Friday, August 7, 2015

NISHATI YA JOTOARDHI KUNUFAISHA BAADHI YA VIJIJI MKOANI MBEYA

NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO, MBEYA.
Nishati ya Jotoardhi imeelezwa kuwa muhimu kwa maeneo ambayo utafiti ulishafanywa hapo awali kwani ina faida lukuki kwa maendeleo ya nchi hususani katika kutatua changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme ikiwemo umeme wa mgao ambao unazikumba baadhi ya mikoa hapa nchini.

Akiongea wakati wa Kampeni endelevu kuhusu jotoardhi 6 Agosti, 2015 katika Kata za Ilomba vijiji vya Ituha na Tonya pamoja na Kata ya Nanyala iliyopo Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Meneja Mkuu wa Shirika la Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe amesema kuwa jamii hainabudi kuonyesha ushirikiano na Serikali pamoja na Kampuni ya TGDC ili kuwepo na uelewa juu ya nishati hiyo na kuleta maendeleo nchini.

"Niwahakikishie kuwa nishati hii ni nzuri kwani itasaidia kutatua changamoto tulizonazo katika uoande wa nishati, hivyo niwasihi kuonyesha ushirikiano baina ya Serikali yetu pamoja na Kampuni hii ili juhudi hizi zizidi kuendelea na kutuletea maendeleo katika maeneo yetu", alisema Njombe.

Mhandisi Njombe aliongeza kuwa TGDC imedhamiria kuzalisha umeme wa Megawati 200 jambo ambalo litasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuuondoa mgao kwani kwa sasa mkoa wa Mbeya pekee unatumia Megawati 40.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Kiufundi toka TGDC, Bwana Taramaeli Mnjokava ameeleza kuwa, jotoardhi ina matumizi mengi ikiwemo matumizi ya moja kwa moja kama vile katika uzalishaji wa samaki kwani samaki hupendelea maji yenye uvuguvugu kiasi, hivyo endapo wanambeya watajikita katika kutengeneza mabwawa ya samaki, maji ya jotoardhi yanasaidia katika kuzalisha samaki kwa wingi na hatimaye kuongeza pato kwa taifa.

"Matumizi mengine ya maji yatokanayo na jotoardhi ni kwamba, maji haya yanaweza kutumika katika Vitalu shamba kwa kiingereza huitwa Green Houses, sasa kwa maji haya tunaweza kuzalisha mboga mboga pamoja na maua jambao ambalo litaweza kutuongezea kipato.
Mjiolojia Mwandamizi toka Wizara ya Nishati na Madini, Bwana Jacob Mayalla akiwaelezea wanakijiji wa Ituha na Tonya hitoria ya tafiti za jotoardhi nchini 6 Agosti, 2015.
Meneja Mkuu wa Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi, Mhandisi Boniface Njombe (alovaa kofia) akiwaelimisha wanakijiji cha Ituha na Tonya juu ya jotoardhi nchini 6 Agosti, 2015 mkoani Mbeya.
Baadhi ya wanakijiji wa Ituha na Tonya wakifuatilia mada kwa makini zikizotolewa na watendaji wa TGDC 6 Agosti, 2015 mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa masuala ya Kiufundi toka TGDC, Bwana Karamaeli Mnjokava (alovaa koti) akiwaeleza wanakijiji cha Ituha na Itonyajuu ya faida za jotoardhi nchini 6 Agosti, 2015 mkoani Mbeya.

PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake