofu na unyonge kwa Lowassa, imeondoka. Ana amani. Anacheka, anafurahi. Simu za ajabu ajabu na vitisho, hazimgusi tena.”

Mmoja wa wasaidizi hao aliyezungumza na JAMHURI, anasema kwamba mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz alimng’ang’ania Lowassa hadi sekunde ya mwisho kabla ya kwenda Hoteli ya Bahari Beach kutangazwa mwanachama mpya wa Chadema.

“Hadi asubuhi ya Jumanne Lowassa alikuwa na Rostam ambaye wakati wote alimsihi asiondoke CCM, lakini Lowassa alijipima kwa muda mrefu, na kufanya uamuzi alioufanya. Kuondoka CCM,” anasema.


Chanzo: Jamhurimedia

17 comments:

  1. Edward lowasa anaitwa fisadi kila kona kwasababu ya kashfa ya Richmond vinginevyo hasingekuwa anaonekana fisadi na kizuri ni kwamba alijiuzuru kupisha uchunguzi na kizuri zaidi wahusika halisi wamefahamika,kwahiyo kama anavyosema lowasa mwenye ushahidi kuwa yeye ndo mwenye richmond aende mahakamani sasa,vinginevyo huyu jemedari apewe ridhaa aitoe nchi hii kwenye umaskini wavkutupwa

    ReplyDelete
  2. Binafsi si mwanachama wa chama chochote, sina ushabiki na kiongozi yeyote lakini tuseme tu ukweli katika nchi yetu kuna kitu chochote kinachoweza kupita bila kuidhinishwa na rais??? Jibu litakuwa hakuna. Tusiwe wepesi wa kusahau, kipindi cha David Jairo alivyowahonga waandishi wa habari ili bajeti ya wizara ipite, tuliona bungeni wabunge wa upinzani na wale wa kundi la CCM wenye kupenda mabadiliko na kuchukia rushwa walitaka David Jairo afukuzwe kazi....Waziri mkuu Pinda alikuwa tayari kumsimamisha na hata kumfukuza kazi(kimsingi uwezo huo waziri mkuu alikuwa nao) lakini Rais Kikwete akiwa ziarani Afrika Kusini alikataa David Jairo asiwajibishwe hadi yeye arudi TZ, je alivyorudi ilikuwaje? Jairo bado hakuwajibishwa. Sasa suala la Richmond lipo wazi alivyoeleza Lowassa hakuficha kitu...kuanzia process yote ilivyokwenda na yeye kama waziri mkuu aliipinga lakini bwana mkubwa akakataa baada ya kuwasiliana na washauri wake (kwa waziri mkuu hiyo ni big insubordination) Ninamfahamu rais Kikwete nimefanya naye kazi kwa miaka mingi, rais wangu huyo ana ile hulka(siwezi kuita tabia..maana inabadilika badilika)ya kuonyesha kwamba yeye ni mwema kwa kila mtu ndiyo maana unamuona kwenye social gatherings nyingi....anachotaka watu wafahamu ni kuwa yeye si mbaya (culture hii ina ubaya wake...kunakuwa na utendaji wa kazi usio sahihi)Lowassa alisemwa kama fisadi wakati wa kujiondoa magamba akiwa pamoja na Andrew Chenge na Rostam Aziz lakini walishindwa kuthibitisha ni kwa vipi yeye ni fisadi.... Kwa Richmond scandal?? au kwa kitu kingine?? Maelezo ya Richmond yanajitosheleza wala hayana hata chembe ya wasiwasi (hata kama waziri au waziri mkuu alikubaliana nayo kitu ambacho hakukubaliana nacho, basi serikali yote ikiongozwa na rais Kikwete ilipaswa ijiuzulu lakini mbona hakujiuzulu??) Kwenye kikao cha kamati kuu Dodoma 2011 nakumbuka Lowassa aliongea wazi kuwa "Mwenyekiti wewe unafahamu suala la Richmond na jinsi mchakato ulivyoenda na mimi nia yangu ya kuvunja mkataba" Mwenyekiti Kikwete aliangalia chini kwa soni akasema " Tuachane na hilo tuendelee na agenda nyingine" je alikuwa na maana gani? Nimesikia watu wakisema Lowassa ni tajiri sana....Lakini hakuna ambaye anajitokeza wazi akisema utajiri wake unahusu nini au akaunti zake zikoje....sijawahi kusikia. Tanzania kuna matajiri wengi tu wengine wameibuka kwa chini ya mwaka mmoja lakini hakuna anayehoji, Lowassa amefanya kazi serikalini miaka nenda rudi...jamani hata nyumba nzuri asiwe nayo???? Kina Lwakatare wana nyumba nzuri za mabilioni na mashule mengi lakini hakuna anayesema chochote...Ezekiel Maige aliyekuwa waziri wa maliasili na wengine wengi wana nyumba nzuri kule beach Dar lakini hakuna anayesema chochote, Pinda mwenyewe ana mashamba makubwa huko Kibaoni, MPANDA hakuna anayesema, Kikwete mwenyewe ana biashara nyingi na mali nyingi hadi ameshindwa kuweka wazi kwenye kamati ya maadili hakuna anayesema chochote, Ridhiwani Kikwete kila mara anatoa misaada ya mabilioni ya shilingi kwenye jimbo lake la Chalinze lakini hakuna anayeliona hilo. Kwenye mabilionea walioweka fedha USWISI jina la Lowassa HALIPO......SASA HIZO PESA ZA LOWASSA ZIPO WAPI? Kuwa na mtoto mwenye nyumba Uingereza ya dollar laki mbili sidhani kama ni issue, watanzania wengi sana walioko nje ya nchi hasa UK, USA, AUSTRALIA, CANADA,HOLLAND etc wana majumba ya thamani zaidi ya hiyo mnayoisema ya mwanawe na wanalipia MORTGAGE ingawa wengine wamelipa na kukabidhiwa nyumba zao. JAMANI TUWE FAIR KWA KILA MMOJA TUSIPENDE KUONGEA TUSICHOKIJUA.

    ReplyDelete
  3. Duh nimependa hii story. Jamaa u mtumishi wa mungu au kazini wa Lowasa? Kweli kabisa Watanzania tunapenda kushutumiana kwa kila kitu. Hadi hii leo si ccm au upinzani walioweza kumshitaki Lowasa wala hata kufungua kesi walau kwenye mahakama za mwanzo. Na waziri yeyote ambaye hawezi kutumia cheo chake kuwa na nyumba nzuri au kuwasomesha watoto wake au kuendeleza jimbo. Lake basi huyo hafai hata kuwa karani wa office ya katibu tarafa. Hongera saana Lowasa na mdau hapo juu.

    ReplyDelete
  4. ESCROW NI MOJAWAAPO YA MIFANO YA KUANGALIA TENA YA MAJUZI TU. KWELI KASHFA KUBWA KIASI HIKI RAIS ULIYEBEBA DHAMANA YA WATANZANIA NA UCHUMI WA NCHI UNYAMAZE KIMYA. KWA NJIA MOJA AU NYINGINE UMEWEKA MKONO. YA RW 1 WALA USIOMBE.

    ReplyDelete
  5. Narudia kusema hili na sitochoka kusema, lowassa ndie mpangaji wa dhulma na kila aina ya wizi serikalini kwa kupitia group yao inayojiita wana mtandao akiwemo rostam aziz, nazir karamagi, mzee mengi na wengineo. Wewe unaehoji kwanini hajashitakiwa inabidi ujiulize ni nani aliemtuhumu lowassa fisadi. Lowassa aliwajibika kwa kukutwa na tuhuma za kuingia mkataba ulioisababishia serikali hasara lkn chadema ndio waliosema lowassa ni mwizi tena yupo ktk listi ya watu 11 walioifilisi tanzania jina lake likiwa namba 3. Na chadema wakasema kama anabisha aende mahakamani kwani wana ushahidi lkn lowassa hakwenda kinachomaanisha aliogopa ushahidi wa chadema sasa leo chadema hao waseme msafi na sisi tukae kimya? Lowassa hafai hata kuwa mlinzi wa shule achilia urais. Alitoka ccm akasema demokrasia imebakwa sababu hakupewa nafasi ya lujitetea lkn ameingia chadema amevunja utaratibu wa siku zote ambapo wagombea wanachukua fomu kisha wanapigiwa kura na mkutano mkuu sasa yeye kwa kuogopa kupingwa akawapa sharti chadema akishachukua fomu yeye zoezi lifungwe. Na pia mkutano mkuu ukazuia kura za siri ili kuepuka asipigiwe za hapana nyingi hivyo mbowe akaweka udikteta wake na kusema eti wanaomkubali awe mgombea wa ukawa wanyooshe mikono juu. Yaani huo ni uhuni wa kutupwa na ubakaji wa demokrasia, mgombea urais anachaguliwa kama monitor wa darasani? Kuweni wa kweli nyie wachaga ukawa wamechemsha na lowassa hatoshinda na ndio mwisho wake na mwisho wa upinzani bongo kwa kifupi ameenda kuumaliza upinzani.

    ReplyDelete
  6. HAHA! Mnahangaika, mnatapatapa,mnajikanyaga kikauli yaani total flip flopping. Kwani aliemtuhumu lowasa kuwa ni fisadi ni nani? Kitu gani kilicho mfanya Dr slaa ajiuzulu chadema? Huyo mnafiki Lisu na hao maprofesa uchwara wote wababaishaji. Nyinyi wenyewe mnaotumia nguvu kubwa za kuukanusha ufisadi wa lowasa ndio mliouvumbua na ushahidi wa kila namna upo kutoka katika kumbi za bunge mpaka kwenye mikutano ya mihadhara, video zote za kauli zenu zipo sasa mnabisha nini. Waswahili wanasema usieke tamaa mbele kila siku fikiria na mauti vile vile. Suburini kampeni zianze mtakiona kilochomfanya kuku ashindwe kuruka maana sioni point ya maana mtakaoitoa watu wskufahamuni. Nyinyi ni wababaishaji wakubwa na matapeli wa kisiasa na watanzania watawaadhibu ipasavyo .

    ReplyDelete
  7. NAANZA KWA KUCHEKA SAAANA KUONA HATA WANAOITWA WASOMI WAMEGEUKA MAMBURURA KWA KUJENGA HOJA DHAIFU NA ZILIZOKOSA MASHIKO KTK KUMTETEA MWIZI NA MBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA LOWASSA, UKWELI NI KWAMBA LOWASSA NI JAMBAZI LA KIMATAIFA NA NDIE MRATIBU WA KILA TUKIO KUBWA LA WIZI LILIWAHI KUTOKEA SERIKALINI BILA YA KUJALI ALIKUA KTK NAFASI GANI NA ALIFANYA HAYO KWA KUSHIRIKIANA NA WENZIE WALIOKUA NA KUNDI LAO MAARUFU KAMA WANA MTANDAO. NDUGU YANGU UNAESEMA KWANINI HAKUSHITAKIWA INABID URUDI DARASANI. CHADEMA WALIPOTAJA LISTI YA MAFISADI PAPA 11 AMBAO NI HATARI NA WAMEIFILISI NCHI JINA YA HUYO LOWASSA LILIKUA LA 3 NA KWA MSISITIZO CHADEMA WAKASEMA WANA USHAHIDI WA KUTOSHA NA KAMA LOWASSA ANABISHA AENDE MAHAKAMANI LKN HAKWENDA JE NINI MAANA YAKE WKATI AKIJUA BAADAE ATAKUJA KUGOMBEA URAIS? MAANA ALIOGOPA USHAHIDI WA CHADEMA UNGEMUUMBUA LKN KWA KUTUMIA UROH WA PESA WA MBOWE NA UMBUMBUMBU WA BAADHI YA VIONGOZI WA UKAWA NDIO 8AKAINGIA HUKO NA KUPEWA NAFASI MARA MOJA KWA KIGEZO ATASHINDA HALAFU WALIOMCHAFUA SASA WANAANZA KUMSAFISHA. ILA WENYE AKILI TIMAMU NA WASIOTAKA RUSHWA AKINA LIPUMBA NA SLAA WAMEKAA PEMBENI NA NMNYIKA ALIJARIBU AKAPEWA PESA AMERUDI KUNDINI. UKWELI HUYO MTU WENU HAKUNA SABUNI INAYOWEZA KUMSAFISHA NA HAFAI HATA KUWA 8MLINZI WA SHULE ACHILIA MBALI URAIS. TIZAMA KAULI ZAKE ZINAVYOONYESHA UDHAIFU WAKE. (1)NIKISHINDA NITAUNDA SERIKALI RAFIKI NA BODABODA NA MAMA NTILIE. JE NCHI YETU INA WATU WA AINA HIZO TU? (2) NACHUKIA UMASIKINI HIVYO NATAKA WATU WOTE WAWE NA PESA KAMA MENGI NA BAKHRESA. JE WEWE TAYARI UMESHAWAFIKIA? (3) NIKISHINDA KILA MTU ATAKUA NA NYUMBA YAKE. MONDULI ULIPOKUA MBUNGE KWA ZAIDI YA MIAKA 20 NI WATU WANGAPI WANA NYUMBA ZAO? NA WANGAPI WANALALA KTK MABOMA YA NG'OMBE? LOWASSA NIKWAMBIE KITU, KIONGOZI SHUJAA NA MWENYE UCHUNGU KWA TAIFA LAKE NI YULE AMBAE YUPO TAYARI KUTOKA KATIKA CHAMA AMBACHO ANAKIONA HAKINA NIA NJEMA NA NCHI TENA KWA KUACHIA MADARAKA YOTE ALIYONAYO. SIO USUBIRI UMESHINDWA KURA ZA MAONI NDIO UNAANZA NGONJERA JE UNGESHINDA UNGESEMA CCM WEZI WA KURA? CCM HAKUNA DEMOKRASIA? JK AMEUA UCHUMI? MAANA UMEKUA UKIMSIFIA SANA JK HUKU UKISEMA HAMJAKUTANA BARABARANI NA KAMWE HAKUNA WA UWAGOMBANISHA, PIA ULISEMA CCM NDIO CHAMA CHAKO NA HAKUNA SEHEMU NYENGINE YA KWENDA ASIEKUTAKA AHAME YEYE. LEO STORI IMEBADILIKA. NA NYIE CHADEMA, UKAWA NA VILAZA WENGINE INGEKUAJE KAMA CCM INGEMPITISHA LOWASSA KUGOMBEA MNGESEMA CCM WAMEFANYA VIZURI? MNGESIMAMA MAJUKWAANI NA KUMTETEA LOWASSA SIO FISADI? AU NDIO MNGETUMIA KASHFA ZAKE KUOMBEA KURA KTK KAMPENI? TANZANIA YA LEO SIO YA JANA MSIFIKIRI WATU BADO WANAUMWA KUSAHAU. YEYE OKTOBA NDIO MWISHO WAKE KISIASA LKN KINACHOUMA ZAIDI NI KWAMBA PIA NDIO ITAKUA MWISHO WA UPINZANI BONGO. MNAKWENDA HATUA MBILI MNARUDI KUMI NA KUJIPONGEZA BILA YA KUZINGATIA HATUA NANE MLIZOPOTEZA. R.I.P UKAWA.

    ReplyDelete
  8. Wakati wa recession USA, rais Kikwete alitaka serikali itenge U.S dollar 1.7 billion kama Shillingi Trillioni 2.6 kwa wakati ule ili kulipa makampuni yaliyoathirika na mtikisiko wa uchumi, kuna anayefahamu makampuni gani yalilipwa ? Na kama hizo fedha zilirejeshwa hazina? Ninavyoelewa na ndivyo ilivyo hakuna nchi ya Africa na zinazoendelea zilizoathirika na mtikisiko kama alivyosema Kikwete......nchi kubwa ndizo zilizoathirika kwa sababu ziliwekeza sana katika sekta za ujenzi wa nyumba halafu kukawa hakuna biashara......sasa kwetu tuliathirika vipi wakati uwekezaji wetu ni negligible? Hizo pesa zilikwenda wapi? Hakuna majibu!! Kwa hizo fedha tungeweza kujenga barabara nzuri zaidi ya kilometa 4000 lakini wajanja wamekula. Ndiyo huyo Kikwete mnayemtetea??

    ReplyDelete
  9. Wote wezi yeye na kikwete alikua wapi asiyaseme hayo tangia mwanzo akiyeshikwa na ngozi ndiye mwizi ikulu haiingiiiii hata ajisafishe vipi aseme Majumba ya ubalozi Sauth africa kanunua na pesa zipi?

    ReplyDelete
  10. Annoy.2, unaonekana ni hypocrite. Kwa nini wewe unalitaja jina la Rais Kikwete ambaye unadai umefanya naye kazi miaka mingi na unajaribu kumpaka matope, wakati unajificha (anonymity). Itakuwa fair game tulijue jina lako ili nasi tuchimbe na kuona yale mema na maovu uliyoyafanya katika wadhifa wako kwaTaifa.. Fair game? Play it then, by revealing your identity!

    ReplyDelete
  11. Jina langu ni mfichua maovu ukitaka kunijua zaidi ingia Google

    ReplyDelete
  12. Annoy wa pili 10.03am kula tano,umeongea point,hakuna asiye fisadi huko ccm ,wote wameoza,muacheni baba wa watu lowassa

    ReplyDelete
  13. Ndugu zangu watanzania nitajaribu kuweka muhutasari tuu wa hili suala zima la Lowasa na mbio za IKULU. Lowasa akiwa Waziri mkuu akiwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Kiserikali Bungeni na Wizara zote ziko chini yake, hawezi kukwepa ukweli kwamba anahusika na mkataba wa Richmond kama mwenyewe anavyokubali kuwa aliona mapungufu ndani ya mkataba mzima lakini kwa kukosa umakini katika uongozi wake akaacha pesa za umma zipotee tu kwa uoga wa kupoteza wadhifa na marupurupu yake kama Waziri Mkuu. Anasema katika waraka wake hapo juu kuwa eti Kikwetwe ndiye muhusika mkuu wa Ufisadi wa Richmond, Tuhuma hizo hata kama zina ukweli samahani zinaonyesha kuto komaa kiuongozi maana hayo alipaswa ayaseme wakati ule akishutumiwa. Hiyo ingemjengea heshima kubwa sana maana angekuwa ameonyesha ushujaa na kutoogopa mtu. Anapoamua kuongea uhusika wa mamlaka ya juu sasa wakati amenyimwa nafasi ambayo kwa mawazo yake ilikuwa LAZIMA apewe hainiingii akilini ila tuu ni bora tufe wote, huo sio utawala na uongozi ambao TANZANIA inahitaji katika kipindi hiki kigumu.Nawashangaa hata hao wahadhili wa Chuo kikuu kwa kumsifia kuwa jasiri. Angethubutu kuueleza umma wa Watanzania kabla ya kujiuzulu ukweli wa mambo(maana alipewa nafasi hiyo bungeni) ingemsafisha kabisa na kwa hakika ingetuhakikishia kuwa yeye siyo tuu muhusika wa Ufisadi bali pia ana ujasiri wa kuwaumbua na kuwawajibisha watendaji wabovu bila kujali nyadhifa zao.
    Watanzania wenzangu tujiulize, je mheshimiwa huyu angepewa nafasi ya ugombea ndani ya CCM ni lini tungejua "ukweli" wa kashfa ile kubwa ya Richmond, kwa uelewa wangu ndugu huyu angebaki na hilo moyoni mwake kama ambavyo amekaa nalo miaka takriban saba. Kwa vyama vya Upinzani nimesikitishwa sana na udhaifu waliouonyesha wa kumkabidhi mikoba ya ugombea Urais mtu ambaye kwa kipindi chote alikuwa na muonekano wa Fisadi ghafla amekuwa mtu safi???? upinzani mmekosa kabisa mtu mwenye sifa zinazostahili kugombea nafasi hii kubwa ya uongozi wa nchi yetu mpaka mkangoja waliotoswa CCM. Kwa kosa hili Adhabu ambayo watanzania watawapatia kwa kuwasaliti ni kuwaaibisha kwenye kura.
    Mwalimu alituasa kwenye moja ya hotuba zake kuwa ukiona mtu anang'angania kwenda ikulu (kama ndugu Lowasa} muulizeni kuna biashara gani Ikulu? akaongeza kusema mtu huyo aogopwe kama ukoma
    MUNGU IBARIKI TANZANIA

    ReplyDelete
  14. Anonymous 9:45PM Kama unakumbuka alishasema kuwa mwanzo aliuunga mkono kutokana na tatizo la umeme wa dharura lakini mwishoni aligundua kuwa ni bomu lile lakini rais alimwambia deal liendelee hivyo alikuwa hana jinsi. Pili mimi naona EL amekomaa Zaidi kuliko unavyo mchukulia kwani ile ilikuwa 2008 na uwezi kusema bosi wako ni mwizi ilo ni kazi ya bunge kupiga kura ya kutokuwa na Imani ni rais ingebidi bunge kuvunjwa na kufanya uchaguzi upya hela hizo umetoa wapi. zaid mwakyembe alisema katika bomu lile asinge weza sema mengine kuinusuru serikali wewe unatafsiri nini hapo. Rais alitangaza wazi kuwa EL amepata ajali kazini na alimmwagia sifa kwa kitendo chake cha kujiuzuru zipo kwenye records fuatilia. jingine EL aliandika barua ya kujiuzuru na hakufukuzwa na rais. huo ni ushujaa mkubwa sana, swali la msingi la kujiuliza je hakukuwa na scandal nyingine yeyote toka wakati ule na ni nani alijiuzuru? Tembo, Escrow, hela za Ghdafi sijaona PINDA anapeleka barua ya kujiuzuru na kukataliwa mawaziri wengine walifukuzwa lakini bado wanang'ang'ania madaraka. hiyo nyimbo ya ufisadi wa EL ni mizenge ya maembe kumchafua EL pamoja na genge lake ili awe na barabara nyeusi lakini yamtokea puani.kwa kifupi EL ana akili sana na ndiye aliyemweka mkuu madarakani nataka ulifahamu hilo jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.

    ReplyDelete
  15. Wewe unayesema AMEN kwenye mjadala huu unajua maana yake?????
    Anyway
    NYERERE SAFI
    MWINYI SAFI
    MKAPA SAFI
    JK SAFI
    LOWASA SAFI
    TANZANIA SAFI

    ReplyDelete
  16. nyinyi na lowwasa tu mbona hamsemi kuhusu epa kigoda kachota mapesa kibao mpaka leo hajulikani kigoda ndio nani kama sio viongozi wa ccm

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake