
Leo nataka kuzungumzia ile hali ya mtu kutokea kumpenda mtu ambaye tayari yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi. Hilo limekuwa likitokea sana huko mtaani, unakuta kijana anampenda sana mke wa mtu kiasi cha kutamani aachike amuoe yeye.
Si hivyo tu, unakuta mwanamke anatokea kumzimikia mume wa mtu na kuhisi yeye ndiye alistahili kuolewa na mwanaume huyo kutokana na namna anavyompenda.Hali hiyo husababisha hata wengine kufikia hatua ya kuwatongoza watu walio kwenye uhusiano wakieleza kuwa, wameshindwa kuzuia hisia zao.
Swali ni je, ni sahihi mwanaume kumtongoza mwanamke ambaye anajua wazi kuwa ana mume wake? Je, inakubalika mwanamke kueleza hisia zake kwa mume wa mtu au mpenzi wa mtu?
Maswali haya wapo ambao watajibu kirahisi tu kwamba, siyo sawa hata kidogo na kibinadamu na hata kimaadili ya Kitanzania siyo kitu kinachokubalika.
Usahihi ni kwamba, hata kama unampenda vipi, kama ameshawahiwa, wewe huna sababu ya kumtokea na kumwambia unampenda. Ukifanya hivyo utaonekana wewe ni mwizi wa mapenzi usiyeheshimu uhusiano wa wenzako.
Ndiyo! Kwa nini ufikie hatua ya kumtokea mtu ambaye ana mtu wake? Kwani wa kuwapenda wameisha? Usifanye hivyo, hilo ni kosa kubwa hata kama ni ukweli ulio wazi kwamba unampenda sana.
Lakini sasa, wakati ukweli ukiwa hivyo, naomba niseme kwamba kamwe haiwezi kuwa dhambi wewe kumpenda mtu ambaye ana mpenzi wake. Ndiyo, siyo dhambi kabisa kwa kuwa, mtu huzuiwi kupenda!
Litakuwa ni tatizo tu pale ambapo utamlazimisha mtu ambaye ana mpenzi wake kuwa na wewe. Unakuta jamaa anajua kabisa msichana f’lani ni shemeji yake kwa rafiki yake lakini kwa kuwa anahisi yeye ndiye mwenye mapenzi ya dhati kwa binti huyo, anaanza kutangaza sera chinichini, tena wakati mwingine kwa kumponda rafiki yake.
Inapofikia hatua hiyo, wewe unayefanya hivyo lazima utakuwa unabeba dhambi kubwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba, wengi wanaingia kwenye uhusiano na wengine kuoana kabisa lakini mmoja akawa hana mapenzi ya kweli na mwenzake wake.
Ndiyo maana tunasema, siyo dhambi kumpenda mpenzi wa rafiki yako kwa kuwa inawezekana hata huyo rafiki yako ana mtu mwingine ambaye anampenda zaidi kuliko huyo mpenzi wake.
Nini ufanye unapotokea kumpenda mpenzi wa rafiki yako? Kwanza, jua siyo jambo linaloweza kumfurahisha rafiki yako endapo atajua kuwa unampenda mpenzi wake. Akijua unaweza kuwa mwisho wa urafiki wenu lakini usishangae pia akakudhuru.
Kwa maana hiyo basi, ukijihisi unampenda mtu ambaye ana mtu wake, fanya kila uwezalo uzizuie hizo hisia zako. Baki na siri moyoni mwako, muache huyo unayempenda aendelee na maisha yake.
GPL
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake