Thursday, August 13, 2015

MBOWE ATOKA HOSPITALINI

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe .

By Raymond Kaminyoge. Mwananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Mbowe aliugua ghafla Jumatatu iliyopita akiwa kwenye maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kupitia tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa aliyekwenda katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu.

Mbowe akiwa na viongozi wenzake wa Ukawa, walianza maandamano katika ofisi ya Chama cha Wananchi (CUF) zilizopo eneo la Buguruni wilayani Ilala, hadi NEC na kwamba aliugua njiani wakati msafara wa Lowassa ulipokuwa ukienda katika viwanja vya Biafra vilivyopo Kinondoni.

Mmoja wa madaktari waliomtibu kiongozi huyo, Dk Tulizo Sanga alisema baada ya kufanyiwa uchunguzi na jopo la madaktari wanne ilibainika kuwa alikuwa na tatizo la uchovu, ambalo kitaalamu linaitwa `fatique’ na alitakiwa kupumzika kwa saa 48.

Jana, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema Mbowe aliruhusiwa na madaktari jana saa 6.00 mchana. “Ameruhusiwa leo (jana) saa 6.00 mchana yuko fiti na wakati wowote ataanza kufanya kazi mbalimbali za chama,” alisema Makene.

Aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi na hali ya kiafya ya kiongozi huyo na kwamba wataanza kumwona kwenye majukwaa wakati wowote.

1 comment:

  1. Mh. Mbowe. Tunakupa pole na kukuombea nguvu na afya njema kweli umefanya kazi na usichoke bado kazinipo mbele hadi kieleweke na baada ya uchaguzi October ijayo kwa lolote litakalokuwa basi bora uchukue likizo walau ya wiki mojabukapumzike na wala sio hapa Tanzania iwe nje kabisa uliwaze moyo. Mungu akuwezeshe kwa kuwapigania waTanzania. Mungu ibariki njia tunayoelekea October kwa manufaa ya walio wengi na sio wachache. Tunaomba.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake