Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji, Damian Lubuva
akitoa mada leo jijini Dar es salaam kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali
waliohudhuria mkutanoni .
Baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria mkutano ulioandaliwa
na NEC leo jijini Dar es salaam wakifuatilia mada iliyokuwa zikiendelea.
Wanasekretarieti ya maandalizi ya mkutano NEC na wadau
mbalimbali na baadhi ya waandishi
wakifuatilia mjadala kuhusu wajibu wa viongozi wa dini kuelekea uchaguzi mkuu
ujao.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji, Damian Lubuva
akiteta jambo na mmoja wa makamishna wa
Tume hiyo Prof Amon Chaligha leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa NEC
na wadau mbalimbali.
Mkurugenzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akitoa mada kuhusu mchakato mzima wa
uchaguzi na hatua zilizofikiwa hadi sasa leo jijini Dar es salaam wakati
wa mkutano wa viongozi wa madhehebu ya dini.
MWANDISHI WETU -MAELEZO-DAR ES
SALAAM
Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC imewaomba
viongozi wa dini zote kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wapiga kura bila
kuonyesha hisia za kuegemea upande wowote wa mgombea ili waweze kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi Mkuuu ujao.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kwenye Mkutano
uliofanyika leo jijini Dar es Salaam uliowakutanisha wadau hao wa uchaguzi na
kuwakumbusha wajibu wao katika jamii hususani katika kipindi hiki ambacho nchi
inaelekea katika uchaguzi mkuu.
Alisema kuwa taasisi za kidini zinaaswa kama walivyo wadau
wengine katika kipindi hiki cha uchaguzi kuhubiri amani na kuendelea kutoa
elimu kwa watanzania ili zoezi hili liishe kwa amani na kuwaacha watanzania wakiwa
na umoja na mshikamano licha ya tofauti
za kiimani zilizopo miongoni mwao.
“Tume inawataka, nyinyi viongozi wa dini, mnapotoa mafundisho ya
uchaguzi kwa waumini wenu kuhakikisha hamuonyeshi hisia za kuwa upande wa chama
chochote cha kisiasa na zaidi kuepuka kushawishi waumini wenu kuegema chama au
mgombea fulani” amesema Jaji Lubuva.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo
, Askofu Philemon Phiri wa kanisa la EAGT-Mikocheni -A ameiasa Tume hiyo kusimama katika haki, uhuru na kuhakikisha
wanatangaza washindi bila kuonyesha upendeleo ili kuivusha nchi ikiwa salama.
Mshiriki mwingine kutoka Kanisa
la Moravian Mchungaji Alamu Kajuna alisema kuwa amani ndiyo tunu kwa kila
mwanadamu, hatutegemei vurugu wakati huu
wa uchaguzi maana amani inapotoweka wanaoumia ni wananchi wakiwamo waumini wao
hivyo wao kama taasisi zinazoshirikiana na wananchi kwa karibu kuhakikisha wanatoa
elimu kwa wananchi ili tupate viongozi kwa amani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imekutano na viongozi hao na wadau wengine ikiwa zimebaki siku mbili kuanza kwa
kampeni hapo Jumamosi ijayo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
1 comment:
Asante sio kutoa mada tu ila na pia mhakikishe hayo majina yetu wapiga kura yako sahihi kwenye hilo daftari na piabkuwahisha vifaa vya kupogia kura kila kona kunakotakiwa visingizio havikubaliki na kama fedha ziko nyingi tu kama zile za ESCROW!!
Post a Comment